Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rombo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa fursa hii ya kuhitimisha hoja. Jumla ya Wabunge 36 wamechangia moja kwa moja Bungeni, na tumepata michango mingine kwa maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji wote kwa pamoja wamezungumza mambo mengi ambayo napenda kuhakikishia kwamba tunayabeba. Mengi ni ushauri ambao tutauzingatia. Kwa hiyo, naomba niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu, nawahakikishia kwamba tutazingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Husna Sekiboko, na Makamu, Mheshimiwa Mussa Sima nao wametoa taarifa yao ambayo kwa ujumla wake kwa kweli hatuna la kubisha, wala kupingananao. Ni suala ambalo tutalichukua na kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hilo tunawashukuru sana Kamati yetu kwa sababu pamoja na kwamba wakati mwingine wamekuwa wakali kidogo wakati wa kutusimamia, lakini siku zote wamefanya hivyo kwa lengo la kujenga, kuendelea mbele. Kwa kweli kama kuna mahali tumefanya vizuri sana, itakuwa ni kwa sababu ya mchango mkubwa wa Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Husna Sekiboko na Makamu wake. Naomba niwashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nielezee kwamba katika michango yote hii tuliyoisikia, kila Mbunge aliyeongea hapa pamoja na Kamati wamempongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wamempongeza kwa mengi; kwa mageuzi makubwa ya elimu ya kihistoria kwa namna fulani ukiacha yale mageuzi yaliyofanyika miaka ya 1960, sasa hivi ni mageuzi ya pili makubwa na huenda yakawa makubwa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wamempongeza kwa ongezeko la bajeti katika Wizara ya Elimu na katika sekta ya elimu kwa ujumla. Pia wamempongeza kwa kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na hata vyuo vya kati. Pongezi kwa ujenzi wa vyuo vya VETA, vyuo 64 jumlisha moja, wamempongeza Rais wetu kwa ujenzi wa shule za amali, wamempongeza Rais wetu kwa kuendelea kujenga kampasi mpya za vyuo vikuu katika mikoa mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, na ninajua Mheshimiwa hapa alizungumza Manyara ni mojawapo ya mikoa ambayo imepata kampasi ya chuo kikuu, kampasi ya taasisi ya elimu na juu. Mtwara kwa mara ya kwanza sasa watakuwa na university college, Kagera wanapata university college, Kigoma, Lindi, Tanga, Njombe, na mikoa mingine ya Singida, Tabora, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga na mikoa mingine yote ambayo ilikuwa haina kampasi ya chuo kikuu. Sasa hivi tutabaki na Mkoa wa Pwani tu ambao na wenyewe mkakati wake unafanywa. Kwa hiyo, wote wamempongeza Mheshimiwa Rais kwa haya yote na mengine mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami naungana na Waheshimiwa Wabunge wote kumpongeza sana Rais wetu kwa uongozi wake makini na ujasiri wake mkubwa wa kusimamia sekta ya elimu na kuruhusu mageuzi makubwa haya yafanyike, jambo ambalo ni rahisi sana kulikwepa na kukimbilia katika miradi mingine ya majengo, madaraja, reli na kadhalika ambayo inaonekana kwa macho kuliko mageuzi ya mfumo ambao matokeo yake yanachukua muda mrefu kuonekana. Tunamshukuru na kumpongeza sana Rais wetu kwa maelekezo yake, uongozi wake na jinsi ambavyo anapeleka Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais ambaye anamsaidia Rais na katika kutusimamia sisi; Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri wetu Mkuu ambaye vilevile anatusimamia katika utekelezaji wa kazi siku hadi siku; na Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko ambaye naye anasaidia katika Ofisi ya Waziri Mkuu katika uongozi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi katika Wizara ya Elimu, Elimu ya Juu tunafanya pamoja mpaka upande wa pili wa Muungano na hata katika elimu nyingine hii tunashirikiana sana. Kweli na nimewahi kutembelea Ikulu ya Zanzibar takribani mara tatu katika masuala ya elimu. Namshukuru sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi