Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Riziki Shahari Mngwali

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia kidogo kwenye Wizara hii. Nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba mbingu na ardhi, aliyenijaalia mimi na ninyi wote kuwa na afya njema na kuwemo humu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina machache vilevile ya kuchangia kama wenzangu wengi walivyosema, labda nami nianze nalo hilo hilo kwamba, pamoja na makandokando yake yote kaka yangu Mheshimiwa Lukuvi, lakini naona hii Wizara anaiweza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwa yale yaliyosemwa na hotuba ya Kambi ya Upinzani kwamba tunachohitaji ni system, lazima uwepo mfumo! Siyo tu kama alivyosema Mheshimiwa Yusuph kwamba Mheshimiwa Lukuvi yeye ni binadamu, lakini pia kawekwa na binadamu. Nani anajua kwamba atakaa hapo miaka yote mitano? Anaweza akahamishwa kesho kutwa. Je, akihamishwa wakati yuko katikati ya hii mikakati yake, tutafanyaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nisisitize hilo kwamba tunahitaji mfumo na huu mfumo sijui unatoka wapi! Usidhani Waziri mwenyewe anaweza akasema mfumo nimeutengeneza huu na utafuatwa na wengine wanaokuja, kwa sababu historia haituoneshi hivyo, imekuwa kila awamu ikija, inakuja na misamiati yake na taratibu zake na mambo yake na mbaya zaidi ni kama vile inafumua lote lililokuwa kabla ya hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kusema, limesemwa pia na wachangiaji wengine kadhaa kuhusu masuala ya mipango Miji. Taratibu, akili ya mwanadamu iliyo sawa huwa anarudia lile lililokaa sawa, wenye lugha yao wanasema kuna success stories. Sasa unapokuja kufanya mambo, unafuata zile success stories.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wameimba sana hapa kuhusu Kigamboni Development Agency, mpaka mwanafunzi wangu Mheshimiwa Mary Mwanjelwa akasema this is a non starter, yaani hakuna pa kuanza, hakuna pa kuelekea. Hivi tuliigiza nini tukaweka ile?
Mheshimiwa Mwenyekiti, CDA ime-fail for more than 40 years. Miaka 40 CDA haijulikani kama inatambaa au imekaa kitako au inasimama dede wanasema, lakini bado tukaanzisha mamlaka nyingine kwenye eneo dogo halafu na hotuba zote zimesema mpaka ya Kamati kwamba mmeanzisha dude halifanyi kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa hiyo hiyo ndogo iliyopo tunasema tunabana matumizi, tunapeleka kule kule; pesa inatumika hakuna productivity. Sasa sijui ndiyo siasa safi na uongozi bora! Sijui, lakini kuna kasoro kubwa katika haya. Tunahitaji kujiangalia kwa kina na tuseme hasa na tuamue tunataka nini kwenda mbele? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, toka nimeanza kuja hapa Dodoma Bungeni kila nikitoka kichwa changu huwa kinapata wasiwasi na mpaka juzi nadhani, sikumbuki nilikuwa na nani, nikamwuliza hivi hili jengo la Bunge kuwekwa hapa, nani aliamua? Hii ndiyo barabara!
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kile kikao cha kwanza nilipofika, nimekaa pale nje getini, nikaona mabasi yanapita yanafuatana. Nikasema haya mabasi yanakwenda wapi? Wakasema hii ndiyo barabara kuu, ndiyo hiyo ulipotokea Dar es Salaam, ndiyo huko inakwenda stand hapo. Naambiwa na jengo la Bunge liko hapa. Kwa nini liliwekwa eneo kama hili? Sasa nikauliza, wana mipango ya kuhamisha watu wa huku au wana mipango ya kuhamisha hili lipelekwe huko mbele ya safari? Jamani, tunafanyaje mambo kama haya? Tunapangaje? Hivi kweli wanaoitwa wapangaji, hawa watu wanaotupangia haya nao wamesoma? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna siku baba mkwe wangu aliniuliza, akaniambia wewe mama ulikwenda kusoma Marekani, umesoma umefaulu kweli au? Kwa sababu anachosema yeye kwamba, tukisharudi huku na degree za huko huko, bado tunawaita wale wataalam tuliosoma nao kule kuja kutusaidia huku. Sisi wenyewe hatuwezi. Kuna tatizo hapa, halafu watu tunakaa tu kama vile mambo yamekaa sawa. Jamani mambo haya hayajakaa sawa. Bado kunahitajika kazi ya kina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sijui, kwa sababu hatujaingia huko na wala hamtushirikishi kwenye mambo yenu, tunaona tu vision na misamiati ya hapa kazi, ya kasi zaidi, kasi mpya lakini tunabaki pale pale. Sijui tunahitaji kufanya nini, lakini ilikuwa vizuri tu mngekuwa waadilifu 2015 mngetupisha kwa sababu naamini UKAWA tulifanya performance nzuri sana na hii ingekwenda vizuri kabisa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna lingine ambalo limegusa suala mahususi kuhusu Jimbo langu la Mafia. Naishukuru Serikali na Wizara hii kwa kwenda kutusaidia angalau shamba moja kati ya mawili ambayo Wilaya ya Mafia tulikuwa na migogoro nayo. Mafia jamani ni ndogo, anapokuwepo mwekezaji sijui au mmiliki mwenyewe wa shamba pori hili la ekari karibu 4,000 na kitu kwa miaka tu linakaa hivi hivi, wananchi wanakuwa hawana mahali; sasa angalau mmetusaidia kwenda na nimeona kwenye taarifa humu kwamba shamba lile limerudishwa kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, Mheshimiwa Waziri atusaidie uhamisho huu ukamilike. Kwa sababu tunapozungumza sasa hivi, huyo mwenye nalo ameshatushtaki, kwa hiyo, tuna kesi na kwa bahati mbaya ni kesi ambayo inabidi tuje kuisemea Dar es Salaam na kwa bahati mbaya Mafia hatusafiri ila kwa ndege kwa sababu hatuna meli ya kuaminika. Ndiyo pale nikagomba sana kuhusu sh. 400,000/= mlizotupangia TAMISEMI kama usafiri, kwa sababu ile ni safari moja tu na nusu kwa sababu ndege sisi tunalipa return kwa 350,000. Sasa ni wazi kabisa hii kesi sisi itatushinda. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri achukulie hii kama special case ili jambo hili liishe haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyongeza katika hilo, liishe pia kwa kutuwekea mipaka ya vijiji vyote vitano vinavyozunguka pale, kwa sababu nimeona kwenye hotuba humu ya Mheshimiwa Waziri, amesema ni vijiji vitatu, sasa pia sivijui ni vijiji gani. Lile shamba la Tumaini linagusa Vijiji vya Jojo, Kirongwe, Baleni, Gonge na Kithinge. Sasa sijui vitatu vipi vimepimwa na viwili vipi vimebaki, lakini ingekuwa ni vizuri zaidi hili tukalikamilisha liishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna hiyo pia ndiyo itakuwa mwendo mzuri sasa wa kushughulikia masuala, tusiwe tunafanya hii nusu nusu; tunagusa, halafu tunaacha halijakamilika, tunaliachia katikati. Kwa hiyo, naomba tena kwa msisitizo kabisa, suala hili likamilike kwa haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba nizungumze kidogo kuhusu masuala ya huduma ya upimwaji ardhi. Sijui kwa nini niliposoma kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri naona hata hao wahitimu kwenye fani hii ni wachache. Najiuliza ni kwa nini? Sikuona, labda kama ipo, wahitimu wa Chuo Kikuu cha Ardhi, sikuona. Nimeona Chuo cha Morogoro na Tabora nadhani. Ni wachache mno! Hawa watu wanahitajika, tatizo ni nini? Hatuwafundishi. Vyuo hivi havina miundombinu ya kutosha kusomesha watu wengi au ni nini hasa tatizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lingine niulize, hivi Serikali inashindwaje kubeba jukumu la kutoa huduma hii? Tatizo ni nini mpaka tunaletewa sasa wapimaji binafsi ambao nao wanakuja na masharti magumu sana, wananchi wanashindwa? Utaambiwa shamba lako kama ni ekari tatu, watakwambia sijui watakutumia heka ngapi uwape na wao sehemu ama wanakutajia pesa nyingi na wananchi wanashindwa. Nilidhani hii ni huduma ya msingi kabisa Serikali ibebe na ifanye kwa taratibu kabisa. Kwani Serikali inashindwa nini kusema mwaka huu tunapima labda mikoa miwili, mwaka ujao mikoa mengine! Kwani nchi yenyewe ni kubwa ya kiasi gani Mheshimiwa Waziri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba sana suala hili la ardhi hebu lishughulikiwe kama walivyosema wengi kwamba ardhi ndiyo kila kitu. Tunahitaji ardhi tuwekeze, tunahitaji ardhi tuishi tu humo kwenye majumba yetu na mambo mengine yote yanahitaji ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba tu nami nimalizie kwa kusema tena kwamba, naunga mkono hotuba ya Kambi ya Upinzani kwa sababu imeonesha reality na tuifuate. Ahsante sana.