Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini pia, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuendelea kutoa michango yangu katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuipongeza Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na hasahasa kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Lukuvi pamoja na Mheshimiwa Mama yangu Mama Angelina. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongelea suala zima la National Housing, kama walivyochangia Wabunge wengi kuhusiana na suala la National Housing kujenga nyumba ambazo zinaonekana ni nyumba za bei nafuu kwa kinadharia tu, lakini nyumba hizi si kwa ajili ya wale wananchi wasiojiweza kwa sababu, nyumba hizi za National Housing ni nyumba ambazo ni za gharama sana. Kwa mfano, katika Hotuba yake Mheshimiwa Waziri page number 58 mpaka page number 61 ameonesha kwamba nyumba za National Housing zinajengwa ili kuweza kuwasaidia wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia hapa mfano Mkoa wa Mwanza, Wilaya ya Ilemela tunazo nyumba za National Housing ambazo zimejengwa Buswelu. Nyumba hizi zilikuwa ni nyumba nzuri, lakini sasa zinauzwa bei ya juu, zinauzwa kwa gharama ya shilingi milioni 80, sasa najiuliza je, mwananchi wa hali ya kawaida, hali ya chini, anao uwezo wa kununua nyumba ya shilingi milioni 80?
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapomwambia kwamba, aende kuchukua mkopo benki, tunafahamu wote kwamba, unapoenda kuchukua mkopo benki unaulipa kwa riba. Hivi kweli, je, tunaposema hii nyumba inauzwa milioni 80 mwananchi huyu aende kuchukua mkopo benki unakuwa umemsaidia mwananchi wa hali ya chini au unakuwa sasa umezidi kumgandamiza. Hii ni kwa sababu, anapokwenda kuchukua mkopo benki riba itakuwa ni kubwa; akikopa milioni 80 anaweza akarudisha milioni 120 kwa hesabu za harakaharaka kwa sababu, mimi pia ni mtaalam wa masuala ya benki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi naishauri Serikali iweze kusaidia shirika hili. Kwa mfano, shirika hili ukiangalia mara nyingi wanasema kwamba, nyumba hizi zinakuwa ni za gharama kwa sababu ya kupitisha miundombinu kwa sababu halmashauri zinakuwa zimewapa eneo lakini miundombinu kama vile maji, umeme, barabara, inakuwa haipo. Kwa hiyo, nashauri kwamba, basi Serikali au Wizara husika isaidie kupitisha miundombinu ya barabara, maji pamoja na umeme, ili pale shirika hili linapoanza kujenga hizo nyumba basi ziwe za bei rahisi, ili kuweza kuwakwamua wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia, niweze kuishauri Serikali kwamba, Shirika la National Housing liweze kujenga nyumba za bei nafuu kwenye makazi ya vijijini kwa sababu, vijijini ndiko sehemu ambako tuseme asilimia kubwa ya wananchi hapa nchini Tanzania wanaishi, lakini makazi yao bado ni duni sana. Kwa hiyo, naishauri Serikali kupitia Shirika lake hili la National Housing kujenga makazi ya bei nafuu huko vijijini.