kwa uongozi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda vilevile kutoa shukrani nyingi sana kwa Spika wetu, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson kwa uongozi wake wa Bunge letu, wewe Mheshimiwa Naibu Spika kwa uongozi wako jasiri na mahiri sana, pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa kutuongoza vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika yote yaliyozungumzwa, nitazungumza machache kwa dondoo. Moja, ni mageuzi na hasa suala la amali ambalo limezungumzwa hapa, kukubali kwamba inabidi tuendelee kuyasema haya mambo zaidi ili watu waweze kuyaelewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ngoja nieleze kidogo katika mageuzi ya elimu, katika suala la kuwa na mkondo wa elimu jumla na elimu ya amali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mageuzi yetu yanatusababisha sasa sekondari ya O’ Level iwe na mikondo miwili; mkondo wa elimu jumla na mkondo wa elimu amali. Nitazungumzia mkondo wa elimu amali. Elimu amali ni kile tunachokiita ufundi na ufundi stadi. Kwa Kiingereza it is technical and vocational training. Ni technical and vocational training.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, amali siyo fundi tu, lakini ufundi ni amali na ufundi stadi ni amali ingawa ufundi stadi siyo ufundi. Kwa hiyo, ule ufundi wa kihandisi ni sub-component ya ufundi ya mafunzo ya amali kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, zile shule alizozungumzia Mheshimiwa Maige hapa, kwa mfano Moshi Technical School, Ifunda Technical School, Tanga Technical School ni shule za amali ufundi. Kilosa shule ya kilimo ilikuwa ni shule, na kwa kweli haikuendeshwa kama shule ya amali kwa sababu ilikuwa bado ni elimu jumla sana na mashamba makubwa, lakini ni shule ambayo inaweza ikawa ni shule ya ufundi stadi; amali na ufundi stadi, siyo ufundi. Kwa hiyo, yenyewe inaweza ikazingatia masuala ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa hivi shule nyingi ambazo tumejaribu kuzifufua hasa hizi tisa ni zile shule za ufundi, amali ufundi. Pia tutakuwa na shule za amali kilimo, amali ukarimu, amali michezo na kadhalika na kadhalika. Hilo suala ni muhimu sana kulielewa. Katika shule za amali, sekondari za amali, baada ya kumaliza form four unapata cheti chako cha NACTVET na cheti cha form four. Ukitaka kwenda high school ya amali, iwe ni ufundi ama ufundi stadi, unakwenda high school kwa miaka mitatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ngoja nizungumzie high school ya ufundi, kama ambavyo alikuwa anaeleza Mheshimiwa Maige. Ukienda high school ya ufundi, unakwenda kwenye Polytechnique kama ilivyokuwa Dar Tech. Tunarudisha tena hapa Tanzania Polytechinical Schools. Tunajenga moja Mwanza, tunajenga nyingine Kigoma, tunajenga nyingine Mtwara, tunajenga nyingine Morogoro, tunajenga nyingine Zanzibar na tayari tuna Chuo cha Ufundi hapa Dodoma kimekamilika, na sasa hivi kimeunganishwa na Taasisi ya Ufundi Dar es Salaam, lakini nacho kitakuwa kama Polytechniques.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa wale wanaosomea elimu ya ufundi, siyo ufundi stadi, wakienda high school wakuwa miaka mitatu watapata diploma na cheti cha form six, lakini ili kuondoa tatizo lililosababisha Dar Tech ibadilike iwe taasisi ya elimu ya juu, wale wakiamua kwenda chuo kikuu kusoma engineering watasoma miaka mitatu badala ya kusoma miaka minne. Kwa hiyo, hawatopoteza tena mwaka mmoja kama ilivyokuwa wakati ule. Kwa hiyo, hii ni hatua kubwa sana, tunamshukuru Rais wetu kwa ilivyo. Narudia tena, mafunzo ya amali ni seti yenye ufundi na ufundi stadi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo limezungumzwa ni kuhusu kuweka vifaa katika shule hizi. Ni kweli kabisa, tungetamani sasa hivi tuwe na takribani nusu ya sekondari zote ziwe shule za mafunzo ya amali, lakini kwa makusudi tumeamua twende hatua kwa hatua. Shule ikiwa ni shule amali lazima iwe na uwekezaji wa kutosha. Tusipeleke shule ikawa shule ya amali