Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. William Vangimembe Lukuvi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ismani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana wewe, lakini nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja hii kuanzia Jumamosi hadi leo. Najua kungekuwa na muda kwa hoja hii kila mtu angependa kusema. Kama wengi mlivyosema mtu unaweza ukachagua ukalala barabarani, unaweza kachagua nguo, chakula lakini hakuna mbadala wa ardhi. Kwa mujibu wa Katiba yetu na maisha yetu kila mmoja anahitaji ardhi kwa matumizi yake ya kawaida. Ndiyo lengo la Wizara yangu na Serikali kuhakikisha kwamba katika mpango kazi wetu wa miaka kumi ijayo tunataka nchi hii iwe imepangwa, imepimwa na imemilikishwa. Kila mtu anayestahili kuwa na ardhi awe amemilikishwa ili ardhi yake iwe salama, hilo ndio lengo letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakushukuru sana na nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote. Nataka niwaambieni msingi wa kazi yetu sisi kama Wizara tunaanzia pale kwenye kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais. Kabla ya uchaguzi na baada ya uchaguzi alikuwa anasema na hata sasa anasisitiza kwamba kazi yetu sisi watumishi na viongozi wa Serikali ni kuwahudumia Watanzania wote bila ya ubaguzi. Hiyo ndiyo kazi yetu ya msingi na huo ndiyo msingi uliyojikita katika Wizara hii.
Kwa hiyo, mimi najua na ninyi wenzangu leo mmechangia vizuri mkijua ardhi haina ubaguzi. Ndugu zangu wapinzani mmechangia vizuri sana kuanzia Waziri Kivuli, wenzangu wa Chama Tawala wamechangia vizuri sana, kwa msingi huo kwamba tunatambua na wote tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais kwamba tunatakiwa tutekeleze majukumu yetu bila ubaguzi na sisi kama Wizara ya Ardhi ndio motto wetu. Kwa hiyo, matatizo yenu yote mliyoyasema bila kujali yanatoka upande gani, sisi kama Wizara tutayafuatilia huko huko yaliko bila kujali ni Jimbo au Wilaya ya nini ili kuyatolea ufafanuzi, kote tutafika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza zimetolewa hoja hapa kutoka kwenye Kamati yangu ya Maliasili na Utalii, Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Injinia Nditiye ameunga mkono hoja na ametoa hoja nyingi sana hapa.
Moja, imetolewa hoja juu ya mfumo mpya ambao wengi mmeuzungumzia hapa wa Integrated Land Management Information System. Ndugu zangu katika menejimenti ya ardhi kisayansi ndiyo maana tumeamua kuingia kwenye mfumo huu ili kuondoa kasoro zote ambazo tumeziona na tumekuwa nazo katika miaka yote juu ya usimamizi wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa taarifa kama ile niliyoitoa hapa kwamba mfumo huu siyo kwamba umekwama maana wengi nafikiri sikuwapa taarifa mapema kwamba hata yule mtekelezaji wa programu hii ameshapewa barua yaani ameshakuwa awarded na baada ya wiki mbili watakuja hapa Dodoma kusaini. Nimeagiza waje wasaini hapa mbele ya Mwenyekiti na Kamati yangu ili tuanze kazi ya kufunga mfumo huu ambayo itachukua si chini ya mwaka mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya kabrasha nililowapa kuna kakitabu kadogo, kameandikwa Mradi wa Kuboresha Sekta ya Ardhi. Wale waliopata nafasi bila shaka wamefunuafunua kidogo. Ukija kwenye ukurasa wa mwisho huku ndio unaonesha mfumo wenyewe utakavyokuwa. Kwa hiyo, tutaachana kabisa na mfumo tuliouzoea na makaratasi mengi na mafaili ya hovyo hovyo kwenye Wilaya, Wizarani na Mikoani, tutaingia kwenye masuala ya kisasa.
