Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Joshua Samwel Nassari

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arumeru-Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ukisoma maandiko, Biblia Yeremia 33 mstari wa tatu, inasema, “niite nami nitakuitikia, nami nitakuonesha mambo makubwa na magumu usiyoyajua.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wamelia na wamemwomba Mungu, wamemwita naye amewasikia na sasa hivi yameanza kujidhihirisha, matokeo yake ndiyo haya, Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, wanakuja Bungeni kuomba sanamu ya Mashujaa iondoke iwekwe ya Diamond. Matokeo yake wengine wanaongea kwenye Bunge hili, wanasema wana uchungu sana, hawataki Bunge lionekane live, halafu siku moja baadaye anakwenda kuomba exclusive interview ya Ayo TV ili aonekane yeye kwenye TV.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile maombi haya ambayo Watanzania wameomba Mungu, yameonekana leo hii, ndiyo maana Mheshimiwa Rais anafanya vetting ya Mawaziri kwa zaidi ya mwezi mmoja, badala yake anatuletea Mawaziri walevi wanaokunywa viroba asubuhi. Hili ndilo tatizo la kukosa sukari kwenye nchi na uongozi thabiti. Ndiyo maana naona Mawaziri wanakunywa viroba. Sasa kama Mawaziri wanalewa, sijui madereva wa bodaboda kule mtaani watafanya namna gani? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nijikite kwenye uchangiaji wa leo kwenye Wizara ya Ardhi. Mwaka 1952, Mtanganyika wa kwanza aliyekwenda Umoja wa Mataifa miaka tisa kabla ya uhuru, alikuwa anaitwa Japhet Kirilo Ngura Ayo, akiwa ni mwananchi wa Meru, baada ya hapo, kilichompeleka UN Marekani 1952, New York, ilikuwa ni suala la ardhi na akianzia Meru, kwa sababu ya mgogoro uliokuwepo wa ardhi ndani ya iliyokuwa inaitwa Wilaya ya Arusha Meru miaka hiyo na Kiriro huyo akaja kuwa Mbunge wa kwanza. Wakati wa harakati za uhuru Mwalimu Nyerere amelala sana pale Meru nyumbani kwa Kiriro, alikuwa anakuja kutafuta ushauri, kwa sababu mwezake alikwishafika kabla yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka tisa kabla ya uhuru Kiriro ametumwa UN, New York, kwa fedha ambazo zilichangwa barabarani kwenye vyungu ambavyo watu wa Meru waliweka zikamsaidia kwenda yeye pamoja na Mwanasheria United Nations, 1952.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata uhuru, ameingia Nyerere, Awamu ya Kwanza, Awamu ya Pili, Awamu ya Tatu, Awamu ya Nne na Awamu ya Tano, bado ardhi ya Meru imeendelea kizungumkuti. Halafu matokeo yake, mnavyotuona sisi kule tunaamua kuchukua sheria mkononi sasa, tukija Bungeni mnaanza kutuambia Mheshimiwa Mbunge unatakiwa utulie, uwe kiongozi, uvae suti vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nivae suti? Kiriro alivaa suti mwaka 1952, mpaka leo ardhi haijarudi. Tumepata uhuru over 50 years, bado kilio ni kile kile! Matatizo ni yale yale! Ndiyo maana tunasema Serikali hii kwa kweli imechoka. You guys are sick and tired!
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niulize kwa mfano, amekuja Mheshimiwa Simbachawene Meru mwaka 2014 kama siyo 13, akiwa Naibu Waziri wa Wizara hii. Tumeongozana kwenda kwenye shamba la ACU la Valesca, Serikali ikakubali kutoa ekari 1500 kwenda kwa wananchi, leo hii ni mwaka 2016, bado zoezi halijawahi kufikia mwisho, bado ni mgogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amekuja Mheshimiwa Ole-Medeye akiwa Naibu Waziri wa Ardhi kabla yake 2012, tumekwenda kwenye shamba la Karamu, mimi na yeye mguu kwa mguu mwaka 2012. Leo ni mwaka 2016, we are crying a very same, we are singing a very same song. Kila siku hadithi ni zile zile. Tufanyeje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujaishia hapo, Tanzania Plantation; na mimeona kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri kikubwa kweli! Mheshimiwa Waziri nakushukuru leo umetupa begi kubwa, nafikiri hili begi nitapeleka nyumbani, litatusaidia kufanya kazi za nyumbani. Kwenye kitabu hiki ukurasa wako wa 39 ambao umeonesha hali ya migogoro ya ardhi kwenye nchi, umetaja hapa mashamba yaliyoko Arumeru, umeyataja mengi; Lusi, Dolly Agakhan sijui nini Tanzania Plantation na mengine na ukasema chanzo cha mgogoro ni wananchi kuingiza mifugo kwa nguvu bila idhini katika mashamba ya wakulima wakubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa mkononi ninalo Gazeti la Serikali (Government Gazette), ambalo limesainiwa na kutolewa mwezi Agosti, 1993 kabla mimi sijaanza Darasa la Kwanza, ambalo linaonesha kabisa kwamba kulikuwa na nia ya Rais ku-revoke. Baada ya hapo ikafutwa na likatwaliwa. Leo hii ni mwaka 2016 tangu mwaka 1993, leo unatuambia wananchi wanaingiza mifugo kwenye shamba la mwekezaji mkubwa, eti ndiyo maana kuna mgogoro. Hivi ni nani ambaye amevamia hapa? Ni wananchi au Mhindi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi inawekewa mfukoni Mhindi mmoja mwenye uraia wa Uingereza, anaishi Tanzania, anamiliki ardhi, ardhi imefutwa na Rais, leo anaendelea kuimiliki, amegawa, ameuza na anaendelea kuuza. Who is powerfull in this country? A business person au the Government itself? