Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kuandaa hotuba na kuileta hapa Bungeni. Kwa dhati nampongeza Waziri kwa mipango mizuri, utendaji mzuri na mikakati mizuri ya kuhakikisha ardhi ya nchi hii inatumika vizuri na kuwepo kwa mpango miji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo tabia ya wananchi kuanzisha miji midogo midogo kiholela pembezoni mwa barabara kuu kila kona. Ukipita barabara kuu kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma kuna miji midogo mingi isiyokuwa na ramani yoyote. Naomba Waziri aeleze Bunge hili ni mikakati gani inapangwa kudhibiti uanzishaji miji kiholela halafu wanadai huduma za jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Kaliua, Kata ya Ushokola wananchi walichukuliwa mashamba yao ya asili kwa lengo la kupimwa viwanja kwa ajili ya makazi na huduma nyingine tangu mwaka 2000 mpaka leo hawajalipwa haki zao. Mashamba hayo yamepimwa viwanja na watu wanauziwa lakini wamiliki hawaambiwi hatma ya haki zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 watendaji wa TANROARDS waliweka mawe ya alama za barabara kwenye viwanja na miji ya watu. Mpaka leo hakuna lolote linaloendelea wala hawaambiwi lolote kuhusiana na mawe hayo yaliyowekwa. Maeneo yaliyowekwa mawe ni Kata ya Ushokola na Zugimlole.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro mingi ya ardhi inasababishwa na watendaji wabovu, wala rushwa katika ngazi ya Halmashauri za Wilaya na Manispaa. Maafisa Ardhi ndiyo chanzo cha matatizo kwani ndiyo wanauza viwanja mara mbili mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Morogoro unaongoza kwa migogoro ya ardhi. Afisa Ardhi Mteule pale Manispaa ya Morogoro ni chanzo cha matatizo kwa muda mrefu yupo pale na hachukuliwi hatua yoyote. Kwa nini Serikali inashindwa kuchukua hatua za nidhamu kwa watu kama hawa na kuwaacha kuendelea kuwatesa wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Ardhi kwa ngazi ya Kata na Wilaya ni muhimu sana kusaidia kutatua migogoro ya ardhi kwa gazi za Wilaya. Serikali ihakikishe Mabaraza ya Ardhi yanaundwa katika wilaya zote hapa nchini. Aidha, Wajumbe wa Mabaraza haya wapewe posho yenye tija ili wafanye kazi zao kwa ufanisi na waache utaratibu wa sasa wa kudai fedha kwa wale wenye matatizo ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya migogoro ya wafugaji na wakulima itakwisha kwa Serikali kuhakikisha kwamba makundi haya yanatengewa maeneo ya mifugo na maeneo ya kilimo. Maeneo hayo yakishatengwa yaheshimiwe na kulindwa kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Uwekezaji inaeleza wazi kuwa wawekezaji wote wanaofika nchini na kuhitaji ardhi kwa lengo la kuwekeza watapata ardhi kwa kufika Kituo cha Uwekezaji (TIC) lakini wapo wanaokwenda moja kwa moja vijijini wanawapa viongozi wa vijiji fedha, wanawapa ardhi ya wananchi tena bila kutumia mkutano na wananchi. Serikali itoe mwongozo wa maandishi kwa ngazi za vijiji, kata na wilaya kuhakikisha sheria zinafuatwa ili kuondoa migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni wajibu wa Serikali kuhakikisha wananchi wake wanapata makazi na nyumba bora ni vyema sasa Serikalii ikaondoa VAT kwenye vifaa vya ujenzi kwa Shirika la NHC. Pia Serikali ipeleke miundombinu ili kupunguza gharama za nyumba ili wanyonge au wananchi wa kawaida waweze kuzimudu/kuzinunua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Serikali inapoona wananchi/mwananchi anajenga nyumba eneo ambalo siyo sahihi mara moja asimamishwe na sio kusubiri akamilishe ndiyo abomolewe. Suala la kubomoa linaathiri sana familia, watoto na kusababisha mzigo mkubwa wa mawazo na watu kupoteza maisha.