Mheshimiwa Mweyekiti, lakini pia, ukiangalia sehemu nyingi za vijijini tayari kunakuwa kuna makazi yamekwishajengwa pale, kulikoni Serikali iende kujenga sehemu nyingine, naishauri Serikali kwamba, itumie lile eneo la kijiji husika kubomoa zile nyumba zilizopo kwa kuwapa elimu wananchi kwamba, ni kwa nini nyumba zinabomolewa, lakini kuweza kunyanyua majengo aidha ya magorofa au majengo ya kawaida, ili wananchi wa eneo hilo waweze kufaidika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia maeneo mengi ya watu wanaoishi vijijini ni wakulima. Kwa hiyo, watakapokuwa wamejenga nyumba zile wananchi wanaweza wakapangishwa au wakauziwa kwa bei nafuu na wakulima hawa wakaweza kulipa kidogo kidogo hatimaye kumaliza deni na nyumba kuwa za kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la squatters, squatter imekuwa ni suala ambalo ni sugu sana hapa nchini Tanzania. Naishauri Serikali kwamba, izisaidie fedha Halmashauri, ili ziweze kusaidia kurasimisha makazi na hii inaweza ikasaidia Serikali pia kupata mapato kwa sababu, katika hizi squatter hawa wananchi wanalipa tu mapato kwa Halmashauri lakini Serikali inakosa mapato kwa kupitia property tax. Kwa hiyo, nashauri Serikali iweze kuzisaidia halmashauri hususan Mkoa wa Mwanza, Wilaya ya Ilemela, watusaidie fedha kwa ajili ya kurasimisha makazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukiangalia wakazi wa Mkoa wa Mwanza wanaishi sana kwenye milima, matokeo yake tunaona disaster zinatokea, wananchi wanaangukiwa na mawe. Kwa hiyo, utaona kama maeneo yale yakiweza kupimwa na Serikali na kuweza kurasimishwa kwa wananchi kihalali, basi tutakuwa tumeondokana na hizo disaster za wananchi kuangukiwa na mawe pia hata kuondoa hili suala zima la bomoabomoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikijiuliza, kuna tatizo moja limetokea hapo Mkoani Mwanza, Wilaya ya Ilemela, kuna rada imejengwa katika Mlima wa Kiseke, rada ile imesababisha makazi 500 sasa yatakwenda kubomolewa ili kupisha rada hiyo ya Mlima huo wa Kiseke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza, hivi wakati hawa wananchi wanaanza kujenga kuanzia nyumba ya kwanza mpaka zimefika nyumba 500 na sasa zinahitajika kubomolewa, Serikali ilikuwa wapi? Haikuwaona hawa wananchi toka wanaanza kujenga nyumba moja mpaka zinafika nyumba 500? Leo hii waseme kwamba, wanataka kuzibomoa nyumba hizo, ili wananchi hawa wapishe eneo hilo la rada, kwa sababu, kwa kweli ni eneo ambalo limekuwa ni hatarishi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri sana Serikali, wananchi wanapovamia sehemu moja kwenda kujenga, basi mwananchi wa kwanza anapoanza kujenga ile nyumba moja, Serikali iweze kutoa elimu kwa wale wananchi, ili wasiendelee kuathirika pale nyumba zinapokuwa nyingi na hatimaye kubomolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri, mtakapokuja kuhitimisha hoja hii mnisaidie tu kunipa majibu kwamba, je Wananchi wale wa Kiseke wategemee nini? Je, watalipwa fidia? Kama watalipwa fidia, ni vigezo gani vitatumika kuangalia katika kulipa fidia hizo? Hilo naomba sana mnisaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kuongelea suala zima la hizi mashine ambazo zilitolewa na Shirika la National Housing, mashine za kufyatulia matofali kwa vijana wetu. Ukiangalia mashine hizi za kufyatulia matofali kwa kweli zina malengo mazuri tu; kwanza ni kupata ajira kwa vijana, lakini pili, kujenga nyumba ambazo ni za bei nafuu na pia ni imara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia vijana hawa wameshindwa kupata soko la kuuza haya matofali ambayo wamepatiwa hizo mashine na hatimaye hata kuna mikoa ambayo iliathirika na wakanyanganywa hizo mashine kwa mfano Mkoa wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini je, Serikali kwa nini inashindwa kuwasaidia hawa vijana ili wanapokuwa wanafatua yale matofali basi wapate tenda hususani kwenye halmashauri zetu, wapate tenda za kujenga. Lakini unakuta kwamba kwenye halmashauri wanatoa tenda kwa watu wengine na wanatumia matofali haya ya kufyatua ya kawaida. Hivi hawa vijana ambao mmewapa hizi mashine kwa nini Serikali isiwasaidie ili na wao waweze kujiendeleza? Pia na hizi Halmashauri nazisihi kwamba ziendelee kutoa mitaji kwa hawa vijana ambao wamegawiwa hizo mashine za kufyatua matofali ili waweze kusaidia kufyatua matofali mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo sikuwa na mengi, ni hayo tu, nashukuru sana.