Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kuwapongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kutuletea bajeti ili tuweze kuijadili. Yapo mambo ambayo nilikuwa nataka kuishauri Serikali pia na mengine kupatiwa ufafanuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leseni ya makazi, wananchi wengi sana wanaoishi katika maeneo yasiyopimwa Serikali iliweka mpango wa kuwapatia leseni za makazi ili waweze kutumia ardhi yao kupata mikopo ya benki au taasisi mbalimbali za kifedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini muda wa miaka mitatu ni kidogo sana, ni kwa nini Serikali isiweke angalau hata miaka mitano mpaka kumi ili kusiwepo na usumbufu wa mkopaji kama anachukua mkopo wa muda mrefu? Naomba hili liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za pango la nyumba za Shirika la Nyumba. Nimpongeze Waziri mwenye dhamana. Tulishawahi kumsikia katika vyombo vya habari akizungumza kuhusu wananchi wa kipato cha chini kushindwa kumiliki nyumba za kuishi au nyumba za biashara. Kama kweli Serikali inataka na ina dhamira ya kweli ya kuwasaidia wananchi wake ingeangalia upya hizi gharama za pango la nyumba za National Housing kwa sababu wananchi wengi wana kipato cha chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hizi nyumba za gharama nafuu ziangaliwe upya, bei ni kubwa sana, watu wenye kipato cha chini si rahisi kuzinunua. Kama tatizo ni kodi ya vifaa vya ujenzi Serikali ingeondoa ili kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi nchini. Nimpongeze Waziri kwa kuanza kupita katika maeneo yenye migogoro ya ardhi, kwasababu migogoro mingi ni kati ya wakulima na wafugaji, hifadhi na wananchi na mingine ni kati ya wawekezaji na wananchi. Ni kwanini Serikali isiwe na mpango wa kutenga kabisa maeneo kabla ya kuyagawa? Ni kwa nini yasitengwe maeneo ya wakulima ili Serikali iweze kuweka mahitaji yote katika maeneo hayo ili kuondoa hii migogoro? Serikali ina wataalam wa mipango miji, ni kwa nini miji yetu haina mipango? Kumekuwa pia na migogoro hata katika miji yetu sababu wananchi hawajengi majengo kwa mpango. Ni vema Serikali kabla ya kugawa viwanja ingetengeneza mpango mji na baada ya kugawa viwanja basi wasimamie majengo yanayojengwa ili kusiwepo na migogoro ya uvamizi hata ya viwanja vya wazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Ardhi. Serikali ilijitahidi kufanya maboresho katika Mabaraza haya ya Ardhi ili mabaraza haya yaweze kutenda haki kwa wananchi. Mara nyingi kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya mabaraza kulalamikiwa kutotenda haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mabaraza haya kumekuwa na changamoto nyingi sana, ni vema Serikali ingeanza kutatua baadhi ya changamoto zinazoyakabili Mabaraza haya.