halafu baadaye wazazi wakaona kwamba tunapoteza muda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna nchi moja tu tuliitembelea tuliona ilianza mageuzi kama haya yaka-collapse kwa sababu wazazi walihisi kwamba wanadanganywa. Kwa hiyo, shule hizi nyingi, pamoja na Moshi Tech na Tanga Tech, vifaa vinanunuliwa ili kuhakikisha kwamba kuna vifaa. Karakana zile zilizokuwepo zamani, nyingi sasa hivi zimepitwa na wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tulimtuma Katibu Mkuu kwenda India, ametembelea kule, tutakwenda China, South Korea, tumezungumza na Ujerumani na Switzerland kwa ajili ya kupata vifaa vya kisasa zaidi vya elimu ya ufundi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ya ufundi wakati mwingine siyo lazima utumie material na kuyamaliza. Sasa hivi unaweza ukatumia virtual training kwanza. Kama ni welding, unatumia kwanza kwa simulation halafu baadaye ndipo unakwenda kufanya actual activity. Sisi pia tunalenga kwenda huko, kwa sababu bila ya hivyo, of course itakuwa ni gharama sana kuendesha shule hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi shule tunazozijenga za amali tulizonazo sasa hivi hazitaanza kufanya kazi bila kuwa na vifaa na wakufunzi wa kutosha. Tuko tayari kwa yale maeneo ambayo hatuna wakufunzi hapa nchini, kutafuta wakufunzi kutoka nje waje kwa muda ili tuweze kuinua viwango vya elimu ambayo tutavitoa hapa nchini, ndiyo maana tunakwenda taratibu. Wako wengine wanasema tunaenda taratibu sana, wengine wanasema tunaenda haraka sana, lakini ukweli ni kwamba, ni lazima twende kwa makini vilevile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa high school nyingine za mafunzo ya amali ambazo siyo ufundi, tuna vyuo vya kilimo hapa nchini, vyuo vya mifugo, vyuo vya utalii na kadhalika. Tutavi-align vitoe fursa ya high school education, kupata diploma na kupata cheti cha form six at the same time, na baada ya hapo akitaka kuendelea wataenda chuo kikuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naomba nilizungumze, limezungumzwa vizuri sana kwa ufasaha na Mheshimiwa Prof. Muhongo, Mheshimiwa Prof. Manya na baadhi ya wachangiaji wengine. Hili ningependa nilielezee, kwanza tayari tumeanza kutoa scholarship, tumeanza kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wanaofanya master’s degree. Tuna wanafunzi takribani 80 ambao wanafanya master’s chini ya Bodi ya Mikopo katika Taasisi yetu ya Sayansi na Teknolojia, Nelson Mandela pale Arusha, kwa sababu tunataka kile Chuo kibaki kuwa ni graduates’ university, kisichanganye kuwa na undergraduate, bali ki-focus kwenye research na kufundisha watu wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni kweli kuwa kuna wakati tuliacha tu tunaletewa scholarship, tunapeleka watu bila ku-define tunataka nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tumebadilika. Kwa mfano, kwenye Tume yetu ya Atomi tumeangalia, hatuna wataalamu wa kutosha hapa Tanzania. Tulikuwa tunatafuta Mtendaji Mkuu tena hata hawapo, wengine wameshastaafu, walikuwa Makamu wa Rais, hapa alikuwa ni mtalamu wa kule. Kwa hiyo, sasa hivi tumeamua kwamba tunapeleka Watanzania kwenda kusoma nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, uwe mtumishi wa Tume, la sivyo mfanyakazi wa chuo kikuu, la sivyo Mtanzania, passport yako iwe ni ya Kitanzania. Tunawapeleka watano kwenda kufanya master’s katika masuala ya Atomi kwa sababu ni muhimu sana katika uchumi wetu. Hiyo inaitwa Samia Extended. Kwa hiyo, tunawapeleka nje kwenda kufanya post graduate.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa kuliko yote, ukisikiliza vizuri mazungumzo ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, wanakwambia the future is uncertain, technological development is going to be destructive, ita-cause dislocation kwenye labour market. Kuna watakao-gain na watakao-lose. Ambao hawajajiandaa wata-lose. Hata katika kujitawala sisi wenyewe, tunapokwenda katika akili-unde, yaani unde ni akili iliyoundwa; pengine hata neno artificial intelligence lingekuwa constructed, intelligence ingekuwa appropriate zaidi. