Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa Profesa Adolph Mkenda, Mbunge na Naibu wake Mheshimiwa Omari Kipanga, Mbunge na wataalamu wa Wizara kwa kazi nzuri wanazofanya kwenye kutekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia kuhusu maboresho ya kimkakati yanayohitajika katika sekta ya elimu ya juu Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu bora ni msingi wa maendeleo ya Taifa na Tanzania, inapaswa kufanywa juhudi za makusudi na kimkakati kukabiliana na changamoto zinazoikumba sekta ya elimu, ikiwemo elimu ya juu hapa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti umeonesha kwamba elimu ya juu ndiyo inayotoa dira na mwelekeo wa kitaifa juu ya maendeleo. Hapa duniani, nchi nyingi zilizopiga hatua kubwa kwenye maendeleo ni nchi zilizofanya mapinduzi makubwa kwenye elimu ya juu. Kwa mfano, nchi za Marekani, China, Canada, Japan, Uingereza, Australia, Urusi, Ujerumani ni nchi zenye uchumi mkubwa. Nchi hizi zina vyuo vikuu vyenye hadhi kubwa duniani vilivyo kwenye orodha bora kutokana na tafiti wanazofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika hata katika Bara la Afrika, vyuo vikuu vyenye hadhi kubwa katika kumi bora vingi zaidi vinatokea Afrika Kusini ikifuatiwa na Misri, na haya ndiyo Mataifa yenye uchumi mkubwa Barani Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upimaji wa ubora wa Vyuo Vya Elimu ya Juu vya Tanzania kwa kuzingatia vigezo vya Kimataifa, vyuo vyetu havijafanya vizuri. Kwenye Bara la Afrika, kwenye vyuo bora 100, Tanzania inashika nafasi ya 26 na ya 1,614 duniani (Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam) ikifuatiwa na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine) ambacho kipo nafasi ya 53 Afrika na ya 2,634 duniani na Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili ambacho kipo nafasi ya 95 Afrika na cha 3,667 duniani (https://edurank.org/geo/af/).

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hii, nachelea kusema kwamba hali hii inaweza kufanana na kasi ya maendeleo ya Taifa letu. Hivyo basi, ili kulikwamua Taifa letu kama wenzetu wa nchi zilizoendelea walivyofanikiwa, ni vyema tukaangalia mahali pa kuanzia kwa kuwekeza kikamilifu na kimkakati ili kutatua changamoto zinazokabili vyuo vya elimu ya juu Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza hapo juu, kuna uhusiano mkubwa sana kati ya elimu ya juu na maendeleo ya nchi. Nalisema hili kwa sababu gunduzi kubwa duniani zenye mchango mkubwa kwenye maendeleo ya dunia hii zinafanywa na taasisi za elimu ya juu. Ni kwa maana hiyo napenda nisisitize hapa kwamba nchi yetu isipowekeza kimkakati katika elimu ya juu, itabidi tusahau kabisa kuhusu maendeleo ya nchi yetu, kwani hatutaweza kutatua matatizo ya kawaida ya wananchi wetu katika nyanja za afya, kilimo, mifugo, uvuvi, maliasili (maji, madini, utalii, nishati), utalii, ujenzi, viwanda, biashara, mazingira, ardhi, ulinzi na mambo mengine muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kulinufaisha Taifa na elimu ya juu, naishauri Serikali ichambue haya mapendekezo ya kimkakati ili kuondoa baadhi ya changamoto zinazokwamisha maendeleo ya vyuo vya elimu ya juu Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza Serikali ifanye maboresho ya Sera ya Elimu na Utafiti wa Vyuo Vya Elimu ya Juu nchini. Pia napendekeza kwamba Serikali iandae sera maalumu ya kuunganisha elimu ya juu na maendeleo ya Taifa letu kwa kuzingatia mipango ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kuboresha Sera ya Elimu ya Juu, ni vyema wakashirikishwa wadau