Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nipo lakini hukuniambia mapema.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Naitwa Japhary Michael, Mbunge wa Jimbo Moshi Mjini. Nichukue fursa hii kuwashukuru wananchi wa Moshi Mjini ambao wamenichagua kwa kura nyingi sana pamoja na Madiwani wangu kuongoza Halmashauri ya Manispaa ya Moshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo machache ya kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Rais. Kabla ya hayo, nataka nitoe observation yangu niliyoiona katika kuchangia huku. Ukiangalia ndani ya Bunge hili utadhani kama vile Serikali tunayoizungumzia leo
imeanguka jana, haikuwepo katika nchi hii kwa hiyo, matatizo yaliyopo hawahusiki nayo. Kwa bahati nzuri kwa zaidi ya miaka 50, Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa matatizo ya Taifa hili kwa vyovyote vile yanawagusa kwa kiwango cha kutosha kabisa. Kwa hiyo, naona kama vile
kuna watu wanaomba toba, sasa ni wajibu wa wanaoombwa toba kukubali au kukataa.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja kwenye hotoba ya Rais pale anapozungumzia habari ya ushirikiano wa Serikali yake na Halmashauri. Nimekuwa Diwani na nimekuwa Meya kwa miaka kumi sasa hivi. Tunapoelekea niiombe sana Serikali ijitahidi kuishi
katika dhana ya decentralization, ya kupeleka madaraka kwa wananchi, izipe mamlaka ya kutosha Halmashauri za Wilaya, Majiji na Manispaa kama sheria inavyosema kwamba madaraka yatatoka kwa wananchi. Hali inavyoendelea, Halmashauri zimekuwa zikiongozwa kwa miongozo, waraka, maagizo na kusababisha leo hii watendaji wengi wa Halmashauri na Madiwani wanakosa creativity (ubunifu). Kwa hiyo, wanajikuta siku zote wataishi kwa maagizo ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais, Ofisi ya Waziri wa TAMISEMI na matokeo yake kiukweli
mambo mengi yanaenda ndivyo sivyo. Kama tunataka wananchi watumikiwe vizuri na ndivyo alivyoelekeza Mheshimiwa Rais, ni vizuri mamlaka zile zipewe power inayostahili ambayo itaweza kuwafanya waweze kuzitumia rasilimali za Taifa vizuri na kuzifanya ziwe na ufanisi na tija kwa wananchi wa taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata maslahi ya Madiwani, Wenyeviti wa Mitaa, huwezi kumwambia Mwenyekiti wa Mtaa hana chochote lakini anaitwa Mheshimiwa, ndiye anatakiwa apokee watu waliogombana kwenye ndoa zao, ndiye anatakiwa apokee kila tatizo halafu hapati chochote ambacho kimeelekezwa na Serikali, mnaziachia Halmashauri ziamue zenyewe wakati hazina hata uwezo wa kujiendesha zenyewe. Ni vizuri Serikali iliangalie hili kwa ndani sana namna gani itasaidia Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ziweze kujiendesha vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie suala la utalii. Jimbo naloongoza lipo karibu sana na Mlima Kilimanjaro. Kama tunataka kuuendeleza utalii ili tuweze kukuza uchumi wa nchi hii ambapo tunafikiri kuwa na mawanda mapana katika viwanda, ni vizuri tujitahidi
kuuboresha utalii na hasa tuutumie vizuri Mlima Kilimanjaro.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Uwanja wa Ndege wa Moshi umekuwa kama gofu lakini hautumiki vizuri. Uwanja huu ungeweza kusaidia watalii wanapotoka kwao waje moja kwa moja pale na uongeze mapato na uchumi wa Mji wa Moshi lakini pia ungesababisha Mji wa Moshi
