Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kupata nafasi ya kuweza kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Ardhi ambayo ni Wizara nyeti kwa sisi ambao bado tuko nyuma kimaendeleo na ambao tunahitaji huduma ya Wizara hii. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo anaifanya na kama walivyotangulia kusema wenzangu, ule mkoba tulioupata una elimu kubwa sana, tukiutumia ule mkoba vizuri, tukasoma, tunaweza tukapata elimu ya kutosha na ikatusaidia sisi kuweza kuwahudumia wananchi wetu vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama ambavyo nimekuwa nazungumza katika uchangiaji wangu wa awali, wilaya mpya zina changamoto kubwa sana. Wilaya ya Mkalama ambayo ni wilaya mpya hatuna Afisa Ardhi Mteule, ambalo ni jambo muhimu sana, tunamhitaji. Tunaye ambaye amehamishiwa pale lakini hajateuliwa kwa hiyo, namwomba Waziri aidha, tupate mwingine kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI au huyo aliyepo ateuliwe, atakuwa ametutendea haki na atakuwa amewatendea haki wananchi wa Mkalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, huduma za Baraza la Ardhi tunatumia kwa wenzetu wa Iramba ya Magharibi, sisi wilaya yetu ilikatwa kutokea huko, kwa hiyo, tuna shida hatuna Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi. Wananchi wangu wa Mkalama wakitaka kupata huduma hiyo inabidi wasafiri waende Kiomboi walale huko wapate hiyo huduma. Kwa hiyo, tunaomba jambo hilo lifanyiwe kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile wakati jambo hilo linafanyiwa kazi, tunaomba Mheshimiwa Waziri atoe kibali au atoe maelekezo, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi awe anakuja kufanya mashauri hayo kwenye Wilaya yetu ya Mkalama, inaweza ikatusaidia zaidi, ili kuwapunguzia wananchi gharama. Pia na haki kutendeka kwa sababu, wananchi wanaona wao wamekuwa neglected kwamba hawapati haki kikamilifu wanapokwenda kule na wala hawasikilizwi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo iko migogoro wamezungumza wenzangu hapa migogoro mingi, lakini katika mazingira ya kawaida na kama machinery za Serikali, organ za Serikali zikiwa zinafanya kazi kawaida haya mambo hayakutakiwa kufika Bungeni wala hayakutakiwa kuzungumziwa hapa, wala hayakutakiwa kufika kwa Mheshimiwa Waziri. Haya mambo tunayozungumza kama Wataalam wangekuwa wamefanya kazi yao vizuri iko migogoro ambayo ingeshamalizwa. Migogoro hii ya mipaka kati ya Wilaya na Wilaya, wakati tunasema tunataka Wilaya au Mkoa upanuke lazima iwekwe miundombinu na wataalam wapelekwe na jambo hilo walimalize na wawashirikishe wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwangu kuna migogoro mikubwa sana; kuna mgogoro kati ya Wilaya ya Mkalama na Mbulu, kuna mgogoro kati ya Mkalama na Hanang, kuna mgogoro kati ya Mkalama na Singida Vijijini. Jambo hilo limekuwa ni kero kubwa, lakini pia kwa sababu jambo hilo halijafanyiwa kazi kikamilifu unakuta Wilaya moja inakwenda kujenga shule mpakani au inakwenda kujenga kwenye Wilaya nyingine. Sasa imeleta mkanganyiko mkubwa sana tunaomba kabisa Mheshimiwa Waziri na Naibu wako tunawaamini jambo hilo lifanyiwe kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia iko migogoro ya ndani ya Wilaya nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yake, wameleta orodha ya migogoro lakini swali nililokuwa najiuliza kuna watu walipewa kazi hii ya kubainisha migogoro mbona migogoro mingine haikuingia? Tafsiri yake ni nini, inanipa picha kwamba, sasa jambo hili linatakiwa Mheshimiwa Waziri mwenyewe avae viatu aingie vitani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyokuwa tunapiga kampeni, unakumbuka mgombea Urais na Makamu wake walikwenda majimboni, mwingine kushoto mwingine kulia, wanaweza kabisa mwingine akaenda kushoto mwingine kulia na wataalam wao jambo hili katika kipindi hiki likamalizika, kwa maana ya Tanzania nzima watu wenye migogoro. Kwa sababu, mambo haya hayahitaji rocket