wote muhimu kama wanachuo walio vyuoni, waliohitimu, walio kwenye ajira katika sekta husika na wadau mbalimbali wa maendeleo. Kushirikisha wadau wote hawa kutapanua wigo wa kugundua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza Serikali ifanye mapitio na maboresho ya mitaala ya vyuo vya elimu ya juu nchini. Ushirikishwaji wa wahitimu walioko kazini pamoja na wakufunzi katika mapitio ya mtaala ni muhimu ili kuamua ni vipengele gani vibaki, viongezwe au viondolewe. Mapitio haya yalenge kufundisha vijana wetu vitu vitakavyosaidia kujenga Taifa lenye maarifa, ustadi na uwezo wa kushindana katika uchumi wa kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza kwamba kimkakati vyuo vya elimu ya juu nchini viwe na ushirikiano wa moja kwa moja na Halmashauri za Serikali za Mitaa. Ni jambo la heri kuhusisha vyuo vikuu katika shughuli za maendeleo ya Halmashauri za Serikali za Mitaa. Kwa kufanya hivyo, watakuwa wanajihusisha moja kwa moja na maendeleo ya wananchi na changamoto ya tafiti za wanazuoni wetu kubakia makabatini itakuwa imetatuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhuisha ari ya utumishi miongoni mwa wahadhiri wa vyuo vya elimu ya juu, Serikali ihakikishe kuwa katika bajeti zake zote madeni yote ya wanataaluma ya posho ya pango kwa wanaostahili yanalipwa, posho za kujikimu wanapokuwa kwenye majukumu na mpango wa kuboresha mafao ya wahadhiri ya uzeeni unatekelezwa kikamilifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la azma hii ni kuwaondolea hofu ya maisha yao ya kila siku wanataaluma wetu ili waweze kujikita kweli katika kutoa elimu, kufanya utafiti kwa utulivu, na kutoa ushauri wa kitaalam ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya changamoto kubwa katika elimu ya juu ni uhaba wa wahadhiri wenye sifa stahiki ili kuendana na ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na vyuo kufanya tafiti na ubunifu. Taarifa mbalimbali zimeonesha kwamba vyuo vyetu vikuu vya umma nchini vina uhaba mkubwa sana wa maprofesa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, ili kuendelea kufaidika na utaalamu na uzoefu wa maprofesa wetu hapa nchini, nashauri kuwa Serikali iangalie uwezekano wa kuongeza umri wa maprofesa kustaafu kutoka miaka 65 ya sasa hadi 70, na kwa wale wenye uwezo wa kufundisha, waruhusiwe kupewa mikataba hadi wanapofikisha umri wa miaka 80. Hili liamuliwe na taasisi husika maadam wamejiridhisha kuwa profesa husika bado utaalamu wake anautumia kikamilifu na unahitajika kwa wakati huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema Serikali ikatoa fursa kwa vyuo vya elimu ya juu kujiendesha kiutawala na kitaaluma, bila kuingiliwa na mamlaka nyingine za Serikali. Hii iwe ni pamoja na uhuru wa kuajiri watumishi wa kada za elimu kwa vipimo walivyojiwekea bila kuingiliwa na mamlaka zisizo za kitaaluma.

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza Serikali ifadhili kikamilifu tafiti za kimkakati, ubunifu na kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti hizo yanatumika katika kuanzisha viwanda hapa nchini. Ni vyema watafiti wa vyuo vya elimu ya juu wakajengewa mazingira bora na kupatiwa ufadhili wa fedha za kutosha kufanya tafiti na bunifu mbalimbali. Serikali ikiwekeza kikamilifu kwenye hili, bunifu za watafiti wetu zitaingia sokoni na kuliletea Taifa letu maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hizi zinahitaji kushughulikiwa ili kufikia lengo la elimu yetu ya juu kuchangia katika maendeleo ya kijamii na uchumi katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.