Kwa hiyo, nataka kuwahakikishia wote wengi ambao wamezungumza kuanzia Kamati yangu na hasa Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa amezungumza sana kwa sababu alikuwepo kwenye Kamati iliyopita na wale waliosema tulikwenda nao Uganda na Ethiopia ni kweli lakini sasa zamu yetu imefika kwa hiyo nataka kuwatoa wasiwasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wote wanaozungumza kwamba fedha haziko kwenye bajeti hii, someni hii, humu ndani mna dola zaidi ya milioni 25 kwenye miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmezungumza habari ya upimaji na tatizo tulilonalo la vifaa vya upimaji kwenye Halmashauri, ukisoma hapa tuna fedha nyingi, tumeshaagiza vifaa vya upimaji lakini hatutavipeleka Wilayani, tutavipeleka kwenye Kanda nane, tunataka Halmashauri zenye kazi ya kupima zikachukue pale kwenye Kanda wakapime bila malipo yoyote. Kwa hiyo, vifaa tunanunua na fedha ziko hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmezungumza habari ya master plan hasa ya Jiji la Dar es Salaam, ilikuwa mwezi uliopita ile ndege ya kupiga picha ya anga itusaidie katika kutengeneza master plan ingekuwa tayari, sasa hivi kwa sababu ya hali ya hewa wanategea tu. Hata hivyo, fedha ziko hapa kama dola milioni tatu hivi, tumeshamlipa contractor na hiyo ndege itapita angani kupiga picha za anga ambazo ndizo zitatusaidia kwa sababu hizi ndio base map za kutusaidia kutengeneza master plan, fedha ziko hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ununuzi wa vifaa hata magari yako hapa. Huo mtandao wenyewe wa ILMIS mnaousema ni dola milioni 12, hamtaziona kwenye bajeti yangu kwa sababu hizi fedha zilionekana kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa hiyo, ukiacha hizi zinazosomwa, nataka kuwaondoa wasiwasi na dola zaidi ya milioni 25, ziko kwenye mfuko mwingine na siyo za leo ni kweli ziko kwa miaka miwili iliyopita lakini zitatumika kwa mafao ya Wizara ya Ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaendesha zoezi la kukusanya maoni ya Sera ya Ardhi. Waheshimiwa Wabunge, katika kabrasha langu hilo nimewapeni bahasha fulani ina flash, ndani ya flash mle kuna barua nimeweka inayoonesha kwamba ndani ya barua ile kulikuwa na sera tatu.
Moja ya sera muhimu ambayo inazaa mikingamo yote ya haya mliyozungumza tangu asubuhi ni Sera ya Ardhi kwa sababu ndiyo imezaa Mabaraza ya Ardhi, sheria na kila kitu. Kwa hiyo, ili kuondoa mzizi wa fitina yote haya, ni muda mrefu sana kwa sababu tulianza kutengeneza sera ndiyo iliyotuelekeza kuwa na Sheria Na.4 na 5 ambayo wengine hapa wametoa mawazo kwa nini tuwe na Sheria mbili za Ardhi tuwe na sheria moja. Ndiyo iliyoanzisha hati za kimila na hati za kawaida na ndiyo iliyoanzisha Mabaraza ya Vijiji, Kata na Wilaya hayo yanayosiganasigana. Kwa sababu tunajua sasa ni muda mrefu umepita ndiyo maana tumeamua kuanzisha kazi ya kutafuta maoni ya wananchi juu ya Sera ya Adhi kuona ni namna gani leo baada ya miaka 50 hii tuweze kumiliki na kusimamia rasilimali ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndani ya bahasha ile kwenye kile wanachoita flash disk (kinyonyi), nawaombeni mnipe muda wenu kidogo Waheshimiwa Wabunge na ninyi nimewaleteeni questionnaire kubwa kidogo, dodoso kwenye kinyonyi nawaombeni sana, ninyi ni wadau muhimu sana katika marekebisho, shida zenu zote hizi zitakwisha tu kama tukishiriki kurekebisha sera halafu baadaye tupitie marekebisho ya sheria zetu. Kwa hiyo, naomba ndani ya kinyonyi nimewapa dodoso m-print ili msumbuke kidogo mtoe maoni yenu humu mkipata nafasi. Nitafurahi Bunge likiisha mwezi wa sita mwishoni kila mmoja wenu anipe maoni yake juu ya anavyofikiri turekebishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nimewapeni sera zote, ndani ya flash kuna sera tatu zote tulizonazo na tunatengeneza kwa mara ya kwanza Sera ya Nyumba. Hatukuwa nayo, tunarekebisha Sera ya Makazi na tunatengeneza na Sera ya Nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani nimewapeni na Sera ya Nyumba na Sera ya Ardhi ili mpate nafasi Waheshimiwa Wabunge, najua mna majukumu mengi, lakini mtafunuafunua kidogo ili angalau m-print mtoe maoni, maana nyie ndio wadau muhimu. Ndani ya flash humo pia nimewapeni sheria 15 ambazo ndiyo zinasimamia utawala mzima wa ardhi, naomba mzisome.
