Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, jana kwenye mchango wangu wa kuzungumza nilikatizwa na hivyo sikuweza kumalizia. Naomba kutoa na kusahihisha maneno yangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu maombi ya ujenzi wa vyuo vya elimu ya juu katika Wilaya ya Mbozi na Jimbo la Vwawa wananchi wa Kata ya Ipunga wametenga eneo litakalotolewa bure kwa taasisi yoyote itakayokuwa tayari kujenga chuo cha elimu ya juu. Eneo lina ukubwa wa ekari 308. Tupo tayari kulitoa bure na lipo tayari. Naomba Mheshimiwa Waziri akubali kupokea eneo hilo ili atutafutie chuo chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye Kata za Nyimbili na Hasanga kuna eneo la zaidi ya ekari 700 linafaa sana kujenga vyuo vya elimu ya juu. Pia Ihanda kando kando ya Mlima Mazuri wa Ng'amba na Kata ya Hasanga pia kuna eneo. Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kutusaidia kupata vyuo ambavyo vitajengwa kwenye maeneo hayo ili kuchangia katika huduma za jamii na uchumi na maendeleo ya wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni kuhusu mitaala ya elimu ya juu kushindwa kukidhi mahitaji ya soko na mabadiliko mbalimbali. Naomba Serikali ichukue hatua za kuboresha mitaala ya vyuo vingi vya elimu ya juu ili iwe ni competency based kwa vitendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuhusu utafiti na machapisho ya vitabu na Makala, ni vizuri vyuo vyetu vikatilia mkazo wa kufanya utafiti na kuandika vitabu na machapisho mbalimbali. Hiyo itaboresha na kuinua hadhi ya vyuo vyetu nchini na duniani. Pia hatua hiyo itavutia wanafunzi wengi kutoka nje ya nchi na kuongeza fedha za kigeni nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri yeye na timu yake na kuendelea kutilia mkazo maeneo ya sayansi, teknolojia na hesabu kwa maendeleo ya nchi. Nchi itaendelea kama elimu yetu itawaandaa vijana hao kwa kupata maarifa na ujuzi vitavyowaandaa vizuri kujitegemea.