Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AMINA BAKAR YUSSUF: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu mpendwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wake mzuri wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, pamoja na kuleta mabadiliko makubwa katika sekta hii ya elimu nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakupongeza wewe na Spika wetu wa viwango kwa kutuongoza na kuliendesha vyema Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa umahiri na uthubutu mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wake wote wa Wizara hii kwa utendaji wao mzuri wa kazi za Wizara katika kuwahudumia wananchi na kumsaidia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango/ushauri wangu katika Wizara ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, mtaala wa elimu ya msingi na sekondari uendane sambamba na mazingira ya maeneo husika ndani mikoa ili uindane na wakati uliopo sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtaala wetu wa elimu kuanzia ngazi ya msingi hadi vyuo vya juu umwandae kijana kuweza kujiajiri na kujitegemea mara baada ya kumaliza masomo yao ili kupunguza ongezeko la vijana wasiokuwa na ajira nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali sasa iongeze jitihada zaidi katika kuboresha mazingira ya vyuo vya elimu ya kati/VETA pamoja na kujenga majengo ya VETA kila wilaya nchi nzima ili kuwasaidia vijana kuweza kupata elimu ya amali kwa urahisi zaidi, ili kupunguza wimbi kubwa la vijana mtaani na kuwaepusha na kujiingiza katika vikundi viovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iendelee kuboresha mazingira rafiki ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia hasa masomo ya sayansi nchini ili wanafunzi waweze kupenda masomo ya sayansi zaidi bila ya kulazimishwa ili tuweze kuzalisha wataalamu na wasomi mahiri wa sayansi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Wizara iandae mfumo/ mpango maalumu wa kutoa elimu ya umuhimu wa elimu ya VETA na maisha yao ili jamii ione umuhimu wa elimu inayotolewa VETA, maana kuna vijana wengi bado hawatambui umuhimu na kudharau na kuona haina tija kwao na maisha yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na ninaunga mkono hoja, ahsante.