Humu ndani kuna wasomi wengi, wengine wanasheria, wengine wazoefu tu, mambo ya ardhi, vita hizi na migogoro hii imetufundisha kusoma vitu vingi. Kwa hiyo na zenyewe kama mnafikiri kuna sheria fulani fulani zinakinzana au haziendi vizuri, someni tupate msingi wa kuzibadilisha. Nawashukuruni sana Waheshimiwa Wabunge na nitawashukuru sana kama mtanisaidia kurekebisha haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua muda hautoshi lakini nije kwenye suala la ujenzi holela limezungumzwa sana. Najua Serikali peke yake zamani ndiyo ilikuwa na jukumu la upimaji na upangaji hatukupanga na kupima vya kutosha. Kwa hiyo, wananchi wametutangulia na wamejenga wanavyotaka kwa sababu hawawezi kutusubiri. Sasa tumeanzisha programu ya kupanga na kupima kwenye miji na vijiji, lakini kazi hii lazima tushirikiane kwa sababu ni kazi ya msingi ya Halmashauri zetu, ndiyo wenye ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi mmezungumza habari ya kupanga hata kwenye vimji vidogo, anayeamua mji mdogo upangwe ni ninyi Halmashuri ya Wilaya, mnaamua kwamba mji huu tunataka tuupange, mnaniletea mimi natangaza kwenye Gazeti la Serikali kwamba sasa Waziri ameridhia kaeneo fulani ka Tarime kapangwe kama mji mdogo; kama Mheshimiwa Esther anavyoomba, kwa hiyo leteni maombi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hamna uwezo wa kupanga sisi tutawasimamia na kuwasaidia watu wenye uwezo wa kupanga tunao wasomi wengi mitaani. Hivi sasa tumeanzisha kampuni 58 za wataalamu. Tuna wataalamu waliobobea kwenye masuala ya mipango miji wapo mitaani, tumeamua waanzishe kampuni za wataalamu wa kupanga na kupima tumezi-register ili ziwe mbadala ya shida ya wapangaji, wapimaji wa Halmashauri, ambao kwanza ni wachache lakini uzoefu wangu nao mara nyingi sana wapimaji wa Halmashauri hawafanyi vizuri kwa uadilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mahali popote kwenye mchoro ambao tumeupitisha sisi ambao una viwanja 1,000 ambapo Wapimaji wa Ardhi wa Halmashauri yoyote wamepima wakavikabidhi Halmashauri viwanja 1000, lazima 100 watavikata. Kuondoa shida hiyo, kwa sababu vifaa tunavyo vitakuwa kwenye Kanda, tumeamua kushirikisha makampuni binafsi yatakuja kupanga, yatapima, umilikishaji utakuwa jukumu lenu Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua muda hautoshi kueleza, lakini concept hii nitaieneza nitakapopita mikoa yote mikoa yote kuelezea juu ya migogoro na namna ya kutatua na tutapanga hizi kampuni kwa mikoa ili zisaidie katika kupanga miji midogo midogo ili nayo isianze kujitanua kama squatter hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunao mpango mwingine wapangaji hawa watakuja kuwafundisha zaidi; tumeshawafundisha, lakini Halmashauri tunataka sasa zijikite katika urasimishaji wa maeneo ambayo tayari yameshakuwa squatter. Hatuwezi kuyavunja yale watu wameshajenga. Kwa hiyo tunakuja kuwafundisha tunawaelimisha na tutatumia kampuni za watu binafsi kurasimisha makazi ili watu wanaoishi kwa makazi yanayoitwa si salama waweze kumilikishwa hati zao, miundombinu ipite wapate hati zao waweze kukopesheka. Kwa hiyo hayo ni mambo tunayokuja kuyafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utoaji wa hati. Hati za kimila zinakopesheka kwenye kitabu changu nimesema na ninawashukuru sana benki ya TIB, Exim, CRDB na NMB wanakopesha na NMB ndiyo benki iliyopo kila mahali. Niambieni kama kuna mahali wamekataa kukopeshea kwa hati ya kimila, wanakopesha. Sasa nasema ushauri wenu nitaongeza nguvu ili mabenki mengine mengi yaweze kukopesha kwa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tutaongeza kasi vilevile ya upimaji na upangaji kwa kushirikiana na Halmashauri lakini kushirikisha kampuni nyingine ambazo hazitatoza hale kubwa, kwa sababu utozaji wa makampuni hawa mengine yanayoingia mikataba kama ya Bukoba na mahali pengine wameingia mikataba hata Lindi na wapimaji binafsi matokeo yake viwanja havinunuliki. Kwa hiyo Wizara yangu vile vile itajikitakatika kutoa bei elekezi ya upangaji wa bei za viwanja ili watu wasijiuzie wanavyotaka. Leo tumesimamisha uuzaji wa viwanja vya Temeke kwa sababu tumekuwa nao, Mheshimiwa Mbunge yupo hapa; yaani mtu anapima tu ardhi gharama ni shilingi 2000 kwa upimaji wa kiwanja halafu wanauza shilingi milioni 27. Haiwezi kuwa, ardhi hii haiwezi kuwa mbadala wa shida zenu zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tutasimamia upangaji lakini tutasimamia na kuelekeza viwango vya kuuza bei vinginevyo mnalilia tu miji ipangwe nani atanunua kiwanja shilingi milioni 27. Ikiwa Wizara ya Ardhi inakopesha milioni 20 kwa mfanyakazi wa kawaida kukopa, kiwanja milioni 27 utapata wapi?
