Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nishukuru kwa kupata nafasi hii. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Ardhi pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya katika Wizara hii. Vilevile tuwashukuru sana kwa sababu wameweza kutupatia taarifa zote ambazo zinahusu Wizara hii ya Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua Mkoa wetu wa Songwe ni mpya na changamoto kubwa ni kwamba maeneo mengi hayajapimwa na wananchi wake wanamiliki ardhi kwa hati za kienyeji. Suala hili kwa Mkoa wa Songwe imekuwa ni changamoto kubwa sana. Kama tunavyojua sasa hivi Wilaya yetu ya Mbozi imeweza kuwa Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe ambapo wananchi wengi wanamiminika kwenda mahali pale kwa ajili ya kupata ardhi. Hata hivyo, ardhi wanauziana kienyejienyeji kwa sababu hakuna mpango wowote wa kuweza kurasmisha ardhi ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi kuomba Wizara ya Ardhi kwa kutambua kwamba Mkoa wa Songwe ni mpya wahakikishe kwanza wanakomboa ile ardhi ambayo inamilikiwa na wananchi lakini ukienda kuangalia katika mpango wa Mkoa unakuta sehemu zingine zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya Serikali. Kwa hiyo, naomba Wizara hii iweze kuliangalia hili suala ili waweze kukomboa yale maeneo ambayo yanamilikiwa na wananchi lakini kiuhalisia yametengwa kwa ajili ya matumizi ya Serikali. Wananchi wale wa Wilaya ya Mbozi walipwe fidia waweze kuyaachia maeneo yale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine, kama tunavyojua katika Wilaya yetu ya Momba, katika Mji wa Tunduma, mji ule unakua kwa kasi kubwa sana lakini mpaka sasa hivi mipango miji ya Mji wa Tunduma kwa kweli haieleweki. Mji ule ni mji wa wafanyabiashara, population iliyopo pale ni kubwa sana na nyumba zimejengwa kiholela holela na pale ndiyo taswira ya Tanzania kwa nchi hizi za Kusini. Mtu anapokuwa anatoka Zambia akifika pale, ile ndiyo picha halisi ya Tanzania, mtu anapotoka South Africa akifika pale ile ndiyo picha halisi ya Tanzania lakini mazingira ya pale Tunduma kwa kweli hayaridhishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuomba Wizara ya Ardhi, nimuombe sana Mheshimiwa Lukuvi aweze kuangalia eneo lile la Tunduma. Tumeshuhudia katika nchi zingine kwa mfano China, wenzetu waliweza kubadilisha miji yao wakajenga maghorofa, wananchi wakapata nyumba ambazo ni makazi mazuri. Kwa hiyo, naiomba Wizara hii iweze kutupia jicho katika Mji ule wa Tunduma ili basi yale maeneo yote ambayo ni squatter yaweze kuondolewa. Yakishaondolewa waje na mpango wa kutujengea majengo ya ghorofa ili basi wananchi wa pale waweze kuishi katika makazi salama. Naamini hili kwako Mheshimiwa Lukuvi linawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo tukijenga majengo ya ghorofa katika eneo lile, moja kwa moja Serikali itakuwa imepata ardhi ya wazi ambayo najua kabisa itatumika kwa ajili ya matumizi mengine ya Serikali. Kwa mfano, katika mji ule suala la miundombinu ya barabara haieleweki, barabara kuu ni moja tu kwa sababu nyumba zimejengwa kiholela. Kwa hiyo, naomba Wizara hii iweze kutupia jicho pale Tunduma, wahakikishe eneo lile linapimwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.