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, akili-unde inakotupeleka sasa hivi itatukimbiza kwa kasi ambayo hatujapata kuona. Wanasema the future is so uncertain, lakini the future is already here. Sasa sisi tunafanyaje? Tayari tumeandaa kwenye bajeti hii, tumetenga shilingi bilioni tano na potentiality zitaongezeka kwa ajili ya kuwapeleka Watanzania kwenda kusoma nje masuala ya data science katika vyuo tutakavyovichagua sisi. Watakwenda kusoma first-degree na baada ya hapo wanaweza wakaendelea. Huko wasome akili-unde, wasome machine learning, wasome internet of things na kadhalika na kadhalika. Tujiandae na future. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, tutafanyaje katika suala hili? Kwanza, wanafunzi wa sayansi ambao wanamaliza mtihani wa form six sasa hivi, matokeo yatakapotoka huwa tuna-shortlist wale wote ambao wana-qualify kwa Samia Scholarship. Mara nyingi wanakuwa ni kuanzia mwanafunzi wa kwanza kwa performance mpaka mwanafunzi wa 640 mpaka 700. Wale tutawatangaza kama kawaida, halafu tutawaambia wanaotaka kwenda kusoma nje ya nchi first degree waombe, tutawa-shortlist. Pengine watakuwa kati ya wanafunzi 50 hadi 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, masharti yake ni kwamba hawataingia chuo kikuu mara moja. Tutawachukua tutawapeleka Nelson Mandela African Institute of Science and Technology pale Arusha ambako watafanya boot camping. Watakaa kwenye kambi pale, watafundishwa uzalendo, watafundishwa maadili, na watafundishwa digital literacy.
Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukawa na first class ya PCM lakini hujagusagusa kompyuta. Utafundishwa namna usije na cultural shock ukienda kusoma nje. Kuwaandaa wawe tayari, na baada ya takribani miezi kumi tutawapeleka kwenda kusoma kwenye vyuo tutakavyochagua kwenye masomo ya computer science in related allied science’s, lakini mostly kwa ku-aim mambo ya artificial intelligence.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kambi tunawapelekaje? Kwanza tunazo Scholarships nyingi ambazo hatuzitumii vizuri hapa Tanzania. Juzi nimetoka Saudi Arabia na Katibu Mkuu, tuna Scholarships hatuzitumii. Tutawaambia Saudi Arabia zile Scholarships, tunataka scholarship 10 hizo au 100 ziende kwa wanafunzi hawa kwa masomo tuliyochagua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna scholarships nyingine tunapata kutoka Hungary, scholarships nyingine tunapata kutoka China, tutasema hizi scholarship tunazichukua lakini tunataka wakasome masomo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumaliza zile nafasi ambazo tunazipata kama scholarships tunawatumia Watanzania diaspora na tunawanaunganisha, watuunganishe katika vyuo ambavyo wanafanya kazi ili mradi tu hatutapeleka mwanafunzi aliyemaliza form six mmoja mmoja tu. Tutahakikisha kwamba tunawapeleka kwa batch ili wasiende wakapata shida kuji-adjust; waende walau watano au kumi kwenye chuo kimoja ili washirikiane, wajenge umoja, wakakaa tu wana-adjust kwa ajili ya kusoma vile. Wanaobaki wengine watasomeshwa na pesa za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tunazungumza na wadau ili hizi bilioni tano ambazo huenda tuna-negotiates ziongezeke, wadau wengine, na niwataje kabisa, CRDB, NMB, Tanzania Commercial Bank, wamekuja wamesema wataangalia namna ya kuungana na sisi. Hii nayo ni Samia Scholarship Extended lakini ita-focus kwenye data science.