Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilindi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watumishi wote wa Wizara hii kwa jitihada kubwa wanazochukua katika kusimamia ardhi ya nchi hii pamoja na dhamira ya dhati katika kutatua migogoro mbalimbali ya ardhi nchini kwetu. Nimepitia hotuba hii na kuona dhamira ya Wizara hii na ilivyojipanga kuona namna gani ambavyo Serikali yetu inasimamia ardhi yetu kwa kuithaminisha kwa taratibu na sheria zilizopo, hili ni jambo jema sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia juu ya migogoro ya ardhi. Suala hili limekuwa likichukua muda mwingi wa wananchi wa kufanya shughuli za kiuchumi badala yake wanakuwa wakitumia kutatua migogoro ya ardhi. Mfano mzuri ni mgororo wa ardhi wa mpaka baina ya Wilaya ya Kilindi na Kiteto, mgogoro huu umechukua muda mrefu sana. Naomba kauli ya Mheshimiwa Waziri hivi ni lini mgogoro huu utakwisha. Naamini mgogoro huu umeasisiwa na watumishi wa Halmashauri wasio waaminifu walioshirikiana na baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Kiteto. Ili wananchi waone Serikali yao inawajali muda umefika sasa kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro huu. Nashauri Serikali iwachukulie hatua watumishi wote waliobadili ramani ya mipaka ya Wilaya hizi mbili kwani awali mgogoro huu haukuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha kuna migogoro ya wafugaji na wakulima, hii pia imekuwa ni migogoro ya muda mrefu. Wafugaji wamekuwa wakigombana na wakulima mara kwa mara kwa wafugaji kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima na wakulima kulima maeneo ya wafugaji. Nashauri maeneo haya yapimwe na wafugaji wawe na maeneo yao na wakulima wawe na maeneo yao ili kupunguza migogoro hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, uwepo utaratibu wa kuwa na maeneo ya kufuga na kunyweshea ili wafugaji wapate malisho ya uhakika kwani imeonekana hili ndilo tatizo kubwa kwa sababu wafugaji wamekuwa wakihamahama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kutafuta malisho ya mifugo yao. Vilevile wafugaji wasihame na mifugo yao kutoka Wilaya moja kwenda nyingine bila kuwa na kibali maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la watumishi hasa wale wanaopima maeneo ya ardhi. Nashauri watumishi hawa wasikae kwenye vituo vyao vya kazi kwa muda mrefu. Mfano katika Kata ya Newiro watumishi wa Halmashauri wameuza kwa wafanyabiashara maeneo mengi ya kata hii, leo hii hakuna hata eneo la wazi, maeneo yote yameuzwa. Wasiwasi wangu vizazi vijavyo vitakosa mashamba ya kulima. Mashamba haya yamepimwa na Wizara kutoa hati. Nitaleta hati hizo zenye maeneo makubwa ambayo hayakufuata utaratibu unaotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, naomba Wizara hii ifute hati ya shamba la Tanzania Leaf Tobacco Company Ltd., lenye ukubwa wa hekari 2,133 lililopo Kata ya Kwadibona. Shamba hili limetelekezwa kwa muda mrefu sana, takribani miaka 20 bila kuendelezwa. Nashauri hati hii ifutwe ili eneo hili litengwe kwa ajili ya wawekezaji. Barua ya kufuta hati hii imekwishafika Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kujibu kilio cha muda mrefu sana cha Baraza la Ardhi. Kwa niaba ya wananchi wa Kilindi tunashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.