Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nianze kwa kuwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Bunda, kwa kunipa nafasi ya kuja hapa Bungeni na mimi nijumuike na wenzangu katika kuwatetea Watanzania wenye matatizo mengi. Nianze kwa migogoro ya moja kwa moja, migogoro ya wafugaji na hifadhi za wanyama pori.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mengi hapa, lakini kwenye Jimbo langu la Bunda kuna eneo maarufu linaitwa Kawanga, na mimi niombe kwa kusema wazi tu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, ng‟ombe ana laana, toka mmetunga Sharia hii ya wanyama pori ya kukamata ng‟ombe mnamfanya kama nyara, mnamkamata porini hachungi na mnampiga risasi, Mawaziri zaidi ya tisa wamesha toka humu ndani; ng‟ombe ana laana. Kwa hiyo, yeyote anayeshughulika na ng‟ombe vibaya ajue mambo yake yatakwenda vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano tu eneo la Kawanga. Eneo hili mwaka 1974 alikuja Mwalimu Nyerere pale kama kijiji cha ujamaa, akawashauri wananchi wa maeneo yale kwamba jamani acheni maeneo ya malisho. Wakavuka Mto Lubana wakaacha eneo la Kawanga, wakawa wamechimba malambo mawili makubwa ya Chifu Makongoro, wananywesha mifugo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1994 ukaja ujanja ujanja eneo hili likachukuliwa kama game reserve, Ikolongo Game Reserve na Grumeti Game Reserve, pori la akiba.
Mheshimiwa Mwwenyekiti, kwanza huwa najiuliza hivi pori la akiba maana yake ni nini? Mwalimu alisema hivi vitu vya akiba viwepo pale ambapo wananchi wana shida wapewe nafasi.
Sasa inavyoonekana mapori ya akiba yote ni ya wanyama pori, ikija kwa binadamu nongwa. Leo ikitokea operation ya kuzuia tembo asiende kwenye mashamba ya watu na operation ya kwenda kuzuia ng‟ombe wasiende porini, operation ya ng‟ombe inachukua nafasi. Kwa sababu ng‟ombe wanakuwa na faida ukiwatoa kwenye operation unawakamata unawatoza, wanatoa hongo na mnawauza sijui hela za ng‟ombe zinazouzwa zinaenda wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Pori la Kawanga wakahama watu, mkalifanya Pori la Gruneti, malambo mawili yako upande ule, mpaka wetu ni mto, na mto ule maana yake ng‟ombe akivuka tu, amekamatwa ndivyo mpaka ulivyo. Lakini kutoka kwenye mpaka wa Mto Rubana kwenda kwenye watu, unatembea nusu kilometa kwenda pale mbele, ndiyo buffer zone yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi najiuliza kama wananchi wa maeneo yale tembo wanakula mazao yao, ngo‟mbe hawavuki kwenye Mto Rubana, malambo yao mmechukua na hamkufidia halafu mnasemaje tuna mahusiano mabaya na ninyi? Profesa Maghembe mimi naomba nikuambie hivi, pengine kule Mwanga ninyi Ubunge wenu wakati fulani akisema fulani mnapata. Sisi Ubunge wetu ni wa kazi, kuna maeneo mengine Ubunge akisema mkubwa fulani watu wanapewa, lakini sisi Ubunge wetu mpaka utoe jasho ndipo upate. Sasa naomba uje Kawanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina ugonvi na wewe, na mimi nikuambie wazi wala huna ugonvi na Wabunge, tatizo lako ni kwamba una-attack ng‟ombe, kwa nini una- attack ng‟ombe sisi tunaolea ng‟ombe. Mimi mke wangu ametoka ng‟ombe namuita Nyabulembo, sasa wewe una-attack ng‟ombe mara kwa mara kwa nini? Tunataka ng‟ombe kweli watoke porini sawa, lakini watoke kwa mpango maalum. Hivi kwa nini majangili wamewashinda porini mnang‟ang‟ana na ng‟ombe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hapa kwenye ripoti ya wapinzani hapa, anasema kwamba ujangili ni mfupa uliowashinda CCM. Na kila siku asubuhi, hata leo asubuhi nimesikia, kwamba kiongozi mmoja mhifadhi wa wanyama pori sijui amekamatwa na pembe za ndovu. Sasa kwa nini msishughulike na hawa mnashughulika na ng‟ombe? Profesa achana na mambo ya ng‟ombe watakulaani hapa. Naomba uje Kawanga uangalie mpaka ulivyo ni mbovu. Lakini ndugu zangu