science, ni mambo ya kiutawala, yanahitaji wafike pale penye mgogoro na wawaelimishe watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko shamba la mifugo linaitwa Makomit, linaleta mgogoro sana katika vijiji vitatu; Kuna Kijiji cha Ishenga, Kijiji cha Kinyangiri na Kijiji cha Kikhonda na nasema ni mgogoro kwa sababu Mbunge siku zote anapita barabara hiyo. Kama walivyosema Wabunge wengine waliopita hapa ni kwamba, viongozi waliokuwepo si Wakuu wa Wilaya ama Wakurugenzi, wanakuja wanafanya kazi, wanafanya mikutano ya ujirani mwema, wanahama. Wanapohama mgogoro wanauacha palepale, anapokuja mtu mpya au kiongozi mpya, mtaalam mpya anaanza jambo hilo upya, sasa jambo hilo limekuwa gumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, nafikiri wale watu hawana muscles za kutatua hii migogoro, sasa muscles hizo ziko Wizarani, Wizara tunaomba itume watu makini waimalize hii migogoro na sisi tuwe Wabunge kwa amani kwa sababu, moja ya changamoto ambayo tunapata ni jinsi tutakavyoimaliza hiyo migogoro. Tusipoimaliza inakuwa ni changamoto kubwa sana, hilo ni jambo la muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, wamezungumza wenzangu suala la sehemu zinaitwa business centres, hizi business centres zinakua kwa haraka sana, maeneo hayo yaje yapimwe, mipango miji iwekwe kwa sababu, baada ya muda nako vijijini kutakuwa na squatters kama zilivyo Dar-es-Salaam na maeneo mengine, lakini ni jambo ambalo linaweza likafanyiwa kazi mara moja na lenyewe likamalizika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza Hati za Kimila; Hati za Kimila zitolewe turasimishe hayo maeneo ili hao ndugu zetu, wananchi wetu tunaowaongoza waweze kukopesheka, lakini pia, waweze kutambuliwa na tuweze kumaliza migogoro midogo midogo ambayo inazunguka mazingira yetu. Mambo haya yanawezekana kabisa kwa makabrasha mliyotupa hapa, inaonekana Wizara ya Ardhi ina wataalam wa kutosha na tuna imani hiyo na katika Serikali hii ya Awamu ya Tano tunataka tuone hayo mabadiliko ili na sisi tuwe tunatembea vifua mbele tujue migogoro hiyo imemalizika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, “yuko mtani wangu mmoja anaitwa Mheshimiwa Waitara” anafikiri Dar-es-Salaam anakaa peke yake. Mimi nakaa Dar-es-Salaam vilevile na nakaa Kimara, eneo la Kimara lirasimishwe watu wapewe maelekezo maeneo yao yatambuliwe. Maeneo yao yakitambuliwa labda wanatakiwa kuhama waambiwe kwa sababu, huwa linakuja suala watu tunaanza kubomolewa nyumba zetu kule na mimi nina nyumba kule tunaanza kuleta mgogoro. Kwa hiyo, tunaomba jambo hili na lenyewe liweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini uko mgogoro mwingine kati ya sisi na Simiyu, ule Mto Sibiti unahama kwa hiyo, mto unapohama na mpaka unahama vilevile. Kwa hiyo, ni muhimu wananchi wetu wakaelekezwa mpaka uko wapi na pande zote mbili hizo zikashirikishwa na sisi kama Wabunge wa maeneo yote niliyoyataja hapa tuweze kushirikishwa ili tuweze kukaa kwa amani na tuweze kuwatumikia wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba na lenyewe tunalialika waje Mkalama, wilaya ile ni mpya kuna wafanyakazi wengi, zaidi ya wafanyakazi 100, hawana mahali pa kuishi. Mkija mkijenga kule na eneo tutawapatia, mtakuwa mmetusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hizi nyumba zinazojengwa zinazouzwa wanazoziita za gharama nafuu ziangaliwe, ziko nyumba zimejengwa pale Singida zimebananabanana, unajua utamaduni wa mikoani na mjini uko tofauti, designing ibadilike; halafu thamani ya milioni 40 au milioni 50 ionekane, kwamba hii ni milioni 40 na hii ni milioni 50. Bado opportunity iko kubwa wanaweza wakapanuka zaidi na Shirika letu la Nyumba likaweza kusaidia zaidi Taifa letu hili na watu wanaona kazi ambayo wanaifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, ujumbe wangu umefika, maana tunasema ni muda wa kazi tu, hatuna mambo mengi sana hapa, unafikisha hoja zako unatulia. Naunga mkono hoja, asanteni.