Kwa hiyo, nawaomba tusimamie. Wenzenu kule Halmashauri wana ingiza vitu ingawa hapa nimeona wengi mnasema gharama ya viwanja ni kubwa upimaji na hela zinakwenda wapi, hizi hewa zinajazwa kule. Kwa kuwa huwa hamshiriki mshiriki vizuri kuhoji gharama hasa hasa mliyoingia Halmashauri ya kupanga ni shilingi ngapi, kupima ni shilingi ngapi. Basi hata faida weka ten percent, twenty percent.
Mtu mmoja Halmashauri ya Jiji mmoja ambaye tumemfukuza, ananiambia mzee hapa bwana tumepata katika hii orodha ya viwanja hivi tumepata faida shilingi bilioni saba. Unawezaje kupata bilioni 7 kwa viwanja vya mkupuo 1500 ulivyopima kwa wakati mmoja? Lazima hizi shilingi billioni saba umewanyonya sana wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka kuwaagiza halmashauri zote msifikiri ardhi ni suala la kujitajirisha tu. Na hata sasa nimezuia, ni marufuku kwa kampuni binafsi kwenda kununua mashamba na kujipimia viwanja, marufuku, haiwezi kuwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani leo Bagamoyo unaenda unanunua shamba heka kumi, kesho umebadilisha matumizi viwanja haiwezi kuwa. Kwanza ukibadilisha shamba kwenda matumizi ya viwanja umepandisha hadhi halafu unapima viwanja. Leo kuna mtu pale wamempa hati 600 za kwake binafsi kwa jina lake kwa sababu ni shamba lake amepima ameweka majina yake. Sasa ni marufuku mtu yeyote aliyenunua shamba litabaki shamba, ukitaka viwe viwanja kabidhi Halmashauri ndio wata deal na mimi kubadilisha matumizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mtu binafsi umenunua shamba ukilenga kwamba unataka kupima viwanja imekula kwako. Kabidhi hilo shamba Halmashauri itapanga, itapima, itamilikisha yenyewe, kwa sababu nimeona sasa watu wanakuja na briefcase zao wanatajirika kwa mashamba yetu kwa kupima viwanja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nirudie kidogo aliyoyasema Mheshimiwa Naibu Waziri juu ya fidia. Jamani fidia ipo kwa mujibu wa sheria, someni sheria sitaki kufafanua zaidi na tumeshasema kwamba ukiukwaji huo basi. Kama kuna mtu anataka kuchukua ardhi hata kwa maendeleo tenga fedha kwenye bajeti. Huo ndio msimamo wa sheria ambao hauna pande mbili ni upande moja tu, iwe ni kwa maendeleo au kwa huduma. Tenga fedha kwenye bajeti, nunua hilo shamba, fanya unachokitaka, huo ndio msimamo wa sheria. Mkitaka basi njooni mbadilishe sheria hapa ili iseme kwamba ardhi ichukuliwe bure kwanza au ikopwe halafu ndipo ifanye shughuli, hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo msimamo wa sheria ni huo na wote mnaochukua hayo ni lazima mfuate sheria. Mimi najua Halmashauri nyingi zimechukua maeneo ya watu wamepima viwanja, wanauza viwanja. Lakini angalau huyo mtu uliyechukua shamba ajue atalipwa kiasi gani aishi kwa matumaini. Lakini msiwe na hofu hata hao wanaocheleweshwa kulipwa fidia inabadilika kwa mujibu wa sheria kwa sababu ukichukua eneo la mtu bila kulipa fidia kwa miezi kadhaa inatozwa interest. Kwa hiyo, wale wote ambao wanafikiri hawajalipwa fidia kwa sababu maeneo yao yamechukuliwa na taasisi fulani fulani wajue wameweka fedha benki watalipwa na interest. Kwa hiyo, wasikate tamaa siku ambapo watalipwa, watalipwa pamoja interest kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Ndugu zangu mmezunguza sana habari ya migogoro ya ardhi. Kwa ufupi sana nataka niseme wale ambao wameniandikia nawashukuru na wengine wameboresha, tutajipanga. Wizara yangu peke yake haiwezi tutajipanga ndani ya Serikali Wizara zote zinazohusika na Maliasili, maana mimi sisababishi migogoro wanaosababisha ni watumiaji wa ardhi yangu. Kwa hiyo, tutajipanga na wenzangu TAMISEMI, Maliasili, Kilimo ili angalau tushirikiane tujipange tuifikie mpaka