Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima. Pili, nina kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwamba siku ya Alhamisi sawa na tarehe 19 kaka yangu Iddi Mohamed Azzan kwa hiari yake aliamua kufuta kesi ya uchaguzi ya Jimbo la Kinondoni. Namshukuru sana Mungu, namshukuru naye kaka yangu kwa ukomavu, maana sisi watu wa Pwani tunasema “mtu mzima akivuliwa nguo, basi huchutama.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu waliotangulia wametoa sifa nyingi sana kwa Mzee wangu, Mzee Lukuvi. Imenipa tabu hata mimi mchangiaji nisije nikaharibu shughuli hii nikaonekana kituko. Kabla sijafika huko, nianze na maswali mawili ambayo naomba Mheshimiwa Lukuvi wakati akifanya majumuisho ayagusie. La kwanza, ujenzi wa mji wetu mpya wa Kinondoni status yake ikoje? Wananchi wa Kigamboni wana mashaka, hawajui. Nilikuwa namwomba Mheshimiwa Waziri atuondoe shaka hii katika majumuisho atakayofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba Mheshimiwa Waziri atueleze, anaonaje; mimi nina mashaka kidogo na hasa ukizingatia sasa tunatarajia au tumeshapitisha kuwa na Manispaa au Wilaya ya Kigamboni. Sasa tutakuwa na Kigamboni Municipal Council, lakini vile vile kuna kitu kinaitwa Kigamboni Development Agency: Je, hatutakuwa na vyombo viwili vyenye mvutano ili kuhakikisha Kigamboni yetu inakuwa nzuri? Mheshimiwa Waziri naomba anisikilize vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Kinondoni, nimekumbwa na suala la bomoa bomoa. Bomoa bomoa ile imenikuta kwenye Kata yangu ya Magomeni, Mtaa wa Kwasuna, Kata yangu ya Hananasif Mtaa wa Kawawa; tena Mtaa umepewa jina la Mzee wetu, namheshimu sana; amepewa Mtaa wa Mabondeni ambapo Serikali wameona pale hawastahili kukaa watu, wakaenda kuvunja bila kujali jina lake walilompa yule mzee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi, siku mbili, tatu nimemsikia kaka yangu Mheshimiwa Waziri January Makamba alikuwa na mkutano wa hadhara kule Segerea, amesema Serikali haina mpango tena wa kuendelea na bomoa bomoa. Vile vile ikasemwa kwamba Serikali ina mpango wa kufanya mabadiliko ya sheria ya mazingira ya kupunguza mita 60 baada ya kuona kwamba utekelezaji wake umekuwa mgumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo siyo hoja yangu. Hoja yangu ya msingi; hawa wapiga kura wangu wa Jimbo la Kinondoni nyumba zao zimevunjwa na mbaya zaidi kuna wengine mpaka leo wanaishi pale kwenye vile vibanda. Mheshimiwa Waziri, kibinadamu Serikali lazima ije na suluhisho. Kwa sababu ninavyojua, jukumu la Serikali pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha watu wake wanapata mahali pazuri pa kuishi. Sasa wale watu wanaishi kwenye vijumba vibovu pale. Tumevunja nyumba zao nzuri, tumewabakishia vijumba vya mabati. Lazima Serikali itumie au itekeleze wajibu wake kuhakikisha wale watu wanapata mahali pazuri pa kuishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wale watu waliovunjiwa nyumba zao, lazima Serikali ije na mpango, tunawapeleka wapi? Hatuwezi kuwa na Serikali ambayo inapomkuta mtu ana nyumba ya vyumba vitatu na sitting room, inamvunjia halafu anabaki kwenye kibanda cha bati. Tulisema tunawavunjia nyumba zao kwa ajili ya usalama, lakini leo wanaishi katika mazingira magumu zaidi kuliko zile tulizovunja. Mheshimiwa Waziri kama atapenda, nina takwimu za watu waliopata maradhi ya shinikizo la damu kutokana tu na nyumba zao kuwekewa X na waliopoteza maisha. (MakofI)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali inatakiwa ihakikishe wananchi hao wanapata mahali pazuri pa kuishi. Nami napenda kushirikiana na Mheshimiwa Waziri katika maeneo yafuatayo:-
Moja, tuna maeneo ya squatters kwenye Kata ya Hananasif na Kata ya Tandale. Tukiamua kufanya maendeleo tukabadilisha kutoka squatters tukafanya mji wa kisasa tukajenga majumba marefu, maana yake hawa watu wote waliokaa mabondeni wanaweza kupata mahali pazuri pa kuishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nafikiri Serikali ifike mahali hasa sisi Wabunge wa Mjini ambao hatuna mashamba ya kupewa na Serikali wala sitakuja hapa nikaomba shamba Mheshimiwa Waziri, najua hana shamba la kunipa. Ninachokitaka, ni lazima Serikali tuje na mpango wa namna gani ya kubadilisha makazi yetu haya ya squatter tuwe na majumba yaliyokuwa kwenye mpango na majumba ya kwenda juu. Aliweza Mheshimiwa Mzee Karume! Mzee Karume kafanya Zanzibar, sisi tunashindwa kwa sababu gani? Kama tutashindwa kufanya Kinondoni, tunataka tukafanye wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ana Shirika lake la Nyumba. Hili Shirika limebadilishwa kabisa kutoka kutengeneza nyumba kwa ajili ya wananchi wanyonge, mpaka sasa wanatengeneza nyumba za kibiashara. Unaambiwa nyumba ya bei nafuu ni sh. 40,000,000 ya bei nafuu ni sh. 60,000,000. Kwa wananchi wetu wenyewe wana uwezo wa kujenga nyumba kwa sh. 30,000,000 ikawa bora kuliko hiyo ya sh. 40,000,000 inayojengwa na Shirika. Sasa kama Shirika hili nalo limekuwa kama la kibepari ambalo lengo lake ni kupata faida, imetokana na lengo la msingi la kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora, tena wananchi wanyonge. Kwa kweli Shirika limetoka kwenye mwelekeo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aliwahi kusema Shirika lisijenge tena nyumba za kibiashara, lakini lazima Shirika lirudi lijenge nyumba za bei nafuu kweli ambazo wananchi wa hali ya chini wanaweza kukaa. Siyo nyumba za bei nafuu za kiini macho za sh. 30,000,000 au sh. 40,000,000 ambazo wananchi hawawezi kukaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali ikiamua kutekeleza haya naogopa kusema, Mheshimiwa Lukuvi namheshimu sana mzee wangu, lakini namwomba sana, wale watu wanaoishi pale Kinondoni Mkwajuni wanaiaibisha Serikali yetu. Siyo wa kwenda kuwafukuza! Lazima sasa Serikali ionane na mwakilishi wa wananchi; tuje na mpango wa namna gani tutawaondoa pale ili nao wapate mahali pa kuishi, wasikie. Wakisikia Mheshimiwa Lukuvi ana roho nzuri, anapendwa, anapigiwa makofi na Waheshimiwa Wabunge, nao waone sababu ya Mheshimiwa Lukuvi kupigiwa makofi na Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge wa Jimbo la Kinondoni niko tayari kushirikiana na Serikali, niko tayari kushirikiana na Mheshimiwa Waziri kuhakikisha tunalitatua tatizo hili ambalo naamini linanitia aibu kama Mbunge, linamtia aibu yeye kama Waziri na linaitia aibu Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni Serikali ya wananchi, madaraka yake imepata kutoka kwa wananchi na lazima itumike kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsanteni sana na naunga mkono hoja ya Upinzani.