Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Dr. Charles John Tizeba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi nitachangia katika maeneo mawili, nitachangia kuhusu sera ya uhifadhi na baadaye nitachangia katika migogoro ya wafugaji na Serikali.
Mheshimiwa Menyekiti, sera ya uhifadhi shirikishi ni sera nzuri sana. Ukiisoma utaona ni kwa namna gani sera ile inavyozingatia maslahi ya wananchi katika uhifadhi wa maliasili za aina zote. Lakini kuna tatizo kubwa sana katika utekelezaji wa hii sera, kwa sababu sheria na kanuni zilizotungwa kuhusiana na hii sera hazitoi nafuu yoyote kwa wananchi, zimeegemea upande mmoja na nitatoa mifano kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, uhifadhi shirikishi wa misitu, utakuta msitu wa Serikali au shamba la miti liko eneo fulani. Wananchi kwa mujibu wa sheria wanalazimika kushiriki katika kuhakikisha kwamba shamba lile la Serikali haliungui moto, halihujumiwi, haliibiwi, halifanywi nini kadhalika na kadhalika. Lakini inapofika muda wa kunufaika na hilo shamba hao wananchi waliokuwa wakiambiwa hayo yote hawaonekani kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mdogo nilikuwa namuuliza hapa Mheshimiwa Kigola wa Mufindi, kwamba hivi huko Mufindi ndugu yangu wananchi wa vijiji vyako shule zao madawati yamo? Jibu hapana!
Mnafaidikaje? Ananiambia kuna baadhi ya vijiji wanapata pata kimgao kidogo hakitoshi hata kuezeka nyumba tano, kumi za walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sasa nimuombe sana Waziri, nilimsikia juzi Mheshimiwa Naibu Waziri alikuwa huko Kusini, nilisikia vyombo vya habari sasa sijui kama ni kweli na nitaomba sana athibitishe hili jambo kwamba sasa Wizara imeelekeza ugawaji wa quater zile za kuvuna katika mashamba haya ya Serikali ushirikishe pia vijiji viliyo katika maeneo hayo, yaani ya Serikali za Vijiji zilizo katika maeneo hayo. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri katika ku-close hotuba yako mtupe basi huo uhakika tusije kutoka hapa tunaamini tuliyasikia kwenye vyombo vya habari kumbe si hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa pili uko kwangu inasikitisha sana, Msitu wa Buhindi uko pale, unaomba Mbunge au Halmashauri mpate mgao wa miti ili muondoe tatizo la madawati, mnapewa cubic meter 100. Cubic meter 100 hizo Mheshimiwa Waziri hatupati bure tunapewa kama mfanyabiashara wa mbao, tunaambiwa na zenyewe tuzilipie. Sasa muanze kupitisha mchango kwa wananchi ili kulipia cubic meter 100 kwenye shamba la umma. Haya mambo yako chini ya uwezo wa Mheshimiwa Waziri, hayahitaji sheria, ayafute tu.
