Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafia
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia fursa ya kuweza kuchangia hoja iliyoko mbele yetu. Awali ya yote napenda kutumia fursa hii adhimu na adimu, kwanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetupa kibali cha kuweza kukutana siku ya leo mahali hapa katika muda huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani ya pili, nimpelekee Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa imani yake ambayo ameendelea kunionesha, kuendelea kuniamini mimi na mwenzangu Mheshimiwa Prof. Mkenda kuweza kumsaidia kwenye eneo hili dogo la Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais na ahadi yetu kwake kwamba, hatutamwangusha, tutahakikisha kwamba tunasimamia Wizara hii kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani nyingine ni ya kwako wewe Naibu Spika, Msheshimiwa Spika na Wenyeviti wetu wa Bunge kwa kusimamia vizuri Bunge letu hili. Shukrani nyingine ni kwa Kamati ya Elimu, Utamaduni na Michezo kwa maelekezo, miongozo na maoni yao, ambayo kila mara wameendelea kutushauri juu ya namna gani tunaweza kuisimamia Wizara yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nitoe shukrani nyingi sana kwa Wabunge wenzangu ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa kwenye Hoja ya Wizara ya Elimu. Tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, lakini tunaomba tu tuwaambie kwamba, maoni na ushauri wenu wote tumeupokea na sisi, kama wasimamizi wakuu, tutaenda kuhakikisha kwamba yale maoni tunakwenda kuyafanyia kazi sawa sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee, nitoe shukrani sana kwa Mheshimiwa Waziri, amekuwa ni mwalimu, amekuwa ni kiongozi, tumekuwa tukishirikiana kwa karibu sana. Pale Wizarani, Mheshimiwa Waziri ana msemo wake unaosema kwamba, ukitaka kwenda haraka nenda peke yako, lakini ukitaka kwenda mbali twende kwa pamoja. Kwa hiyo, ametengeneza sense of ownership, vilevile sense ya kufanya kazi kama team work. Mheshimiwa Waziri tunakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee namshukuru Katibu Mkuu, Prof. Nombo na Manaibu Wakuu wote wawili, Prof. Mushi pamoja na Daktari Mahela; Wakuu wa Idara, Vitengo na Wafanyakazi wote wa Wizara ya Elimu kwa ushirikiano ambao wanatupa katika kipindi hiki chote ambacho tunasimamia Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa niwashukuru sana wananchi wa Mafia kwa kuniamini na kuendelea kunipa ushirikiano katika kipindi chote ambacho tunatekeleza majukumu ya Kiserikali. Niwaahidi tu wananchi wa Mafia, kwa namna yoyote ile sitawaangusha, tuendelee kushirikiana na kushikamana kuwa kitu kimoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa naomba niishukuru sana familia yangu kwa ushirikiano na uvumilivu katika kipindi hiki chote wakati tunatekeleza majukumu ya Kiserikali. Baada ya utangulizi huo naomba sasa nijikite kuchangia.
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naongeza muda kidogo.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo dogo ambalo Waheshimiwa Wabunge wameleta ushauri, pamoja na hoja zao mbalimbali, eneo la kwanza ni kwenye Ujenzi wa Vyuo vyetu vya VETA, vile 64 vya wilaya na kile kimoja cha mkoa, ambayo ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba, twende tukajenge vyuo vya VETA katika maeneo yote katika wilaya zote ambazo zilikuwa hazina VETA hapo awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge wote ambao mmechangia hoja hii kwamba, sisi kama Wizara, tutasimamia kwa karibu au tumeendelea kusimamia kwa karibu na mpaka hivi leo naomba niwahakikishie tu kwamba, zaidi ya shilingi bilioni 72 zimeshatoka, zile za awamu ya kwanza kati ya zile shilingi bilioni 100 na ujenzi kule umefikia asilimia 45.