ukue kwa haraka. Mji wa Moshi umekuwa kwa taratibu mno kama vile siyo Mji Mkongwe na wa zamani. Naomba sana Serikali ilione hili kwa mapana yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la rushwa na ufisadi ambalo limezungumzwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais na kwa sauti kubwa sana. Naomba kwa dhati kabisa, katika Bunge lililopita wakati linamaliza muda wake, Mheshimiwa Halima Mdee, alileta kwenye
Bunge hili Tukufu hoja ya udanganyifu uliofanywa na taasisi fulani kupitia RITA wa kughushi saini za marehemu na wakabadilisha Bodi ya Wadhamini wa taasisi hiyo ili wapore eneo ambalo Halmashauri ya Manisapaa ya Moshi imelikalia zaidi ya miaka 20. Hoja hiyo imekuja hapa lakini Mbunge aliyeleta hoja ile hakupewa majibu na leo watu wale wamebarikiwa, wamekabidhiwa udhamini wa ile taasisi na tayari kiwanja kile kimeshachukuliwa na hiyo taasisi na kimeuzwa kwa watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumza habari ya ufisadi, lazima tumsaidie Rais, seriously. Tukizungumza mambo kama hatuko seriously tutakuwa tunazungumza mambo yaleyale, kwa sura zilezile na matokeo yatakuwa ni yaleyale. Kwa hiyo, ni lazima tuwe na
jitihada za kutosha kwa yale ambayo tunataka kuiaminisha jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la hali ya watu wa chini ambalo kimsingi ukiliangalia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais limeongelewa kwa mapana yake na amelenga zaidi huko, hali ilivyo na kwa namna utekelezaji wake unavyoendelea watu wa chini siyo muda mrefu
wataichukia Serikali. Kwa sababu inaonekana kiukweli, kumekuwa na matamko mengi ambayo yanawaumiza watu wa chini. Ni lazima tukubaliane kuna mambo ya msingi ambayo hatuna nafasi ya kuyafumbia macho, hatuwezi kufumbia macho uhalifu wa aina yoyote katika
Taifa hili wa ufisadi na rushwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kuna mambo yanahitaji huruma ya kawaida tu hasa ikizingatiwa kuwa Serikali ni ileile kwa muda wa miaka 50 na mambo mengine mmeyasimamia ninyi leo mnapokwenda bila jicho la ubinadamu mnawafanya wananchi
wasiwaelewe na hasa wa hali ya chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unapokwenda ukavunja nyumba ya mwananchi wa hali ya chini ambaye pato lake ni la chini mno wakati miaka 50 amekaa katika eneo hilo ndani ya utawala wa chama hichohicho, ni hatari sana. Ni lazima tujitahidi kuwa watu wenye huruma, wenye ubinadamu kama ambavyo hotuba ya Mheshimiwa Rais imejaribu kuonesha kwamba tujielekeze huko, tuwahurumie hawa watu wa chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini namna gani tunaweza kuwasaidia watu wa chini kama Wamachinga na wachuuzi mbalimbali, lazima tuone kwamba hakuna Taifa lolote duniani watu wamekuwa matajiri bila kuanza katika hiyo primitive accumulation lazima tujitahidi kuona
tunawasaidiaje watu hawa. Alichotuagiza Rais ni kwamba watendaji wabadilishe spirit na attitude zao, wawe na tabia ya kuwa wabunifu ni namna gani watengeneze mazingira rafiki kwa hawa watu wa chini kuweza kusaidiwa na sio wawe watu wa kuwabugudhi na kuwaumiza,
ni lazima hilo lifanyike kwa nguvu zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri anapokwenda kuongea na wananchi akaongea kibabe ni hatari wakati akienda kuomba anaomba kiungwana na kama binadamu. Namna mnavyoomba kura ni namna hiyohiyo mnatakiwa muwatumikie wananchi ili waone kwamba
siku zote mko nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuishauri Serikali, lazima sisi wanasiasa maana Mawaziri hamvui vazi la siasa ninyi bado ni wanasiasa, mnapozungumza na wananchi…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Japhary muda wako umekwisha, tafadhali naomba ukae.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)