Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya leo. Mwenyezi Mungu amesema katika Quran, Sura ya 41, aya ya tisa mpaka ya 11 katika juzuu ya 24 kwamba ameitandika ardhi na akaipa neema mbalimbali za ndani ya ardhi na juu ya ardhi, akaipa milima na mabonde, akaipa mito na maziwa, akaipa misitu, akaipa na viumbe hai na madini ili kwayo ituneemeshe na itufaidishe wanadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha katika ardhi hii ya Tanzania imekuwa kama ni laana sasa kwetu, badala ya heri inakuwa shari. Mwenyezi Mungu ametuambia hayo na turudi katika vitabu vyake ili tujifunze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi katika uchangiaji wake, Mwenyekiti wangu Mchakachuliwa, Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, alikariri falsafa ya Baba wa Taifa, kwamba ili tuendelee tunahitaji mambo manne; watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.
Watanzania tuna ardhi kubwa, tunamshukuru Mungu. Tupo wengi, tunakaribia milioni 50 sasa Alhamdulillah, lakini kwa nini tunagombana, tunahasimiana, tunapigana mpaka tunauwana? Ni kwa sababu ya ardhi. Ni kwa sababu ya ama ya siasa safi, uongozi bora ama yote mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali ya Chama cha Mapinduzi, kwa muda wa miaka 54, bado inawaomba tena mkae chini mtafakari, tatizo letu ni nini mpaka iwe ardhi hii haijatuletea tija? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitu ambacho kinaleta matatizo katika ardhi na kusababisha maafa makubwa ni kukosekana kwa kile kinachoitwa Integrated Land Information Management System. Pamoja na mipango mizuri iliyopangwa na Mheshimiwa Waziri na timu yake, pamoja na World Bank kutoa pesa zaidi ya Dola milioni 20 kwa ajili ya kazi hii, pesa hizi kwa zaidi ya miaka miwili zimezuiliwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, hili halijatendeka. Watanzania wanauana, wanaumizana, wanahasimiana, kwa nini? Siasa safi, au uongozi bora? Tatizo ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nikasema kwa miaka 54 hebu wenzetu kaeni chini kuwe na vision, leo kila mchangiaji anasimama anakwambia tunamshukuru Mheshimiwa Lukuvi tokea awe Waziri, amejaribu kutatua migogoro. Mheshimiwa Lukuvi ni mwanadamu, ni kiumbe. Hivi akiondoka Mheshimiwa Lukuvi, tunarudi kule kule?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kaeni chini Serikali ya CCM tuwe na vision, yeyote atakayekuja katika Wizara hizi, awe anaanza pale anakwenda mbele. Leo akiondoka Mheshimiwa Lukuvi iwe Wizara hii haipo; akiondoka Mheshimiwa Mwigulu, Wizara ya Kilimo, kwisha! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Namshukuru Mheshimiwa Profesa Muhongo. Ukienda katika ile Wizara, unajua hasa kwamba anatoka wapi anakwenda wapi, step by step. Amejipanga! Kwa hiyo, pale unajua namna gani mtu amejipanga, anatoka wapi, anakwenda wapi. Jamani ukweli lazima usemwe! Kwa hiyo, tunaomba Serikali ya CCM katika Wizara zote tujipange, tuwe na vision tujue tunakwenda wapi, siyo kusema kwamba aah, Lukuvi! Lukuvi kiumbe! Lukuvi ni binadamu huyu! Akiondoka huyu jamani, tuwe tunarudi kule? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naliomba Bunge hili, leo hii, wakati bwana mkubwa anawasilisha huyo, tujue fedha hii iliyotolewa na World Bank itatoka lini, wapewe wafanye kazi ili Watanzania wasiuwane na wasihasimiane kwa neema waliyopewa na Mwenyezi Mungu. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije la pili. Namwomba Mheshimiwa Waziri Lukuvi, pamoja na kutushawishi sana Wajumbe wa Kamati yake, pamoja na maelezo mazuri sana aliyotutolea, lakini bado tuna wasiwasi na bado mimi binafsi sijakubaliana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha miaka nane wananchi wa Kigamboni wamekuwa mayatima, wamekuwa na hofu juu ya hatima ya ardhi yao, Mji wa Kigamboni utakavyokuwa. Pamoja na kupunguza eneo likarejeshwa kwa wananchi, hilo lililobakia la hekta 6000, hadi leo Serikali hii haikupi fedha ya kwenda kufanya hizi shughuli ambazo zinatakiwa kufanywa. Hii miundombinu. Sasa kama hupewi fedha na ardhi ile tayari imezuiwa na wananchi wale wamepewa tu maelezo kwamba mwingie kwenye uwekezaji, mwingie hivi, mwingie hivi, lakini kwa muda wa miaka nane sasa hakuna fedha inayotoka, pale tunategemea nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tunasema jamani, Serikali ya CCM tunapanga; lakini tunajitekenya wenyewe, mkicheka wenyewe, kama hamjampa fedha huyo Lukuvi, atafanya nini? Kwa hiyo, kama fedha haijatengwa, wale wafanyakazi na ile Ofisi; wafanyakazi warudi Wizarani na Ofisi ifungwe, mpaka atakapopewa fedha ile itarudi ikae kwa miundombinu, ili ule Mji wa Kigamboni uje katika hilo linalotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika nyumba za gharama nafuu. Kuna wazo zuri, mipango mizuri na kwa kweli namshukuru sana. Kama analipwa hiyo shilingi milioni 40, basi ni haki yake, alipwe Mkurugenzi wa Nyumba na Makazi, kutokana na kazi anayoifanya. Kwa sababu mtu kama anafanya kazi, basi mwache apewe kwa namna anavyofanya kazi. Anafanya kazi na anastahiki. Tunaiomba Serikali waondoe suala VAT katika nyumba za gharama nafuu ili wananchi wanyonge waweze kununua hizi nyumba ziwafaidishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi jamani mtu anayelipwa mshahara wa sh. 150,000/=, ataweza kweli kununua nyumba yenye thamani ya shilingi milioni 45 kwenda juu? Kama hakuna wizi huko nyuma, ataweza? Sasa tunaiomba kodi hii VAT iondolewe katika hizi nyumba ili nyumba hizi, lile lengo lililokusudiwa la wale wanyonge kuweza kununua na kuishi katika nyumba hizi ziwafikie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Mheshimiwa Waziri, Tanzania imekua, Watanzania wanaongezeka, mahitaji ya ardhi yanaongezeka, lakini na teknolojia ya kutumia ardhi inaongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kasi ya upimaji wa ardhi ni ndogo sana. Pamoja na kuruhusu taasisi binafsi, wakawapa vibali wapime ardhi, lakini bado kasi ni ndogo sana hususan huko vijijini. Namwomba Mheshimiwa Waziri, hii kasi iongezeke ili upimaji uendelee kwa kasi na wananchi wa vijijini wamiliki ardhi ziwasaidie waweze kukopesheka kwa faida yao na kwa faida ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.