Wabunge tunaotoka kwenye maeneo ya wafugaji, naomba niwaambie wazi, hizi kanuni na sheria za wanyama pori zitaua watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni zitaua humu ndani, sheria hii imeandika ng‟ombe ni kama nyara, akikamatwa anapelekwa mahakamani, akionekana ameingia porini auzwe. Ng‟ombe wa Usukumani, ng‟ombe wa Jimbo la Bunda, ng‟ombe wa Tarime na maeneo mengine ana tofauti gani na ng‟ombe wa Ngorongoro? Ng‟ombe wa Ngorongoro anachunga na wanyama, kwani ile sheria ya Ngorongoro imekuwa ni sheria ya Mungu haibadiliki? Sheria ya Ngorongoro ambayo ng‟ombe wanachunga na wanyama haibadiliki imekuwa ni sheria ya Mungu? It’s too rigid haiwezi kubadilika. Tuone maeneo mengine ambayo yanahitaji uhitaji wa Ngorongoro wapelekewe hiyo sheria. Profesa nakuomba uje Bunda, uangalie eneo la Kawanga tuone ni namna gani tunafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo. Nakupongeza kwa maana ya kwamba msimu mdogo uliopita umenisaidia sana, tembo kidogo, watu wamevuna. Lakini ndugu zangu Wabunge na ndugu zangu Watanzania, mnyama tembo, mama mmoja tulienda kwenye mkutano akatuuliza hivi, hivi hao tembo hawana uzazi wa mpango? (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana kama wamezidi tuwafanyie uzazi wa mpango, tembo siku hizi wanakwenda kwenye maghala, wanaangusha maghala wanakula mazao. Maeneo ya Bunda, Unyari, Kiumbu, Mariwanda na kwa Mheshimiwa Ester Bulaya pale Bukore na Mihale wanakula mazao asubuhi na mchana na Profesa upo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipiga kelele hapa mnasema tumekuwa wabaya, watu hawa wanaozunguka wanyama pori hawa, mazao yao yanaliwa fidia haipo. Tunadai fidia zaidi ya milioni 400 hamjalipa kutoka mwaka 2012 mpaka leo, na wanakula mazao kila siku na magari mnayo, watu mnao, mkiambiwa mnasema kwamba Halmashauri ndiyo ilinde wale wanyama. Halmashauri ina askari pori mmoja na gari bovu halipo na Halmashauri hazina own source. Halmashauri hazina hela unawaambia walinde tembo watalinda saa ngapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu mbaya zaidi Halmashauri alinde tembo, asipolinda tembo anakula mazao, wakila mazao mnalipa nyie hivi kwa nini mpo hasara sasa? Kwa hiyo nilikuwa nafikiri kwamba ni vizuri ukaangalia. Lakini mambo mengine niseme mapambano ya kuzuia ujangili yaendelee kuwepo, kuimalisha misitu yetu muendelee kuimarisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumze kidogo juu ya TFS. Hao TFS ulionao nikushukuru kwanza umewashughulikia, ni jipu. Haiwezekani kwenye makusanyo yao, kila mwaka asilimia 100, asilimia 200, asilimia 150 uliona wapi? Yaani kila makusanyo ya TFS asilimia 100, asilimia 250, asilimia 300 uliona wapi? Angalieni makusanyo yao asilimia walizokusanya kila mwaka, asilimia 120, asilimia 110, asilimia116 kila mwaka, wao makadirio yao yanakuwaje mpaka wapate hizo asilimia? Kwa hiyo, mliangalie hili nalo hao watu inawezekana wakawa jipu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia ya shilingi milioni 400 watu wa Bunda unawalipa lini? Hii fidia sijaiona kwenye bajeti yako. Profesa ukija hapa uniambie kwamba hii kitu unalipa lini. Lakini naomba kuanzia leo na kwenda muda unaokwisha, kwa muda wa mwezi mmoja na nusu naomba mtusaidie kupata magari ili watu wale wapate mavuno yao. Wamebakiza mwezi mmoja tu, tembo leo wanaenda usiku na mchana na kama hamuwezi, Profesa ngoja nikuambie, Marekani ni wanjanja sana lakini wanaishi na Mexico. Waliona haiwezekani kuishi na Mexico maskini na wao wakiwa matajiri, ikabidi wawafadhili wao wapate hela. Hamuwezi mkafanya wananchi wanaozunguka maeneo ya pori, mkasema eti mtakuwa marafiki wakati ninyi mnawanyonya haiwekani, lazima muwafadhili ili waweze kuishi na wanyama vizuri. Na ninyi niwaambie huku Serikalini… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.