Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipa nafasi katika kuongelea Wizara hii muhimu sana katika nchi yetu. Bila Wizara hii kuwepo vyanzo vya maji vyote vingekauka, kama Wizara hii haikuwepo hakuna miti katika nchi hii, ingekuwa jangwa. Kusema kweli lazima tufuate sheria. Leo kuna maziwa kwenye bahari, Lake Tanganiyika, Lake Nyasa, Lake Rukwa, Lake Victoria na mwambao wa bahari, lakini nyavu haramu zinakamatwa zinachomwa hatusikii kelele. Kwa sababu wanakwenda kinyume na sheria. Watu wanaojenga kwenye road reserve wanavunjiwa maghorofa yao, hatusikii kelele. Lakini kelele ng‟ombe anapoingia kwenye Game Reserve au National Park tunasikia kelele, kwa nini tusikie kelele? Tufuate sheria, kila kitu kina mpaka wake, haiwezekani mimi leo niingie kwenye nyumba ya mtu bila hodi. Ile ni sheria, ni nyumba zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazungu na ubaya wao, lakini tangu enzi za zamani walikuwa wanaita mashamba ya bibi, ilikuwa mwiko hata kuchuma jani. Leo tunakwenda kuchoma pori, tunafanya tunavyotaka na kila kitu, lazima tufuate sheria ndugu zangu. Morogoro tulikuwa tunaita Morogoro maji yanatiririka, leo Morogoro maji yako wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri, kabla ya Bunge kuisha nipe magari kwenda kwenye doria kule Lwafi Game Reserve na Rukwa, kupambana na waingiza mifugo mle ndani, wanatuharibia mbuga zetu. Nilizungumza na Mheshimiwa Nyalandu hapa akiwa Waziri, alikuwa tayari kunipa gari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaingiza ng‟ombe kule, tuna mbuga kule, game reseve ya kilometa 6,800 lakini hakuna gari, majangili wanaua tembo hovyo, leo hata mavi ya tembo hatuyaoni. Wanachoma pori hovyo, ng‟ombe wamekuwa ndiyo nyati badala ya nyati mle ndani, hatuwezi kukubali, sheria zifuatwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kugeuza jangwa ndugu zangu, nchi itakwenda wapi? Tutapata wapi maji ya kunywa! Bora mimi Lake Tanganyika inaweza ikawa na maji mengi, ninyi mtakwenda wapi, Dodoma itakwenda wapi? Acheni kuwa na jazba, fugeni ng‟ombe kama Denmark, Denmark wana ng‟ombe chache lakini wanauza maziwa nchi nzima. Leo mnafuga ng‟ombe, ng‟ombe moja ana kilo 70 unasema una ng‟ombe! Hatuwezi kukubali kuharibu mazingira kwa ajili ya wafugaji, hatutakubali!
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wetu ni asilimia 75, wewe umezungumza wafugaji milioni mbili na wakulima wako wangapi nchi hii? Leo hawana sehemu ya kulima, watakosa maji wakulima wetu, tutapata wapi chakula tukikosa mvua, hatuna uwezo wa kumwagilia nchi nzima, kwa hiyo, ndugu zangu lazima tufuate sheria. Game reserves zipo kwa sheria national parks zipo kwa sheria na mfugaji yupo kwa sheria na mkulima yupo kwa sheria, hatukubali mkulima kwenda kulima kwenye game reserve wala mfugaji kwenda kwenye reserves.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoma nyavu hapa kila siku mnasikia, wavuvi haramu kule Ziwa Tanganyika. Mimi mwenyewe shahidi, nilishaenda kushuhudia wanachoma nyavu za milioni saba, milioni nane, Mwanza wanachoma nyavu, Bukoba wanachoma nyavu, Pangani wanachoma nyavu, huku kote wanachoma nyavu, hatusikii kelele, kwa sababu wanavunja sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba zote zinavunjwa, juzi wamevunja nyumba Dar es Salaam kwenye njia za maji, nani anapiga kelele hapa, kwa sababu wamejenga kinyume na sheria.
