Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Mashimba Mashauri Ndaki

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada anazozifanya ili kuhakikisha watoto wetu wanasoma kwenye mazingira mazuri, na walimu kuboreshewa mishahara na mafao yao mengine. Hongera sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana pia Mheshimiwa Waziri wa Elimu Profesa Mkenda, kwa kazi nzuri ya kuhakikisha Wizara ya Elimu inasimamiwa vilivyo ili kupata rasilimali watu walio bora kwa maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa mchango wangu kwa Wizara ya Elimu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naipongeza Wizara kwa kuja na mwongozo wa utambuzi wa vipawa na vipaji kwa wanafunzi wa shule zetu. Ushauri wangu ni kuwa mwongozo huu uwe jumuishi kwa maana ya kwamba utambuzi usiishie kwa wanafunzi mashuleni tu, bali uende mbali mpaka kuwatambua watu wazima wanaofanya mambo kwa kutumia vipawa na vipaji vyao vya kubuni mambo au vitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, tuna watu wazima wana kipaji cha kutengeneza bunduki, sera na sheria zetu zinazuia ubunifu wa aina hii na watu hawa wakipatikana wanakamatwa na kuhukumiwa kufungwa kwamba wamevunja sheria zetu. Kwa nini tusifikirie kuwa na watu hawa kwenye kambi maalumu za ufundi na kuendeleza vipaji vyao na kuwatumia hatimaye kufanya mambo makubwa baadaye?

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwangu mimi naona ni wakati muafaka sasa kwa Wizara ya Elimu kuwa Wizara ya Muungano, kama ilivyo kwa Wizara ya Mambo ya Ndani, Mambo ya Nje na kadhalika. Hoja yangu ni kuwa tangu enzi za kupata uhuru elimu imetumika kama nguzo mojawapo iliyotuunganisha Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wa Kanda ya Ziwa walisoma Kusini na Kaskazini na Watanzania wa Kusini walisoma Shule za Kanda ya Ziwa na Kaskazini mwa nchi, na hivyo hivyo wa Magharibi walisoma Mashariki na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu likiwa jambo la Muungano litafanya Utanzania wetu kuwa na mshikamano na umoja zaidi na hivyo kufanya Taifa letu kuwa moja lenye watu wamoja. Kwa maana hiyo, Watanzania walioko Pemba au Unguja watakuja kusoma Bara na Watanzania wa Bara hivyo hivyo kwenda kusoma Zanzibar hasa kuanzia kidato cha tano na sita na vyuo vikuu, na hivyo kuwafanya Watanzania wa Bara na wa Visiwani kutokuwa na utofauti wowote, na hivyo ku-cement zaidi umoja wetu wa Kitaifa.