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, nina nyaraka nyingi hapa mkononi na Mheshimiwa Waziri, anajua vizuri kwa sababu kwake mimi nimekuwa ni mgeni wa kila siku. Nimemwomba pengine aje Arumeru akae hata wiki moja au mbili; kama hana sehemu ya kukaa mimi nitam-host kama ni chakula mimi nitampa. Aje kwa gharama zangu, siyo kwa gharama ya Ofisi ya Mbunge, tufanye kazi tumalize. Leo naomba nimpe tu list ya mashamba ambayo kuna nyaraka zake ziko hapa na nitaziwasilisha mezani kwa Mwenyekiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba ambayo ni kizungumkuti ni Shamba la Valesca ekari 1500, shamba la Karamu, shamba la Tanzania Plantation, shamba la Madira ambalo lilitwaliwa na wenyewe na lilipaswa kurudi kwa wananchi na nyaraka zipo hapa nitakupa badala yake tumepewa ekari 200, nyingine akapewa ekari 50 Mbunge mmoja wa Chama cha Mapinduzi alikuwa wa Vunjo anaitwa Aloyce Kimaro. Wakati huo amekwenda nje huko akadanganya anakuja kujenga hoteli, asaidie ku-host Mkutano wa Sullivan, leo ni miaka karibu 10 baada ya Mkutano wa Sullivan, hakuna hoteli wala nini, ardhi bado imehodhiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, achia mbali shamba la Madira, kuna shamba la kwa Hidaya. Mzungu mmiliki hayuko Tanzania, miaka zaidi ya nane, nimekwenda kumtatufa, hayupo. Limeachwa, limekuwa pori hapo, sijui yupo nchi gani huko, tunaangalia. Shamba la kwa Ugoro, mpaka na kesi Mahakamani wananchi walishinda, lakini halirudishwi kwa wananchi. Shamba la kwa Oscar, badala yake linakodishiwa wananchi au watu mpaka leo; nimekuja na risiti ninazo nitaziwasilisha kwako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe hii barua mojawapo hapa, imeandikwa mwaka 2001 na ikasainiwa na mtu anayeitwa T. J. Nkya, Msajili wa Hati Msaidizi, Kanda ya Kaskazini na anaonesha kabisa kwamba shamba la Arusha Ex Coffee Farm limekuwa revoked. Kwenye barua yake kwenda kwa Kamishina wa Ardhi anasema kabisa kwamba napenda kuthibitisha kwamba hati tajwa hapo juu ilitwaliwa; kwenye mabano ikaandikwa (revoked) na Mheshimiwa Rais, tangu tarehe 27 Februari, 1990, revocation kusajiliwa tarehe 3 Januari, 1991; chini ya waraka namba 6156. Mpaka leo hii tunavyozungumza lile shamba linamilikiwa na Wazungu na wameuza, wamegawa na wamepata hati, wamefanya subdivision Serikali imelala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nina nyaraka nyingine tena kwa mtu anayeitwa N. J. Masuwa, Kamishina wa Ardhi, alizungumzia suala hilo hilo na akasema kwamba utaratibu wake ulikwisha, anamwambia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru awagawie wananchi. Mpaka leo hii hakuna kitu. Matokeo yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake sasa ni kwamba wananchi wanapojaribu kuingia kwenye shamba hilo kwa nyaraka hizi, wananchi wa Kijiji cha Maksoru mwaka 2015 wakashikwa wakafunguliwa kesi, tena wakapewa kesi ya armed robbery. Mimi Mbunge ndiyo nilihangaika mpaka kesi ikabadilishwa wakatoka wako nje leo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu mwezi wa Tatu, Arumeru Magharibi kwa Mheshimiwa Gibson hapo, wananchi wengine kwenye lile lile shamba la Tanzania Plantation ambalo nimesoma taarifa yake ambayo imekuwa gazetted kwenye gazeti la Serikali hapa, wamefunguliwa kesi mwaka huu mwezi wa Tatu wakapewa armed robbery. Wengine tena upande wa huku kwangu mwaka 2015 akapewa kesi ya mauaji, kisa tu au chokochoko anadai ardhi. Nataka niulize, Serikali hii mtaweza nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nikija hapa sijawahi kuomba kwamba eti naomba kule kwangu sijui kuna shule haina choo au madawati. Kama mnashindwa kusimamia nyaraka, mtaweza kusaidia wananchi wapate madawati nyie! Mtaweza kujenga matundu ya vyoo kwenye shule? Mtaweza kununua ndege? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda na nimeshagongewa kengele ya kwanza, Mheshimiwa Waziri hizi nyaraka zote na nyingine nimeshazifikisha kwake na leo nimekuja nazo nitapeleka kwa Mwenyekiti. Wakati akihitimisha hotuba yake leo, kama asipozungumzia masuala hayo, kwa kweli naomba niweke nia kabisa kwamba nitatoa shilingi. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili na la mwisho ambalo naomba niliguse kabla ya kengele kulia, Mheshimiwa…
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Nashukuru, lakini ujumbe umefika.