migogoro ya mipaka ya kijiji na kijiji. Tutajipanga na tutakuja kwenu, nataka kuwahakikishieni tutafika kote tutajipanga na wataalamu wetu ili tufike tuisome. Kama ni marekebisho ya mipaka tutafanya, kama ni ramani tutasoma, kama ni marekebisho ya jambo lolote tutafanya, kwa sababu Serikali ni moja na Mheshimiwa Rais ameagiza katika miaka mitano hii lazima tuwaondolee machungu wananchi, tuondoe migogoro ya ardhi. Kwa hiyo, kwa motto huo tutafika huko kote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lwakatare amezungumza mengi sana lakini asishike shilingi yangu. Najua matatizo yake ya Bukoba ni makubwa, lakini kama tulivyoongea Chief Valuer wa Wizara yangu Evelyine baada ya Bunge hili pamoja na Kamishna wa Ardhi wa Kanda wanakuja Bukoba. Kuna mgogoro wa viwanja 5,000, sasa wanakuja kwa sababu tulishaelekezwa na Waziri Mkuu, wewe umeandika lakini sisi tulishaelekezwa na Waziri Mkuu kwamba lazima TAMISEMI na mimi nipeleke. Kwa hiyo, mimi napeleka watu wawili, lakini atakwenda na mtu wa TAMISEMI kuhakikisha kwamba mgogoro wa Bukoba sasa tunautafutia dawa once and for all, kwa hiyo, tunakuja huko. (Makofi)
Mheshimiwa Nassari kwanza yale uliyoyasema naomba radhi sana, yale yalioandikwa kwenye kitabu wamekosea, yale mashamba yote yalishafutwa.
Sasa wewe na mimi tunajua, nimehangaika sana ili mradi sasa unataka nije nikae nyumbani kwako wiki mbili nitakuja. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tulishahangaika sana nimetumia fedha zangu mpaka nimetoa shilingi milioni 271 za kuja kupanga vipande vidogo vidogo kwa kumilikisha wananchi wako wenye shida kutoka kwenye mashamba hayo. Lakini watendaji wangu wa upande ule wameniangusha, hawajafanya. Nimefanya sana na Arusha DC anajua nimempa watu wake 4,000 nimewapa vipande kwenye mashamba ambayo tumefuta, lakini hawajapanga kwa sababu sielewi wamenipa taarifa na fedha zangu za kupanga walikuwa hawana Halmashauri ya Arumeru na DC nimewapa 271 ya kufanya kazi hiyo. (Makofi)
Ndugu zangu, Chuachua wa Masasi kwanza ngoja nijipongeze mwenyewe pale unaposema tumejenga nyumba za National Housing nilikupa na bonus ya zahanati ila haukusema.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Eee! Chuachua pale, nilikupa bonus ya zahanati lakini hukuisema, wewe umezungumzia fidia tu. Lakini nataka kuwahakikishia watu wote, wa Dar es Salaam mmezungumza kwa uchungu sana juu ya migogoro yenu yote, Kazimzumbwi tunaenda kuimaliza Alhamisi, tumeshaelekezwa na Waziri Mkuu mimi na Mheshimiwa Maghembe tunakwenda Dar es Salaam tunaenda kumaliza shughuli ya Kazimzumbwi haitakuwepo tena, tunamaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamezungumza, rafiki yangu wa Siha naye amezungumza sana, lakini wewe mambo yako lazima tufike kule tumalize. Mzee wa Karagwe nakumbuka umezungumza sana, Mzee wa Efatha kule Malocha, wazee wa Sumbawanga kule wamezunguza sana habari ya Efatha. Efatha jamani sio jina la mtu maana mnazunguza hapa ni taasisi ya dini naona mmezungumza Efatha sana. Lakini nataka kuwahakikishia ndugu zangu wa Mkoa wa Rukwa, issue ile ya Efatha ipo mahakamani, siwezi kuizungumza sana, mimi nitakacho kifanya nitaimarisha nguvu ya mwanasheria wenu wa Sumbawanga ili kumsaidia ili kuharakisha ile kesi iishe haraka. Lakini dhamira ya Serikali ya kutwaa lile shamba iko pale pale, na madhumuni yake ni yale yale. Kwa hiyo, Mzee Malocha nafikiri umenisikia hapo. (Makofi)
Ndugu zangu mmechangia watu wengi waliochangia kwa maandishi mpo 57 naomba sana niwashukuru katika hoja hizi mbalimbali nilizozungumza hizi za mwanzo, Waheshimiwa waliochangia hasa hasa kwa kusema ni wengi lakini namkumbuka zaidi ndugu yangu Julius Laizer ambaye alifoka sana.