Mheshimiwa Mwenyekti, wananchi wale ndio wanaoutunza ule msitu, sasa iweje tena ikifika wakati wa kuvuna wanaambiwa walipie fedha ili kupata miti kadhaa pale kwa ajili ya kujengea darasa la umma, kujengea zahanati ya umma, kujengea nyumba ya mwalimu ya umma? Nikuombe sana, lakini pia msemaji mmoja amewasifia TFS kwa kukusanya sana mapato, nadhani yuko kule bwana kwanye kambi ile kule. Nakubaliana naye kabisa wenzetu wale wanajua kweli kukusanya, lakini sasa wanakusanyaje? Swali la pili hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka miwili iliyopita kwa mfano katika hifadhi za Serikali hizi ambazo kulikuwa na wananchi wanafanya shughuli zao mbalimbali, kwa ruhusa ya TFS watu hawa walikuwa wanatozwa kiasi kidogo tu cha kuwa kule ndani shilingi 64,000 kwa mwaka. Hawa watu walioko kule wanaganga njaa hakuna matajiri kule. Baadaye ghafla imetungwa kanuni nina hakika sio wewe Mheshimiwa Maghembe, atakuwa aliyekutangulia. Imetungwa kanuni watu hawa wanatakiwa walipie shilingi 74,000 kwa square meter moja. Sasa fikiria huyu mtu, mvuvi, na hili nadhani Mheshimiwa Mwigulu unafahamu tulishakuambia, mvuvi anazo kodi zingine 13 tofauti, lakini hata makazi tu kwenye eneo anakofanyia kazi anaambiwa alipe shilingi 74,000 kwa square meter moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mvuvi wa dagaa anahitaji eneo la kuanikia dagaa. Sasa lile linapigiwa na lenyewe hesabu, square meter moja shilingi 74,000 mtu kama ana square meter 20 shilingi milioni moja sijui kiasi gani uko. Watu wanatozwa mpaka shilingi milioni tano, wale maskini wale wanaambiwa walipe shilingi milioni tano hutaki toka, Sasa haya mambo siyo mazuri sana na nimemuomba Mheshimiwa Waziri kwa kweli liko ndani ya uwezo wako, hili unaweza kulifuta mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye hili la migogoro ya wafugaji na Serikali, mimi nasema mgogoro wa wafugaji na Serikali na si mgogoro wa wafugaji na wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri Serikali yote iko hapa, hivi tafsiri ya ufugaji wa kisasa kwa leo ni ipi? Maana tunaambiwa kuchunga ni vibaya kwa hiyo, wafugaji wapunguze mifugo yao kwa sababu wanachunga. Lakini yule anayegawiwa ranchi pale Kitengule au wapi, huyo anaonekana na mfugaji mzuri kwa sababu amekatiwa kipande cha ardhi na mifugo yake iko mle ndani. Be it 300, 1,000 kwa sababu ina kipande cha ardhi amegawiwa huyu ni mfugaji mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yule ambaye hajagawiwa kipande rasmi na Serikali ni mchungaji, ni mtu mbaya, apunguze mifugo yake. Niombe sana tupate kwanza tafsiri ya ufugaji uliokuwa mzuri, ni ule wa ng‟ombe ndani ya banda unakata manyasi unaweka au namna gani. Lakini tatizo langu sio tu hapo, tatizo ni sera yenyewe ya mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya mifugo haikwenda mbali ikaitazama mifugo hii wakati wa majanga, sisi binadamu tumejiwekea kinga kwenye mazao kwa sababu tunakula sisi, kwamba ikitokea jua likawaka sana wananchi wakaacha kuvuna kwa vile ni binadamu basi tulianzisha NRFA na kadhalika. Utaratibu upo ulionyooka wa kuhakikisha watu hawafi njaa, mbona hatuweki utaratibu wa mifugo kuhakikisha haifi njaa? Mifugo si tunaihitaji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa sababu ya muda Mheshimiwa Waziri, haitoshi hapa mimi nikaelezea mimi ninachokifikiria chote, nitakuomba tu kabla ya kesho jioni tafuta muda hata wa dakika 20 tuzungumze niseme ninachokifikiria kuhusu hili jambo. Tunaweza kabisa katika Awamu hii ya Tano tukaweka nyuma suala la migogoro ya Serikali na wafugaji kwa sababu uwezekano huo upo na Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kumaliza tatizo la hivi, wako wengine wameshafanya na hawana habari tena na migogoro ya hifadhi na vitu vya namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanakuandama tu, Maghembe na migogoro ya wafugaji, si lako hili ni mtambuka mno. Linahitaji ushirikishwaji wa Serikali nzima ili kuhakikisha kwamba tatizo hili linakwisha kabisa na miaka ijayo wananchi waendelee kufanya ufugaji usiokuwa na shida na kilimo kisichokuwa na shida; kwa sababu issue inayosumbua wafugaji ni pale mifugo yao inapokosa malisho basi. Mifugo kama ina malisho huwezi kumuona Msukuma anatoka Meatu anakwenda Sumbawanga…
MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango mzuri.