Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuweza kushiriki Bunge hili kwa mara ya kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda siyo rafiki sana, dakika kumi naziona chache, napenda kuanza kuzungumzia suala la utawala bora. Tunapozungumzia utawala bora tunamaanisha, usiwe utawala bora wa maandishi uwe wa vitendo. Tunapozungumzia vitendo, amezungumza mzungumzaji aliyepita sasa hivi, kazi yetu sisi siyo kupongeza Serikali, kazi yetu ni kuikosoa na kuisimamia Serikali. Hatuwezi kuogopa polisi pale ambapo tunaona kuzungumza ni haki yetu, hatuwezi kuogopa kupigwa pale tunapoona Serikali imekosea, tutaisimamia na tutaikosoa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia utawala bora, nianze na suala la maslahi ya walimu. Walimu wa nchi hii ni watumishi kama watumishi wengine. Kama kweli utawala ni bora, kwa nini madai yao imekuwa ni wimbo wa nchi hii? Kila Mbunge anayesimama hapa akizungumzia Jimbo lake anazungumzia masuala ya walimu. Leo ukitazama hata kwenye vyuo, kwa sasa wanachuo wakikosa haki zao muhimu, wanaposimama kudai haki yao wengi wanafukuzwa vyuoni, je, huo ni utawala bora? Tukisimama hapa tukidai haki zetu…
MWENYEKITI: Mheshimiwa tuisaidie Serikali na nchi yetu kuboresha mapendekezo ya Mpango. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniongoza kwa sababu najua ni kazi yako. Ninapozungumzia suala la utawala bora hatuzungumzi kwa sababu ya uoga na nidhamu ya uoga sisi wengine hatuna. Mnapozunguka mnatazama nchi zinazounda Umoja wa Afrika utawala bora wanafanyaje, lakini utawala bora wa Tanzania tunauzungumzia kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vipaumbele mlivyoleta kwenye Mpango, Serikali makini haiwezi kuwa na vipaumbele vingi visivyokuwa na idadi. Inaonyesha ni jinsi gani mmeandika tu lakini utekelezaji ni sifuri. Nikianza na suala la kilimo. Natokea Mkoa wa Rukwa, tunalima sana mahindi na maharage. Leo hii wakulima wa Mkoa wa Rukwa wanajiona kama wakimbizi ndani ya nchi yao. Pembejeo ni tatizo kwao lakini hata vile vichache wanavyopata kwa nguvu zao ili angalau kuzisaidia familia zao kuna ushuru usiokuwa na tija. Tunapozungumzia ushuru, huyo Mtanzania wa Rukwa ambaye ni mkulima, amekosa pembejeo, amejikongoja akalima kilimo chake tena kwa mkono lakini na kilekile kidogo Serikali inatoza ushuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini watakapoanza kuwathamini wakulima wa nchi hii hasa wa Mkoa wa Rukwa? Wamelima mahindi na mnajua walikosa soko, mmezungumzia hapa, lakini huyu mkulima wa Tanzania ili ajue kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inamthamini, inamthamini kwa lipi, kwenye pembejeo ni shida, kwenye masoko ni shida.
Naishauri Serikali, kama kweli tunaamini asilimia kubwa ya Watanzania ni wakulima, tutengeneze mazingira rafiki ya wakulima hawa. Isibaki stori za kwenye madaftari na vitabu yanabaki kwenye makabrasha, tunataka vitendo vifanyike. Kama kweli ni kazi tu mmemaanisha mfanye kazi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye suala la maji, nikiwa natazama Bunge kwa njia ya TV, Mheshimiwa Keissy imekuwa ni wimbo wake, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, iko Mkoa wa Rukwa. Watu wa Nkasi Kaskazini na wenyewe ni Watanzania kama Watanzania wengine, kwa nini kila siku iwe ni wimbo tu wa maji? Kwenye Mpango mnaoleta mtuambie ni mikakati gani mipya mliyokuja nayo ukiachana na nyimbo mnazoimba kila siku. Mikakati mipya iko wapi ambayo itatufanya sisi tuwaamini kama kweli mnakwenda kutenda? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wananchi, imefikia mahali wamechoka na nyimbo hizi sasa wanataka utendaji. Ukitazama Bunge hili Wabunge wengi wanasimama wanazungumzia suala la maji, sawa, yawezekana tunazungumza na tunaleta kwa maandishi kama hivi, ni kitu gani kinawazuia sasa mnapoandika mnashindwa kutenda? Kama kweli ni Serikali sikivu na siyo kinyume, tendeni sasa, muache kupiga story.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la miundombinu. Mkoa wa Rukwa umesahaulika kwa kila kitu. Watu wa Rukwa siyo Watanzania? Ukizungumzia Nkasi Kaskazini na Kusini barabara ni hadithi. Amezungumza hapa Mheshimiwa Mipata na anazungumza kila siku lakini sisi tunapozungumza hatuombi, tunaitaka Serikali ifanye kwa sababu ni wajibu wenu kufanya na msipofanya tunajua hamsikii na hamuelewi. Msifikiri Chama cha Mapinduzi kuendelea kuongoza ni kwamba mnapendwa sana, no, lazima mjitafakari. Pale mliposhinda kwa haki mjitafakari lakini mapito mliyoyapata katika kipindi hiki mnajua kwamba ni jinsi gani mmekosea step, lazima mjipange. Sasa kwenye Mpango mnaokuja nao tunahitaji mikakati madhubuti ambayo kweli inamaanisha kwenda kuwasaidia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la elimu. Suala la elimu haliwezi kufanikiwa kama mnakurupuka lazima mtafakari kabla ya kusema. Mnasema elimu bure, elimu bure itakujaje wakati walimu wenyewe madai yao yako palepale? Sawa wanafunzi wamefika shuleni lakini sasa hivi wanafunzi idadi yao ni kubwa kuliko walimu. Hii elimu bure inakwenda sambamba na yale mnayoyasema au mnasema tu ili kutimiza wajibu? Mimi naamini hata hili mmeibuka tu kulisema, hamjajipanga. Ni mipango gani madhubuti ambayo mmetuonyesha hapa kama kweli mmekusudia kutoa elimu bure? Mimi nawashauri msiwe mnakurupuka, mjipange kwanza. Mkiona UKAWA wamekuja nayo wanazungumza msifikiri na nyie mnaweza mkafanya.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kazi yangu kuiambia Serikali pale walipokosea lazima wajirekebishe na wasikurupuke lazima wajipange. Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekuwa na maneno mengi kuliko kutenda na Watanzania wanaona. Haya wanayoyazungumza inaonyesha ni jinsi gani kweli wamekurupuka, hawajajipanga. Vipaumbele ambavyo wanashindwa kuvitekeleza, vipaumbele vingi, hakuna Serikali inayoendeshwa kwa staili hii. Lazima uwe na vipaumbele unavyojua utatekeleza. Ni kipi ambacho mlikileta kwenye Mpango uliopita na mmetekeleza kama mlivyokuwa mmepanga, hakuna! Imekuwa ni maneno ya kila siku ya kuandikwa yanashindwa kutekelezeka. Tunaitaka Serikali ya Chama cha Mapinduzi iachane na porojo, ifanye kazi. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.