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuanzia sasa hivi wanaomaliza form six na waisikie Serikali inasema wale watoto wa mkulima ambaye hakusoma International School kama wengine, kwamba sasa hawezi kuomba scholarships, tutakapomweka Nelson Mandela pale tutamsaidia na kuomba hizo scholarship, tutawa-guide ili Watanzania nao waanze kuchukua hizi scholarship ambazo zinakuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, vijana wetu hawawezi kuziomba, wanaoomba wengi ni wale waliosoma international school, watoto wa wakulima na wafugaji wataenda lini kupata hizi fursa wakati na wenyewe wana uwezo? Kwa hiyo, tunalifungua hilo suala moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda lingine niliseme haraka haraka, limezungumzwa hapa kuhusu vyuo vya elimu tiba kuwa na hospitali ya kufundishia. Naomba niseme kwamba hakuna chuo kikuu cha elimu tiba hapa Tanzania ambacho hakina hospitali ya kufundishia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ugomvi uliopo ni umiliki wa hospitali, kwamba usipomiliki pengine uratibu unaweza ukawa na shida, kwamba wewe una chuo, ni cha Serikali, humiliki hospitali ambayo una mkataba nayo halafu hospitali ikiamua kuleta wanafunzi kutoka nje, labda wametoka Sudan, ukajaza nafasi ambazo wale wanafunzi wa chuo kikuu walitakiwa wakitumie kwa ajili ya kujifunzia, inaleta utata.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa duniani, siyo vyuo vyote vya elimu-tiba vinamiliki hospitali. Kuna muundo wa hospitali na chuo kikuu kuwa chini ya entity moja na bado kuna muundo. Hata Marekani na nchi nyingine, chuo kikuu na hospitali huwa na makubaliano ya namna ya kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunaendelea na mazungumzo hasa pale Mloganzila ili kuona cha kufanya. Kwa sababu Mloganzila sasa hivi, na jana nimepata taarifa nzuri, two more centers of excellence in East Africa vimeanzishwa pale Mloganzila. Sasa na wenyewe wanauliza, hii hospitali tunaimiliki vipi? Kwa sababu hizo centers of excellence ni pamoja na tiba. Kama zinafanya utabibu, hata bajeti yao watapitisha wapi? Watapitisha Wizara ya Elimu au Wizara ya Afya? Hilo najua linafanyiwa kazi, tutajaribu kulitatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, zile tension zinazo-exist kati ya vyuo vikuu na hospitali za kufundishia tunazifanyia kazi, lakini kwa asilimia kubwa sana mambo yanaenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nimetoka kuzindua Chuo Kikuu cha KCMC. Hakimiliki Hospitali ya KCMC ingawa sasa chuo kikuu kile na hospitali ya KCMC vinamilikiwa na taasisi moja. Sasa, na sisi hospitali zetu na vyuo vyetu vinamilikiwa na Serikali moja. Kwa hiyo, naamini kama ni uratibu, tutafanya uratibu unaotakiwa, na pale ambapo tunahisi inabidi kabisa chuo kikuu kimiliki hospitali, tutazungumza, halafu tujue bajeti ya afya ile itapitia Wizara gani? Ndiyo utata mdogo ambao uliopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, napenda kuwahakikishia Watanzania wasije wakaelewa vibaya kwamba suala hilo ni umiliki, siyo matumizi, kwa sababu tayari yapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine ambalo limezungumzwa na Mheshimiwa Kanyasu na hili niliseme vizuri. Juzi hapa nimekutana na kijana anafanya kazi Guinea Conakry amesoma VETA ya Moshi ya mambo ya mining kwa sababu tu VETA ya Moshi ina industrial link na GGM. Tulifanya mapema sana na tuliandika barua Wizara ya Madini, tumemwomba Mkuu wa Mkoa na Mheshimiwa Mbunge anajua kwamba, Chuo cha VETA pale Geita kiwe ni chuo cha kufundisha masuala ya madini kwa kushirikiana na migodi iliyopo pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kuongea na wenzetu wa madini watusaidie tufanye vile. Nilishangaa na kufurahi kuona vijana wa VETA ambao wamesoma mambo ya madini pale Moshi wanafanya kazi Mauritania, nchi inayoongea Kifaransa na Kiarabu, wanafanya kazi Ghana, Guinea Conakry na Namibia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, fursa hii ya ajira ni kubwa endapo tutajenga industrial link. Kuna maelekezo mahususi tumewapatia VETA na tunawapima kwamba, lazima wa-establish industrial link, siyo tu na migodi, lakini pia na wanaoshona nguo na suti. Tumefanya nao vikao wale watengeneza furniture na shughuli nyingine zote za uzalishaji, ili ufundishaji unaofanyika kwenye VETA ulandane na mahitaji ya industry yanavyokwenda na tutawapima wenzentu wa VETA wamefikia wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine Mheshimiwa Mulugo alizungumza