Nataka kukuhakikishia kwamba yale uliyoyasema nakubali kwamba lile shamba la Makuyuni lazima lirudi kwa wananchi. Lile shamba lilipangwa liende kwa wananchi na litarudi kwa wananchi. Ila ujue inakula kwako kwa sababu aliyejimilikisha hili shamba ni Edward Lowassa, nilitaka kukupa hiyo taarifa tu hapo umeingia pagumu kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba hili lilidhamiriwa na Rais Mkapa wapewe wananchi, lilikuwa shamba la Stein Seed Vallay wanaokumbuka historia ile aliyefukuzwa na ndege na kila kitu..
Naam, Mheshimiwa Waziri wakati ule akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu alisisitiza kwa Mheshimiwa Mkapa kwamba shamba hili naomba sana wapewe wananchi na vijiji vile wameshaniandikia mimi. Lakini bahati mbaya sana hati niliyonayo hapa imesainiwa na Mheshimiwa Lowassa. Kwa hiyo, mimi nakusaidia wewe kwamba hati hii tutairekebisha yeyeto aliyesaini hapa tutarekebisha na ardhi hii itarudi kwa wananchi. Nakushukuru sana tumeshirikiana kwa mengi na hili tutalimaliza na lazima tushirikiane mimi na Halmashauri ya Monduli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mary Mwanjelwa amezungumza kwa uchungu sana, Mheshimiwa Augustino Masele huyu leo amefunga bao la pili maana hata Jumamosi alichangia. Mheshimiwa Chatanda nasema hawa wote ambao wamezungumza hoja zinazofanana Mheshimiwa Abdallah Mtolea, Mheshimiwa Shangazi, Mheshimiwa Salma Mohamed Mwassa, Mheshimiwa Anatropia Theonest, Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mheshimiwa Rashidi Mohamed Chuachua, Mheshimiwa Joram Hongoli na Mheshimiwa Zuberi Kuchauka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine ni Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed, Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mheshimiwa Amina Saleh Mollel, Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mheshimiwa Omary Tebweta Mgumba, Mheshimiwa Sixtus Mapunda, Mheshimiwa Maria Ndila Kangoye, Mheshimiwa Riziki Mngwali, Mheshimiwa Joseph Roman Selasini, Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang‟ata, Mheshimiwa Joshua Samwel Nassari, Mheshimiwa Maulidi Mtulia, Mheshimiwa Stephen Ngonyani, Mheshimiwa Massay, Mheshimiwa Moshi Kakoso, Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mheshimiwa Kiteto Koshuma, Mheshimiwa Kunti, Mheshimiwa Halima Mdee, Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza, Mheshimiwa Dkt. Godwini Mollel, Mheshimwia Zainab Katimba, Mheshimiwa Felister Bura, Mheshimiwa Emmanuel Papian, Mheshimiwa Agustino Masele again, Mheshimwia Rose Tweve na Mheshimiwa Juliana Shoza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia waliochangia hoja hizi, Mheshimiwa Edward Mwalongo, Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu, Mheshimiwa Sixtus Mapunda, Mheshimiwa Shally Raymond, Mheshimiwa Mwijage, Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja hizi nimezijumlisha zote na majibu yake ndiyo hayo kwamba ndugu zangu hawa ndio wamechangia kwa kusema, lakini wapo waliochangia kwa maandishi na hoja zinafanana. Ninachoomba tu Waheshimiwa Wabunge mnivumilie. Najua hata mdogo wangu pale Mbunge wa Mikumi ananiangalia hajasema sana lakini huko nje anasema sana. Najua ndugu zangu mnaniangalia sana, lakini mengi mnasema hata nje huko tumeongea mengi sana. Nimewataja majina hapa ili wajue wananchi huko kwamba hawa wamechangia kwa kusema. Lakini pia zipo hoja hapa ambazo nitazizungumza zimezungumzwa na hawa wafuatao lakini kwa kuandika, wasije wakasema hawa wabunge wetu ni mabubu hawakusema, hapana upo utaratibu. