Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja lakini naishauri Serikali bajeti inayotengwa itolewe yote na kwa wakati hasa ikizingatiwa Wizara hii inakabiliana na changamoto nyingi zinazohusiana na migogoro ya ardhi na maendeleo yanayohusiana na upimaji na uboreshaji wa mipango Miji na Majiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu ikamilishe haraka mchakato wa ununuzi wa vifaa vitakavyotumika kwenye mfumo wa utunzaji wa kumbukumbu za ardhi yaani Intergrated Land Information Management System, kutofanya haraka kunazorotesha ufanisi katika utawala wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya kuna mlundikano wa kesi nyingi kutokana na kushindwa kuhimili, kushughulikia zaidi ya Wilaya nne. Kwa mfano, Baraza la Ardhi la Korogwe linashughulikia Wilaya za Kilindi, Handeni, Lushoto, Korogwe Vijijini na Korogwe Mjini. Kwa kushika zaidi ya Majimbo na Wilaya tano kunasababisha uwepo wa rushwa jambo ambalo linazuia haki za wananchi.
Naishauri Serikali kuanzisha Mabaraza mengine kwa Wilaya ya Kilindi, Handeni, Korogwe Vijijini iwe na Korogwe Mjini na Lushoto iwe peke yake kulingana na ukubwa wa Wilaya hiyo yenye Majimbo makubwa matatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa uendelezaji Mji wa Kigamboni haujatekelezwa muda mrefu na hata haina bajeti ya maendeleo zaidi ya kuwa na bajeti ya mishahara na ulipaji wa pango la ofisi bila ya uwepo wa majukumu ya kufanya. Naishauri Serikali kuifunga ofisi hiyo na watumishi wapelekwe maeneo mengine yenye upungufu wa watumishi wa ardhi kwenye Miji na Majiji hadi Kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuanza kuona umuhimu wa kutoa maeneo ya wawekezaji nje ya maeneo ya mashamba ya wananchi au makazi ya wananchi ili kuepuka ulipaji wa fidia. Wawekezaji wanaofaidika kupata maeneo kwenye Vijiji au Halmashauri wawe na mahusiano mazuri na wananchi katika maeneo yao kwa kuvisaidia vijiji huduma za jamii kwa maendeleo ya vijiji hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa master plan za vijiji, miji na majiji ni vema elimu ikatolewa kwa wananchi kabla ya ujenzi holela ambao unapoteza maana ya miji kwa kutokuwa na miundombinu ya barabara mifereji ya maji taka, maji ya mvua mabomba ya maji, viwanja vya michezo na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze juhudi za NHC kwa kazi nzuri wanayoifanya ya ujenzi wa nyumba bora na kauli mbiu yao ya maisha ni nyumba. Naishauri Serikali shirika hili lianze kuona umuhimu wa kujenga nyumba zenye bei nafuu ili kuwawezesha hata wale wenye kipato cha chini waweze kununua nyumba hizo. Aidha, Serikali ione namna itakavyoweza kuondoa VAT kwenye vifaa vya ujenzi wa nyumba hizi za NHC kwa lengo la kuwawezesha kufanikisha ujenzi wa nyumba zenye bei nafuu.