Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa natoa mchango wangu nitambue mchakato unaoendelea Chasimba, wananchi wangu wameanza mchakato wa kupatiwa hati, kwa hiyo kwa hili mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, nampongeza sana Mheshimiwa Lukuvi kwa hili, kwa sababu wananchi wale takribani elfu ishirini walikuwa wanatakiwa kuondoka, lakini sasa hivi wameanza kupata matumaini na wanapatiwa hati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile natambua mradi mkubwa wa Shirika la Nyumba unaoendelea Jimbo la Kawe, eneo lililokuwa la Tanganyika Packers, baada ya mapambano ya muda mrefu, kuokoa lile eneo kutoka kwa wanyang‟anyi wanchache, tumefanikiwa limerudishwa chini ya Shirika letu la Nyumba. Vile vile wako pamoja na mwekezaji, kuna maendeleo wanafanya pale, kwa hiyo na hiyo pia natambua mradi mkubwa unaoendelea pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutamsifu sana Mheshimiwa Lukuvi hapa, lakini tusipompatia fedha ni sawa na bure, Mheshimiwa Lukuvi mwaka jana bajeti yake ya maendeleo aliyopata bilioni tatu point tano mwaka huu anaomba bilioni ishirini, kumi za nje kumi za ndani. Wakati Lukuvi anaomba hii fedha taarifa ya review ya miaka mitano ya Mpango wa Miaka Mitano inatuambia ni asilimia 10 tu ya Watanzania ama nyumba ambazo zina hati za kimila na hati za kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 10, miaka 54 baada ya uhuru, tunampa huyu jamaa bilioni 20. Inawezekana ana dhamira njema, lakini hiyo dhamira njema, haiwezi kuishia kwa kutatua migogoro, jukumu la Waziri sio kutatua migogoro, ndiyo maana tuna vyombo mpaka ngazi ya kijiji, huyu anatatua migogoro kwa sababu mfumo umefeli, anakwenda kufanya kazi ambayo kimsingi siyo yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka 54 baada ya uhuru asilimia 20 tu ya ardhi ya Tanzania, imewekewa mpango, iko planned. Hivi kweli migogoro ya ardhi itakwisha? Hivi kweli wakulima na wafugaji wataacha kuuana. Mtakumbuka miaka minne iliyopita, alipokuwa Waziri mama Tibaijuka nilileta hoja, nikasema sasa hivi tumepewa hivi vitabu, lakini nitawaambia hizi takwimu zilizokuwa humu na uhalisia uliopo kule chini, ni vitu viwili tofauti, tunafanya kuhisia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikasema kwa nia njema kusaidia nchi hii, naomba Mheshimiwa Lukuvi anisikilize na alifanyie kazi, tunahitaji kufanya land auditing, ili tujue kila kipande cha ardhi ya nchi hii kinafanya nini, nani ana nini, kiko wapi, kinafanya nini, mali ya Serikali Kuu ni ipi, mali ya vijiji ni ipi, mali ya halmashauri ni ipi. Ili tukishajua thamani ya kila kipande, tutajua na juu ya kila kipande kuna nini, kuna majengo gani, hayo majengo yanasaidia nini katika uchumi wa nchi. Kwa hiyo, tukitumia fedha nyingi, tukafanya kitu kimoja, kitu kikawa kina tija kwa Taifa; kitajibu kodi ya ardhi, kitajibu mipango ya nchi, kitajibu property tax, tutajikuta biashara ya kuzungumzia mapato haipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kikaenda kikarudi, zikapigwa danadana, miaka minne baadaye, hakuna kitu kinachoendelea. Sasa swali linakuja Mheshimiwa Lukuvi kazi yakoeitakuwa ni kutatua migogoro? Hivi nikimuuliza leo kama Waziri wa Ardhi ni vipande gani vinafaa kwa ajili ya kilimo cha kumwagilia maji atakuwa anaotea, nikimwambia nani ana nini, atakuwa anaotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nikimuuliza Mheshimiwa Mwijage hapa anazungumza eti biashara ya viwanda na yeye kwenye ukurasa wa 45, amezungumza utengaji wa maeneo ya viwanda. Tunajua, juzi kwenye hotuba yake ya viwanda na biashara, alivyobanwa kwenye maeneo ya EPZ na SEZ alikuwa anang‟atang‟ata meno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaambiwa Tanzania ya viwanda, ardhi ya EPZ ya SEZ karibu hekta 31 hakuna fidia iliyolipwa, elfu kumi ndiyo inafanyiwa tathmini, hiyo