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo waliochangia hapa kwa kuandika vilevile. Hoja hizi ni hizi ambazo nitazisoma baadae lakini waliochangia ni Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mheshimiwa Mwita Waitara, Mheshimiwa George Lubeleje, Mheshimiwa Charles Mwijage, Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mheshimiwa Mussa Sima, Mheshimiwa Juma Hija, Mheshimiwa Silafu Maufi, Mheshimiwa Halima Mohamedi, Mheshimiwa Risala Kabongo, Mheshimiwa Engineer Ngonyani, Mheshimiwa Aida Joseph, Mheshimiwa Shabani Omary na Mheshimiwa Mary Pius Chatanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine ni, Mheshimiwa Allan Kiula, Mheshimiwa Paschal Yohana Haonga, Mheshimiwa Saumu Sakala, Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mheshimiwa Lucy Owenya, Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mheshimiwa William Olenasha, Mheshimiwa Ritta Kabati, Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mheshimiwa Desderius Mipata, Mheshimiwa Haji Kai, Mheshimiwa Zuberi Kuchauka, Mheshimiwa Ignas Malocha, Mheshimiwa Bhagwanji, Mheshimiwa Frank George, Mheshimiwa Mbarouk Salim, Mheshimiwa Maftaha, Mheshimiwa Gibson, Mheshimiwa Mendrad Kigola, Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mheshimiwa Lucia Mlowe, Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mheshimiwa Daniel Nicodemus, Mwenyekiti pia umechangia na lile shamba lako nitalifuatilia.
Waliochangia wengine ni Mheshimiwa Daniel Nicodemus, Mheshimiwa Constantine Kinyasi, Mheshimiwa Mbarouk Salim Ali, Mheshimiwa Esther Matiko, Mheshimiwa Omari Kigua, Mheshimiwa Dunstan Kitandula, Mheshimiwa Magdalena Sakaya, Mheshimiwa Ally Ungando, Mheshimiwa Joseph Haule, Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mheshimiwa Willy Qambalo, Mheshimiwa Pascal Yohana, Mheshimiwa Sikudhani Chikambo, Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mheshimiwa Esther Matiko, masuala yako ya upimaji wa Mji wa Tarime nimeyazungumza hapa.
Wengine ni Mheshimiwa Joseph Mbilinyi, Mheshimiwa Mpakate Daimu Iddi, Mheshimiwa Davidi Silinde, Mheshimiwa Jitu Soni, Mheshimiwa Harrison Mwakyembe na Mheshimiwa Daniel Mtuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimalizie kwa kuwashukuru sana benki ya dunia kwa msaada mkubwa sana wa fedha nyingi ambazo hazikuoneshwa hapa lakini zilipitia Ofisi ya Waziri Mkuu ambazo matumaini yangu ni kwamba mwakani mnaweza mkaona vitu fulani fulani kwa macho ambavyo vimefanywa kutokana na fedha ambazo hazikuombwa kwenye bajeti yangu. Bajeti yangu inaonekana nyepesi sana, lakini kuna fedha ambazo zipo kule kwenye Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kama nilivyosema zaidi ya dola milioni 25, hazijafanya kazi ya kutosha lakini katika kipindi cha mwaka huu wa fedha mtaona matokeo yake. Nawashukuru sana Benki ya Dunia.
