Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii mchana huu ili nami nichangie kidogo katika Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ambayo inagusa karibu kila jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchagua majembe haya mawili ambayo yanapiga kazi katika Chama hiki na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali hususan ya awamu iliyopita, Waziri aliyekuwa na dhamana katika Wizara hii alitusaidia watu wa Wilaya ya Manyoni. Tulikuwa na mgogoro wa muda mrefu sana na Wilaya ya Sikonge, Mkoani Tabora. Kwa sasa mgogoro ule umekwisha na ulitatuliwa baada ya wataalam wa ardhi kuja kufufua mipaka ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nina machache ambayo nitapenda kuyagusia. Katika Jimbo langu tuna mgogoro mdogo lakini una kero kubwa baina ya Kijiji cha Lulanga ambacho zamani kilikuwa Itagata na hifadhi yetu ya Muhesi na Rungwa Game Reserve. Najua jambo hili pengine lina-interfere Wizara hizi mbili ikiwemo Wizara ya Maliasili lakini mtu wa ardhi naomba naye alichukue hili kwa upande wake ili aone jinsi ya kusaidia wananchi hawa wa Kijiji cha Lulanga katika Jimbo la Manyoni Magharibi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba pia Waziri atuletee wataalam katika kufufua mipaka ya Vijiji vya iliyokuwa Majengo zamani na sasa Sanjaranda. Kuna mgogoro mdogo pale lakini Vijiji vya sasa ni Kihanju, Songambele na hiyo Sanjaranda ambavyo vinasuguana, kwa hiyo tunashindwa kuelewa kipi ni kipi hata tunapotaka kufanya maendeleo ikiwemo kujenga shule tunasukumana kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napenda nipongeze jitihada za Serikali kupitia Shirika hili la National Housing kwa uwekezaji wake mkubwa katika nchi hii. Japo nyumba hizi kuna changamoto zina bei kubwa, lakini ni watu ambao tunapaswa tuwasifie sasa na tuwatie moyo ili waendelee na juhudi hizi ila changamoto hizi ziangaliwe. Hapa kuna changamoto kubwa ya kodi ya VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani), kama ingeondolewa basi wananchi wetu wangeweza kumudu gharama za manunuzi lakini pia katika vifaa vya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza mji huu wa Kigamboni kuna kitu kimeanzishwa pale kinaitwa KDA ambayo haitofautiani sana na CDA ambayo iko hapa Dodoma. CDA wamepoka mamlaka ya Manispaa ya Dodoma, matokeo yake kuna migogoro mikubwa sana baina ya Halmashauri ya Manispaa na wao CDA. Kipindi cha nyuma Serikali ilikuwa imetia mkono, imetia nguvu kubwa ikawepo hadi Wizara inayoshughulikia Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu lakini leo CDA wamebaki wanajiendesha kwa makusanyo ya kodi, matokeo yake wanatoza watu wa Dodoma kodi kubwa ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hofu yangu ni kwamba inawezekana na hii KDA ikaja katika mpango ule. Kama Serikali katika ukurasa wa 47 inaonyesha barabara elekezi kilomita 71, lakini hakuna mafungu yanayoelekea pale, naamini tunapoelekea Kigamboni napo tutakuja kama CDA ilivyo sasa kwamba imeachwa pale kama mamlaka inafanya kazi za Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma. Tusije tukazua mgogoro baina ya Halmashauri ya Temeke au Halmashauri ya Wilaya mpya ya Kigamboni pamoja na hii KDA. Niombe sasa juhudi za makusudi zichukuliwe ili wahusika wajitambue na kila mmoja awe na mipaka yake mapema kuondoa hii changamoto ambazo zimejitokeza na uzoefu unatuonyesha kwa CDA ya Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vitabu hivi tulivyopewa leo katika mabegi haya nilikuwa napitiapitia nimeona shamba moja ambalo na mimi pale ni mfugaji labda, niombe ku-declare interest nafuga katika Kijiji cha Magodani katika Wilaya ya Rufiji. Mwekezaji mwenye shamba hili lililotajwa katika ukurasa huu wa 122 sehemu ya kwanza ya kitabu hiki ni mtu ambaye kwa hakika amewanyanyasa sana wananchi wa maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuliona hili na kuliweka katika kitabu hiki kwani wananchi wa Vijiji hivi vya Magodani, Kazore pamoja na Lugwadu wamefikia mahali hata kuuawa katika msitu ambao umefugwa na mwekezaji huyu lakini amekuwa anafanya patrol na bunduki na kutishia kuwapiga risasi wananchi wale. Hata wananchi waliovamia ni watu majasiri tu kuingia katika eneo lile lakini kama ingekuwa siyo juhudi kubwa za Mwenyekiti wa Kijiji kile Adam John, basi leo ungekuta maiti nyingi sana katika eneo lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ameonesha hapa katika kitabu hiki kwamba mamlaka ya utatuzi ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga. Halmashauri ile ndiyo iliyopelekea mgogoro huu kuwepo hadi leo. Kile Kijiji cha Vikindu ambacho kilitoa muhstasari ule wa heka 1,000 baadaye mwekezaji kapimiwa zaidi ekari 3,000. Kama mipaka ile itafufuliwa itaonekana ni zaidi ya ekari 3,000 lakini zimeonyeshwa pia ekari 1,700 katika nyaraka zake. Kwa hiyo, ni kwamba kuna udanganyifu mkubwa baina ya maafisa wetu hawa wa Halmashauri ambao wanashiriki katika haya mambo. Niombe sasa Mheshimiwa Waziri achukue juhudi za makusudi kusaidia wananchi hawa wa vijiji hivi ili waondokane na hii hali ya kunyanyasika na mwekezaji ambaye hana tija katika eneo lao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niipongeze Wizara kwa kujali, katika ukurasa wake wa 71 katika afua za UKIMWI wameonesha kuwajali wafanyakazi wao ambao wanafanya kazi katika Wizara hii. Mimi nikiwa mjumbe wa Kamati ile niipongeze Serikali na hasa Wizara hii, nimeona katika ukurasa wa 71 katika hotuba ya kitabu cha Mheshimiwa Waziri ameonesha Wizara yake inajali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.