hapa, nilizungumze kidogo. Mheshimiwa Rais wetu wakati anazindua Sera ya Elimu na Mafunzo alilisema, PPP kwenye elimu, tunapoelekea tunahitaji kuwa na transition ya watoto wote wanaomaliza darasa la sita kwenda sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawekeza miundombinu, tunaongeza uwekezaji, sisi na TAMISEMI tunafanya kazi pamoja. Tumetengeneza booklet, tunaendelea ku-update geographical distance ya households na shule kuhakikisha kwamba, tunaweka miundombinu ya kutosha na inshallah tutapata na walimu wa kutosha kuhakikisha kwamba, kweli wanafunzi wote wanaomaliza watasonga mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, kwa maelekezo kwamba tuangalie fursa ya PPP, tunaangalia na sekta binafsi utusikie kwamba, tunaweza ikibidi tutafute namna ya kuingia makubaliano ya muda fulani ambayo wewe umejenga Sekondari hasa ya Amali, Serikali ku-guarantee ni kwa muda gani itakuwa ikileta wanafunzi na kuwalipia katika shule yako ili kuhakikisha kwamba tunachukua wanafunzi wote waendelee kusoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tukiona speed haiendi vizuri, nadhani sekta binafsi ina-role to play. Kwa hiyo, natoa wito kwa sekta binafsi ambao wameonekana kuchangamkia sana Elimu ya Amali kwamba, huenda kutakuwa na fursa na tutaanza majadiliano hivi karibuni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiwekeza vizuri kwa viwango vinavyotakiwa, na walimu wanaofaa, usipoweka fees ambazo ni exorbitant zitakazozuia watu wasiende, Serikali iangalie uwezekano kwamba, wanafunzi waliobaki, hawa tunawa-allocate katika shule inayoendeshwa na watu binafsi, ili waendelee kusoma. Kama ni mkataba wa miaka mitano au 10, hayo tutaamua pamoja na Hazina ambao wanasimamia utaratibu wa PPP, lakini tunaweza tukawahitaji sana sekta binafsi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunavuka vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu lugha ya alama, ni kweli imezungumzwa hapa vizuri, kuna Mheshimiwa Mbunge hapa alizungumza hoja yake yote ilikuwa ni kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum. Namshukuru sana, ninadhani tutamwita tukae naye, ana uelewa mpana sana. Kwenye Sera yetu ya Elimu, lugha ya alama itakuwa ni mandatory kwa watu wanaosomea ualimu kwa sababu kama unafundisha shuleni ni lazima uweze ku-communicate na wanafunzi wa aina zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba tuna Shule Maalum lakini tungependa zaidi Shule Mchanganyiko, ili hawa wasionekane kama wanatengwa na jamii, wanaenda kwenye shule zao wao wenyewe. Hilo lipo katika sera kwa sababu tulizungumza wote tukashirikiana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kidogo kabla sijatoa shukrani, mwongozo wa walimu wa kujitolea tupo tayari kuendelea kupokea maoni nimeyasikiliza, lakini mpaka sasa hivi kuna walimu 23,405 wameweza kukamilisha kupitia mwongozo huu. Mwongozo huu unamtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ashirikishwe, Kamati ya Shule ishirikishwe na taratibu zipo, lakini tunasema kila kitu kina nafasi ya kuboresha. Tutakaa na wenzetu kuona kama kuna nafasi ya kuboresha ili tupate wengi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa shukrani. Nimshukuru kwa dhati ya moyo wangu Mheshimiwa Kipanga kweli kwa kuwa mwenzangu katika uongozi wa Wizara na kuwa mwepesi sana tunapopeana majukumu. Amesababisha kazi yetu iwe rahisi sana. Mheshimiwa Kipanga nakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru sana Katibu wetu Mkuu Prof. Carolyne Nombo na Naibu wake Prof. Mushi na Dkt. Mahera, kwa kuwa ni wachapakazi wanaosababisha kazi yetu iwe nyepesi sana na kuweza kutimiza majukumu tuliyopewa na Rais wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwashukuru Wakurugenzi na watumishi wote na taasisi zote zilizopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa sababu kwa kweli wanafanya kazi round the clock. Naomba wapokee shukrani zangu za dhati hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kutoa hoja. (Makofi)