elfu kumi Serikali ilitakiwa ilipe bilioni 60, Serikali haina fedha, sasa hivi katika zile elfu kumi Serikali mnatakiwa mlipe bilioni 190, bilioni 130 zaidi. Hivi hizo kweli ni akili jamani, hapo bado zile hekta elfu ishirini na moja bado hazijafanyiwa tathmini. Halafu tunasema oooh Tanzania ya viwanda, ardhi yenyewe huna, hujalipa fidia, Sheria za nchi zinamlinda Mtanzania dhidi ya kulipwa fidia ili aweze kuondoka, tunapigana maneno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Lukuvi, tuisaidie hii nchi, tufanye land auditing, let us do that. Tulivyopendekeza aliyekuwa Waziri akaenda akakagua hayo mashamba yaliyokuwepo. Sijui mashamba 964, ekari karibu laki tisa sijui na ngapi mwenyewe anakuja kugundua yale mashamba kwamba kwa wastani wageni wanamiliki ekari, 6,300, wazalendo wanamiliki ekari 280 kwa wastani. Wageni 6,000 wazalendo 200, kwa hiyo tukiwa na hizi taarifa tutajua tunaipeleka wapi nchi, tukiwa hatuna hizi taarifa, tutabakia tu tunafikiria hapa puani, hatufikirii kizazi cha sasa, kijacho na cha kesho kutwa. Nimwombe tena tutasaidia mpango wetu wa kilimo, tutasaidia mipango yetu ya viwanda, tutasaidia mambo ya kodi, tutaweza kuisogeza nchi mbele, tutakuwa na takwimu ambazo ni tangible. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba, hili shirika tumshukuru kijana wetu ameli-transform, Waswahili wanasema mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni na Watanzania tujifunze kuwalipa watu kutokana na uwezo wao wa akili, tuache fikira za kimaskini. Nchi za wenzetu wako tayari kumlipa mtu hela nyingi kama ataweza kurudisha kitu chenye tija, sasa leo tunawalaumu Shirika la Nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitaje tu kodi wanazolipa na naomba nitaje tu, hili shirika tunaambiwa wajenge nyumba za maskini. Asilimia 10 ya mapato yao ya mwaka yanatakiwa yapelekwe Mfuko Mkuu wa Hazina, wanatakiwa walipe kodi ya makampuni asilimia 30, wanatakiwa walipe gawio milioni 300, wanatakiwa walipe riba ya mikopo wanayojengea asilimia 16 hakuna cha ruzuku ya Serikali. Wanatakiwa walipe kodi ya ardhi, kodi ya jengo, kodi ya zuio, kodi za Halmashauri Civil Service Levy, kodi ya VAT, hawa hawa wananunua ardhi kwa bei ya soko, hivi kutakuwa kuna nyumba ya bei nafuu hapo? Hakuna! Wenzetu huko mnakokwenda kutembea kila siku, haya mashirika yanawezeshwa na Serikali zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu huko mnakoenda kutembea kila siku haya mashirika yanawezeshwa na Serikali zao kama kweli hizi lugha mnazosema, tunataka ooh, tusaidie maskini, Waziri atujibu hapa, ana mpango gani wa kupunguza huu mzigo kwa shirika, ili hao maskini wasaidiwe tunaojifanya tunaimba kwa maneno wakati kwa vitendo hatulisaidii Shirika letu. (Makofi)
Mheshimimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, tuwape moyo lakini tuwasaidie huu mzigo wote wa haya makodi kumi niliyoyataja hapa, yote yanabebwa na mlaji. Mwaka 2014 hawa mapato yao ya mwaka yaliyokuwa bilioni 176 ukitoa tu asilimia 10 ya withholding wanatakiwa wapeleke Serikalini bilioni 17, wanasema ile pesa walioipeleka Serikalini walikuwa na uwezo wa kupata mkopo wa bilioni 101 ya kujenga nyumba nyingine. Yaani badala mfikirie vyanzo vipya vya kodi mkiona tu amekuwa creative pesa zinaingia mnataka mvune, hebu jiongezeni basi. Nimewaambia fanyeni land auditing, msifikirie uchaguzi, yaani shida yetu sisi Watanzania huwa tunawaza uchaguzi na tukiwa tunafanya mambo kwa kuwaza uchaguzi tutakuwa tunawaza puani, hatuwazi mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri asijali hata kama itam-cost ten million kufanya auditing nchi nzima, anaweza akaziagiza hata halmashauri kwa sababu ndiyo maana tunakuwa tuna mfumo wa utawala, aagize halmashauri tunataka mtupe taarifa kwenye halmashauri zenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba nawakilisha.