Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Risala Said Kabongo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuchangia hoja iliyopo mezani ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi ya ujenzi wa nyumba, mfano Shirika la Nyumba (NHC) nyumba zao ni gharama kubwa sana kuanzia shilingi milioni 50 mpaka milioni 270 na kuendelea. Nyumba hizi kimsingi hazimnufaishi Mtanzania wa kawaida mwenye kipato cha chini. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inapunguza gharama hizi ambazo kimsingi zinatokana na Serikali kutokuchangia gharama za miundombinu kama barabara, maji na umeme, gharama ambazo sasa zinatolewa na NHC kupitia mikopo ya ujenzi wa nyumba hizi, hali inayosababisha gharama ya ujenzi kuwa kubwa sana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na miundombinu hii kumekuwa na suala la VAT ya asilimia 18 katika kununua nyumba hizi ambazo kimsingi VAT zimelipwa kwenye vifaa vya ujenzi. Ninaitaka Serikali itoe tamko kupitia Wizara hii ni lini itatoa VAT hizi kwa nyumba zote za Shirika la Nyumba ambalo ndilo mkombozi wa Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo mikopo ya magari, ningeshauri Serikali itoe mikopo ya nyumba za NHC kwa watumishi ili waweze kukatwa fedha kiasi. Hii itaondoa hali ngumu za wastaafu wetu ambazo wanapata baada ya kustaafu katika utumishi wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Ardhi imekuwa ikifanya kazi bila kuwa na bajeti. Tatizo la Tume hii inafanya kazi ya kuangalia eneo baada ya shughuli kubwa ya upimaji. Ningeshauri kama Tume hii itaendelea kuwepo ipewe bajeti ya kutosha na itoe ushauri kabla ya eneo kupimwa. Ninaitaka Serikali itoe majibu ya kina kuhusiana na Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, ninaitaka Serikali itoe tamko kuhusu wananchi wanaovamia vyanzo vya maji (waliopo ndani ya mita 60) ambazo wanatakiwa kuondoka. Mfano mzuri ni vyanzo vya maji vilivyopo Mkoa wa Arusha ambako kuna tatizo kubwa la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya maziko hasa ya mijini yamekuwa na changamoto kubwa sana. Ninamtaka Waziri anipe majibu kuwa Wizara yake imejipangaje kukabiliana na tatizo hili la maziko katika maeneo ya miji kama Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Kilimanjaro ambazo ardhi ni changamoto kubwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bomoa bomoa ninamtaka Waziri aniambie Serikali imejipangaje katika kulipa fidia kwa wananchi hawa ambao wanaendelea kubomolewa nyumba zao na fidia zinazotolewa haziendani na hali halisi ya gharama za ujenzi wa nyumba? Ni kwa namna gani wananchi hawa watafidiwa kulingana na hali halisi ya maisha ya leo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.