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matamanio yetu kwamba utakapofika mwezi wa Kumi mwaka huu 2025 ile awamu ya kwanza ya majengo tisa tuwe tumeweza kuikamilisha, ili basi mafunzo yale ya muda mfupi utakapofika mwezi Novemba au Disemba, mwaka huu 2025 yaanze kutolewa na itakapofika Januari mwakani, 2026 kwa awamu hii ya kwanza, basi vyuo hivi viweze kuanza kutoa mafunzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge wenzangu, ujenzi wa vyuo hivi 64 unaenda sambamba na ununuaji wa vifaa. Kama mnavyofahamu, tulianza ujenzi wa vyuo vya awali kabisa, vyuo 25 vile vya wilaya vinne, vile vya mikoa na vyuo, hivi vyote vinahitaji vifaa kwa sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niwathibitishie kwamba, katika bajeti yetu ya 2023/2024 tulitenga fedha zaidi ya shilingi bilioni 2.1, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa. Vilevile tulitenga fedha, kwa ajili ya ununuzi wa vitabu katika mwaka huo huo, zaidi ya shilingi milioni 345. Vifaa hivi kwa mwaka huu, ambapo kwa fedha hizi tulizotenga, vilikuwa vimenunuliwa kwa ukamilifu wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha 2024/2025, tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 7.2. Tayari wazabuni wamepatikana kwa ajili ya usambazaji wa vifaa hivi. Vimeshanunuliwa na hivi sasa wazabuni wako tayari kwa ajili ya kuvipeleka kwenye maeneo mbalimbali ambayo tayari vyuo vimekamilika na vifaa hivi vinahitajika. Kwa hiyo, wale Wabunge wenzangu wa Ikungi, ambao walizungumza hapa habari ya zile VETA 25, vifaa vyake viko tayari na hivi sasa tunavipeleka kuhakikisha kwamba, huduma ya elimu kule inatolewa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2025/2026 tumetenga fedha katika bajeti yetu zaidi ya shilingi bilioni 2.5, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Pia, tuna mradi mkubwa wa ESPJ ambao una fedha zaidi ya shilingi bilioni 286, fedha hizi zinaenda kutumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa katika vyuo vile vya zamani 21.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, vyuo 34 ambavyo tayari ujenzi wake umekamilika vilevile vitasaidia kununua vifaa katika hizi VETA 64 za wilaya na kile kimoja cha Mkoa wa Songwe, ambavyo tunakadiria kufika mwezi wa Kumi ujenzi utakuwa umekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, vyuo 34 ambavyo tayari ujenzi wake umekamilika vilevile vitasaidia kununua vifaa katika hizi VETA 64 za wilaya na kile kimoja cha Mkoa wa Songwe, ambavyo tunakadiria kufika mwezi wa Kumi ujenzi utakuwa umekamilika. Kwa maana hiyo, vifaa vitakuwa vinahitajika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tayari tumeshajipanga vizuri, bajeti yetu hii ambayo tutaipitisha hapa leo, itakapofika mwezi wa Saba tutakapoanza kutumia kipaumbele cha kwanza tutakipeleka kwenye ununuzi wa vifaa kwa ajili ya VETA zetu hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna vyuo vyetu 54 vya FDC, navyo vilevile vitakuwa covered kwenye hii shilingi bilioni 286. Kwa hiyo, niwaondoe hofu kwenye eneo hili la ununuzi wa vifaa kwa ajili ya vyuo vyetu vya VETA, vile vilivyokamilika na hivi tunavyoendelea kujenga.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na ununuzi wa vifaa, tumeendelea kutoa ajira kwa walimu wa ufundi ambapo zaidi ya walimu 465 tayari wameshaajiriwa kwenye eneo hili. Kwa hiyo, kazi hii tunaendeleanayo Waheshimiwa Wabunge na tutaendelea kuifanya kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili lililozungumzwa hapa ni eneo la wadhibiti ubora. Tunafahamu kuwa tulifanya mabadiliko kidogo ya muundo wa Wizara kwa kuwaingiza wadhibiti ubora kuwa kama ni maafisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge kwamba wadhibiti ubora katika wilaya zote 164 walipandishwa daraja, na hivi sasa tunavyozungumza wako kwenye muundo mpya kistahiki na maslahi yao yote. Kwa hiyo zile stahiki na maslahi yao yote yamezingatiwa kwenye muundo huu mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, Wizara au Serikali imeweza kujenga ofisi mpya za wadhibiti ubora katika wilaya 165. Vilevile tumefanya ukarabati wa ofisi zile za zamani kwenye zaidi ya wilaya 30. Sambamba na hiyo, tumepeleka vifaa vya ofisi, kwa maana ya laptop, printer takribani ofisi hizo zote ninazozizungumzia. Kwa hiyo, mazingira yale ya kufanya kazi kwa maana ya wadhibiti ubora tumeyaaminisha kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumenunua magari kwa ajili ya kufanyia kazi wadhibiti ubora katika wilaya karibu zote 164…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, muda wako umekwisha.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: … kwa hiyo, wilaya zetu karibu zote za udhibiti ubora tayari zina magari kwa ajili ya matumizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nami naunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)