Katika mradi huu wa awali wa kupanga, kupima na kumilikisha Wilaya tatu wenzetu wa Denmark, Sweden na Uingereza wanatusaidia sana nawashukuru sana nao. Lakini nawashukuru sana watu wa Benki Kuu ya Tanzania ambao wanasimamia sana masuala ya mortgage finance, tunashirikiana nao nazishukuru na benki zote 29 ambazo zinashiriki katika utoaji wa mikopo ya nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwa uchache niwashukuru hao na kwamba tutaendelea kushirikiana nao. Kuna hoja nyingine ambayo imetolewa hapa kuanzia Bunge lililopita la uanzishwaji wa Real Estate Development Authority. Tunajua ujenzi wa majumba sasa na biashara ya majumba imekuwa kubwa, kwa hiyo tumeamua sasa tutaleta sheria hapa Bungeni. Imeulizwa sana kuanzia Bunge lililopita Bunge hili la mwaka huu tutaleta sheria ili angalau nchi iweze kutambua na kusimamia sekta hii muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naommba nirudie tena kuwashukuru kwanza Kamati yangu nataka kusema Kamati yangu kama wenzangu mmepata Kamati mimi nimepata yakwangu nzuri sana, ina watu waliotulia, ingawa wengi wageni lakini ni watu wenye uzoefu na waliotulia wanatoa ushauri mzuri, nawashukuruni sana. Sikusema mengi kwa sababu ninyi mkisema kwangu ni maagizo, kwa hiyo maagizo yenu na maelekezo yenu nitayafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la KDA ndugu zanguni mnajua tulikotoka, tulikofikia, sasa naomba ushauri wenu huo, nimeupokea lakini narudi ng‟ambo kule Kigamboni nikakae na wadau wa KDA, wananchi wa Kigamboni ili tuzungumze tuelewane alafu tunashauriana ndani ya Serikali the way forward.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuwahahakishieni, hakuna pesa humu lakini mimi ninazo shilingi bilioni saba tulikuwa hatujazitumia kwenye bajeti hii kwa ajili ya kuanza kulipa fidia ya watu wachache ambao wapo barabarani. Haziko hapa kwa sababu ziko kwenye bajeti hii ninazo ziko kwenye Mfuko wa Amana na Waziri wa Fedha anajua tunazo sio kwamba, pale hatufanyi, hatufanyi tu kwa sababu hatujamaliza kazi ya kuainisha lakini hatujaenda kujadiliana na wananchi wa Kigamboni juu ya utaratibu wa ulipaji wa fidia na kiwango cha fidia maana huwezi kuwashtukiza. Kwa hiyo kuna kazi inaendela kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekubaliana na kwa watu wa kigamboni; madiwani wote wa Kigamboni wameshaniandikia barua niende kwao kwa sababu mambo haya huwa tunaenda hatua kwa hatua, tunazungumza na tunaelewana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo nataka kuwahakikishia wenzangu wote wenye hofu ya Kigamboni muondoe hofu. Lakini ushauri wenu tumeuchukua. Ikiwa kunahitajika marekebisho fulani kwa sababu mlitunga sheria ya kuanzisha mamlaka hii tutairudisha hapa ili mfanye marekebisho. Hata kama ikiwa ni kufuta tutairudisha ili tuifute.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishieni kwamba, tunazo fedha tutafanya mambo machache. Kuanzini sasa kama nilivyoagiza, masuala ya utoaji wa hati katika eneo lile nimeyafungulia, wataanza kupata hati. Kwa sababu kwa miaka yote hii watu walikuwa hawaruhusiwi kupata hati na kupata vibali vya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, midhali sasa michoro imekamilika na yale wanayotakiwa kujenga kwenye site yao yanajulikana kwahiyo nimeshawaagiza wangu tuanze kutoa vibali vya ujenzi kwa watu wanaojenga kulingana na michoro inavyoelekeza katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini watu wenye ardhi yao wapewe hati ili wapate nguvu ya ku-bargain na hao wawekezaji ambao watawekeza fedha katika maeneo hayo. Kwa hiyo, haya mawili nitayafanya lakini naomba nisiwapotezee muda mrefu nitazungumza na wadau wa Kigamboni kwa niaba yenu nafikiri tutaelewana maana tumeshaelewana mambo mengi hapa nafikiri tunaenda vizuri.
Kwa hiyo, ndugu zanguni nataka nikiri kwa mbali, mambo mlioniandikia ni mengi, mambo mlionishauri kwa mdomo ni mengi lakini mengi ni migogoro. Msingi wa migogoro kwanza nataka mnisaidie marekebisho ya sera, ambayo itarekebisha hata sheria zijazo, lakini pili maana yake naomba mnikaribishe tunapiga hodi tutakuja Mkoa kwa Mkoa kusimamia utatuzi wa migogoro hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana mniunge mkono mnipe pesa hizi ili angalau nianze safari hata kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.