Wewe unaingiza ng‟ombe wako kwa nguvu zako utegemee pesa zako na wakulima wetu wanapata shida, wanakwenda kuhonga Mahakimu, hakuna kesi ya mkulima ilishida, mimi nina ushahidi. Hakuna kesi ya mkulima na mfugaji imekwenda mahakamani mkulima akashinda, hakuna! Hatuwezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwangu kule kuna ng‟ombe 200,000 wakati tulikuwa na ng‟ombe labda 200 au 300. Wafipa ng‟ombe wao ni wa kulimia. Mfipa kabisa mfugaji ng‟ombe 50, leo kuna ng‟ombe 200,000. Na mimi nimeshazungumza, walipe kodi. Hatuwezi kuwaachia namna hii walipe kodi, wana uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi inalalamika haina hela MCC imetufinya misaada, wakati kuna mahali wanasema wana ng‟ombe wengi, hawalipi kodi hawa. Vyanzo vingi vya hela hapa mnaviacha, ndiyo maana wanakuja kutambukatambuka hapa. Sisi hatukuona siku ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi mkulima hapa nje, Wizara hii tumeona wafugaji wamejazana hapa. Ndugu zangu tukiachia watachunga ng‟ombe mpaka Ikulu. Hatuwezi, twende kwa sheria. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kule kwangu kuna matatizo, mamba ndiyo wametuzidia. Watu wangu waliumwa na mamba, tumepiga kelele walipwe hiyo fidia maana yake huwezi kulipa maiti aliyekufa, thamani yake ni kubwa sana. Lakini sheria inasema mtu akiliwa na mamba, akiliwa na tembo, alipwe. Kwa hiyo nafuata taratibu, nina watu wangu kule wameliwa na mamba Lake Tanganyika, walipwe fedha zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, lazima tuheshimu sheria nchi hii. Ni kama wewe una nyumba yako mimi nikuingilie mle ndani, ninywe chai bila idhini yako, ninywe maji bila idhini yako utanipeleka Polisi. Ni kama Katavi Game Reserve, Luafi Game Reserve, hizi zote zina sheria na sheria zimetungwa hapa Bungeni na nyingine tangu Mkoloni ametunga sheria hizi, tukiachia hivi wenyewe ndugu zangu ni mwaka mmoja hakuna mnyama nchi hii, kuna watu wanachukua national parks ndugu zangu, ajabu kabisa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila national park, bila game reserve ndugu zangu mvua hakuna, vyanzo vya maji vitakwisha. Mnaweza ninyi, mna hela Wabunge mnanunua maji ya chupa, watu wetu hawana hela ya kununua maji. Hatuna hela ya kununua maji, ni haya maji ya mvua ndiyo yanakwenda ardhini tunachimba visima. Leo miaka mitatu ikiwa hakuna maji hapa, mvua hakuna, tutakufa na ng‟ombe wenu watakufa na mbuzi watakufa na kondoo watakufa na nguruwe vilevile, mtabaki na nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nawaambia ndugu zangu, hakuna kwenda kinyume cha sheria, sheria ni msumeno, mtu yeyote anavamia ni kama vile wavuvi wanavua haramu, lazima wakamatwe wachomewe nyavu zao ili samaki waendelee kuishi. Samaki watakwisha, kwa hiyo tunaomba sheria itekelezwe. Hatuwezi kubembelezana, hatuwezi kutishana humu ndani, hakuna kumtishia mtu humu ndani. Mheshimiwa Maghembe amekuta sheria ipo. Nawapongeza TANAPA kwa kutupa madawati, kafanyeni kazi. Serikali yetu ina meno ya tembo yamejazana, msifanye kama Kenya. Uzeni, tupate pesa tununue magari na silaha kupambana na majangili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tupambane na haya majangili kwa hali yoyote. Vijana wetu hawa ma-game rangers wakienda mule ndani wanapambana kwa bunduki na yale majangali, akimuwahi anamuua. Kwa hiyo na ninyi wafanyakazi wa Serikali ma-game rangers, mtu unamkuta game reserves, national parks, mpige risasi afe! Kwa sababu ukimuachia atakuua wewe. Kaenda kufanya nini mule ndani, kwa idhini ya nani! Kaenda mfano, Katavi National Park, kufanya nini mle ndani kama siyo jangili, nani kampa idhini? Ni kumtandika risasi tu maana yake ukichelewa kumpiga risasi anakupiga wewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ni watu wabaya, tumewakamata Namanyere na bunduki nakuambia Mheshimiwa Maghembe, lakini wanaachiwa polisi. Nimekuletea ushahidi, wamekamatwa majangili na nyama ya tembo kilo 200 imepakiwa ndani ya gari linaitwa Noah, lakini siku mbili tatu wanaachiwa. Wanakamatwa na bunduki, siku mbili tatu wanaachiwa mpaka vijana wa TANAPA wanachoka! Kesi zao zinaishia hovyo hovyo tu. Nimekuletea sijapata majibu mpaka leo, nina wiki ya tatu, kwa ushahidi kabisa kwamba majangili wamekamatwa kule Nkasi lakini wanaachiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Rais Magufuli anasema, unamkamata mtu red-handed na jino la tembo, unamkamata na bunduki, na nyama ya tembo, unampeleka mahakamani anashinda kesi, red-handed! Hapa kuna nini, rushwa kubwa, siyo ndogo. Hawa dawa yao ni kule wanapokamatwa maana yake ukimpeleka mahakamani anakushinda, ni kumtandika risasi mambo yaishe huko huko mbugani. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuchezewa, kuharibu mapori yetu kwa ajili ya faida ya ninyi kizazi cha leo, kumbukeni kizazi kinachokuja. Je, miaka ya nyuma wangekuwa wanaharibu kama mnavyoharibu ninyi mikaa, kuni, ng‟ombe mle ndani, tungeishi hapa? Kumbukeni na ninyi bado mnaendelea kusihi nchi hii. Mwenyezi Mungu kawaambia dunia karibu miaka miwili iiishe? Mna ahadi ya Mwenyezi Mungu dunia karibu iishe? Kwa hiyo, kuna vizazi na vizazi vinavyokuja na hii ni mali yetu wote, lazima tuitunze na tufuate sheria, sheria ni msumeno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja.