Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii nichangie kwenye Wizara muhimu ya ardhi. Awali ya yote, nampongeza kwa dhati Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ambaye amefanya kazi nzuri. Tunaamini kazi hii anayoifanya ni kwa manufaa ya Watanzania. Namwomba aongeze jitihada hasa aelekeze na maeneo ambayo yako pembezoni kama Mkoa wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo migogoro ya ardhi kwenye Mkoa wa Katavi. Mkoa wa Katavi ni mkoa ambao asilimia kubwa sana umemilikiwa na hifadhi za misitu na hifadhi ya Taifa ya Katavi. Karibu vijiji vingi ambavyo vimezunguka mkoa huu viko kwenye migogoro ya ardhi, lakini ni mkoa ambao una ardhi kubwa sana. Namwomba Mheshimiwa Waziri ajaribu sana kuelekeza nguvu kwenye maeneo haya ili aje aangalie migogogro ambayo ipo. Ipo kwenye vijiji kadhaa ambavyo viko kwenye Jimbo langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Kijiji cha Kabage na Kijiji cha Nkungwi. Vijiji hivi vina migogoro miwili. Moja, ni mgogoro wa mashamba kati ya wananchi waliomilikishwa ardhi kinyume na utaratibu. Wamechukua ardhi kubwa sana ambayo hawaiendelezi matokeo yake wananchi ndio wanaolima na wanabughudhiwa na wanauawa. Naomba aelekeze nguvu kwenye Kijiji cha Kabage. Yapo mauaji yamefanyika kwa matatizo ya ardhi; ayafuatilie kwa karibu ili tupate suluhisho la mgogoro huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo kwenye Kijiji cha Nkungwi. Kijiji hiki kina tatizo la mgogoro wa ardhi wa Mpairo. Mpairo ni ardhi ambayo imemilikwa na wananchi wachache. Ipo kwenye Serikali ya Kijiji na Serikali ya Wilaya ilishatoa maelekezo lakini bado mgogoro huu ni mkubwa sana. Naomba Serikali iweze kuingilia mgogoro huu ili tuweze kuwasaidia wananchi wa Kijiji cha Nkungwi. Vijiji hivi ambavyo viko kwenye Tarafa ya Mwese, vina tatizo sana la migogoro ya ardhi kati ya Serikali za Vijiji na WMA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa nia njema iliweka hifadhi kwa manufaa ya Watanzania, lakini bado Serikali hii sikivu imeweka utaratibu wa kuangalia WMA kuwashirikisha Serikali za Vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali hasa kupitia kwa Mheshimiwa Waziri, ajaribu kuja, afike Mpanda akamilishe tatizo la migogoro ya ardhi hasa inayosababishwa na WMA kuwa na kiburi bila kuwashirikisha wananchi wala kushirikisha Serikali, wanafanya wanavyotaka wao. Hili akilishughulikia atakuwa ametatua tatizo la Vijiji vya Mkabage, Mkungwi, Kasekese, Sibwesa, Kapalamsenga na Kaseganyama. Maeneo haya na mengineyo mengi kwenye Mkoa wa Katavi yana tatizo kubwa hili ambalo atakuwa amesaidia kutoa utatuzi kwenye eneo hili la migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lipo eneo la Vijiji vya Kapanga, Lugonesi na Lwega. Ni tatizo la migogoro ya ardhi ya mipaka ambayo kimsingi kama utatoa maelekezo kama Mheshimiwa Waziri, lina nafasi kubwa sana ya kuweza kutekelezwa kwa sababu ni usimamizi tu unaotakiwa ili kuweza kutoa tatizo hili kwenye vijiji hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa amefanya ziara kwenye Mkoa wa Katavi, ajitahidi sana kushirikisha Waheshimiwa Wabunge wamweleze migogoro ya ardhi ambayo ipo. Nikumbushe, wakati wa harakati za kuomba nafasi ya ridhaa ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, alikuja na Mheshimiwa Rais, yeye ni shahidi; alisimama eneo moja la Luhafu ambalo lina wakazi 25,000, mpaka sasa wananchi wanaendelea kukaa bila kuwa na amani kwa sababu Serikali imeshindwa kutoa utatuzi wa ardhi kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri ajitahidi sana kutoa maelekezo ya Serikali yatakayowapa manufaa wananchi kwenye maeneo yale ambayo yeye mwenyewe ni shahidi, alifika na alisikia kilio cha wananchi na Mheshimiwa Rais alizungumza na akatoa ridhaa kwa wananchi, akatoa matumaini makubwa sana. Naomba hilo alifuatilie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni Shirika la Nyumba. Kwanza nampongeza Mkurugenzi wa Shirika hili kwa kazi kubwa sana anayoifanya ya kizalendo. Naomba sasa Shirika libadili mwelekeo wa kuelekeza ujenzi wa nyumba kwenye maeneo ya Miji Mikuu tu. Namwomba aelekeze kwenye mji ambao unakua sasa hivi, Mji wa Katavi. Tunajua Shirika lipo linafanya kazi vizuri, lakini tunaomba kulishauri shirika hili; kwanza, lijenge nyumba ambazo zitakuwa na thamani inayofanana na watu wanaojengewa nyumba, waweze kumudu gharama za upangishaji au gharama za manunuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika limekuwa likijenga nyumba kwa gharama kubwa sana kiasi kwamba sasa wanaojengewa nyumba hizi ni baadhi ya wale wachache tu ambao wanaweza wakamudu gharama hizo. Naomba Shirika liangalie mwelekeo mpya ili liweze kujenga nyumba ambazo wananchi wataweza kumudu kukaa na wataweza kuzinunua kwa gharama ambazo zinafanana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana, kwenye eneo lingine kuna tatizo la uhaba wa wataalam wa ardhi. Kumekuwa na tatizo kubwa sana la uhaba wa wataalam. Eneo la kwetu Mkoa wa Katavi ni sehemu ambayo kuna tatizo kubwa sana la wataalam wanaohusika na suala zima la ardhi na ndiyo maana unakuta miji mingi inajengwa kwa uholela kwa sababu wataalam wanakuwa hawapo na hata kama wapo vitendea kazi vinakuwa havipo.
Naiomba Serikali ielekeze nguvu, itenge fedha za kutosha ili iweze kutoa tatizo la upimaji wa ardhi kwa manufaa ya wananchi wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie eneo la hatimiliki. Tunapotaka kuwasaidia wananchi na walio wengi wanaoishi vijijini, ni lazima Serikali ije na mkakati wa kuwezesha wananchi kumiliki ardhi ambayo itawasaidia kuweka masuala yao katika hali nzuri, hasa kwenye dhana ya kukopeshwa. Wananchi wengi wa vijijini hawakopesheki kwa sababu ardhi walizonazo hazijamilikishwa kihalali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ije na mpango wa kuweza kuwasaidia wananchi wapate hatimiliki, hata zile za kimila ziharakishwe kutengenezewa mazingira ili wananchi waweze kumiliki ardhi yao. Maeneo mengi wananchi wanalima, wanafanya shughuli zao za uvuvi lakini hawana kitu ambacho kinaweza kikawasaidia kuwezeshwa na Serikali. Naomba eneo hili lipewe kipaumbele sana kwa sababu ni eneo ambalo linaweza likawasaidia na likawainua wananchi walio wengi, wanaokaa vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa hotuba ya Waziri wa Ardhi na naunga mkono hoja.