Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni bajeti ya Serikali wala siyo ya Dkt. Mpango. Wapo watu wengine wanalaumu kama vile Dkt. Mpango hii bajeti ni ya kwake, hii ni bajeti ya Serikali inayosomwa na Waziri wa Fedha Dkt. Mpango. Kwa hiyo niwaombe sana tunapojadili tujadili bajeti, tusijadili mtu alivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri kwa Dkt. Mpango kwa sababu yeye ndiye Waziri wa Fedha, yapo mawazo mazuri sana ya Kamati, nashauri kwa mfano suala zima la maji ile tozo kutoka sh. 50/= kwenda sh. 100/= Wabunge wote, Watanzania wote, kama itaongezwa iwe sh. 100 kwa ajili ya maji, nina uhakika Watanzania watanufaika, naomba suala hili ulitazame kwa jicho jema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai, mtoto mdogo anategemea maji, akinamama kule wanategemea maji, maji yakiwa mengi vijijini kero kwa chama changu itapungua. Nakuomba sana juu ya hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, imependekezwa, Mheshimiwa Waziri najua yeye ni muungwana sana, chombo chetu kikuu, kisemeo cha Serikali ni TBC, TBC ndiyo mdomo wa Serikali, TBC ndicho chombo ambacho kinaweza kusema kwamba hapa sasa Serikali ifanye hivi, namwomba hebu atumie busara na watalaam wake, hili nalo alione. Mheshimiwa Waziri tukifanya hivyo kwa kweli tutakuwa tumefanya jambo jema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nimelifurahia sana na niipongeze sana Serikali, nimekuwa Mbunge wa siku nyingi kidogo humu ndani, Wabunge wote wa Vyama vyote tulitakiwa tuipongeze sana Serikali kwa kutenga asilimia 40 ya pesa ya bajeti kwenda kwenye maendeleo, haijawahi kutokea. Nilitegemea Wabunge wote watapongeza kwa sababu pesa hizi asilimia 40 ya bajeti ya trilioni 29 inakwenda kwenye shughuli za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri kwamba, ingekuwa ni amri yangu kwa sababu kweli tumetoka kwenye asilimia 23 tumekwenda sasa kwenye asilimia 40 lazima tuipongeze sana Serikali. Mbali na hilo katika ukurasa wa 98 wa kitabu chako, ninakushauri ile aya ya 102 unapoanza kwanza mpaka namba kumi nishauri hii ndiyo iwe kama ndiyo amri kumi kwa sababu yako maagizo kumi, hii ndiyo iwe amri kumi, sitaki kusema kwa sababu ya muda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri maelezo aliyoyaeleza hapa kuanzia kipengele cha Kwanza, Pili, Tatu, Nne, Tano, Sita, Saba, Nane, Tisa na Kumi, iwe ndiyo mwongozo kwa Maafisa Masuuli wote Tanzania. Atakayekiuka haya wala tusimwonee aibu, kwa sababu ili pesa hizi ziende kufanya kazi yake vizuri, hii asilimia 40 ya bajeti yote kama hizi amri kumi alizoziorodhesha zikisimamiwa vizuri, nina uhakika tutasonga mbele, tukifanya hivyo na naomba nirudie kusema tena hapa, Maafisa Masuuli wote waandikiwe secular kuhusu hizi amri kumi wazitekeleze. Mimi naziita amri kumi kwa sababu kwa jinsi alivyozipanga na kama kila mtu akifuata moja baada ya nyingine, nina uhakika tutafika mbali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine naunga mkono, kwanza niipongeze sana TRA kwa kufanya kazi vizuri sana. Tunawaamini, mmepewa jukumu zito, lakini niwaombe hasa kwa upande wa kodi za majengo, tukisimamia vizuri kodi za majengo, Dar es Salaam tukafanya tathmini ya kutosha, Mwanza tukafanya tathmini ya kutosha, Arusha na maeneo mengine tukafanya tathmini ya kutosha, Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuna pesa nyingi sana pale, tutaboresha miji yetu, tutaboresha miundombinu yetu, kwa sababu pesa zilizoko pale zilikuwa zinapotea bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri mwingine kwa Waziri wa Fedha na Wabunge wenzangu, naomba kuhusu misamaha ya kodi, sikubaliani nayo, lakini hebu mkae vizuri na Wataalam wako mwangalie hasa upande wa madhehebu ya dini, tusiwahukumu kiujumla tukae, tufanye tathmini ya kina, najua mmeshafanya, kwa sababu madhehebu ya dini mengine yanatoa huduma upande wa hospitali, upande wa shule. Kwa hiyo, naomba sana kuhusu hili, mkae mfanye tathmini ya kutosha ili tusilete mgogoro na madhehebu ya dini. Najua Serikali yangu ni sikivu hili italifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine niipongeze Serikali na niweke tu msisitizo, nimesema leo kazi yangu ni kushauri bajeti ijayo ndiyo tutakwenda kwa detail. Kuhusu ujenzi wa reli naipongeza sana Serikali, ununuaji wa ndege hili wala msichelewe, msisikilize yale maneno ya kule, kwa sababu najua Serikali imekaa. Nawashangaa watu wengine tulikuwa tukisimama humu tunasema Tanzania hatuna ndege sasa Serikali imekuja na mpango mzuri wa kununua ndege tatu, watu wengine wanaanza kuhoji! Jamani hivi tunataka Serikali ifanye nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nashauri asiwe na kigugumizi kununua hizi ndege tatu, atwange mzigo, alete ndege tatu hizo ili kusudi Watanzania watumie ndege zao, siyo ndege zile zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni ununuzi wa meli, chonde chonde! Meli hizi kwa jinsi ambavyo mmejipanga kama Serikali zinunuliwe bila kusuasua, hivyo maeneo ambayo tumeshaahidi kuwa tutanunua meli au kukarabati tufanye bila kuchelewa. Ili tufanye hivyo niwaombe sana wenzetu wa TRA kwa sababu tunawategemea. TRA ni kama mshipa kwenye mwili wa binadamu, ukikatika mshipa mmoja au ukisimama mshipa mmoja, ina maana eneo moja lita-paralise, kwa hiyo ili tutekeleze haya ambayo Dkt. Mpango Waziri wa Fedha ameyaainisha humu ndani ni lazima makusanyo yakusanywe na yasimamiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukusanya matumizi yetu yawe na nidhamu, tukifanya hivyo tutakwenda vizuri. Kwa kweli naunga mkono sana bajeti hii kwa sababu ina mambo mengi sana mazuri na imegusa wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo Waziri wa Kilimo ni muhimu kuliangalia, hebu tazama kwenye tozo za mazao, tumeyasema mwanzo tozo ni nyingi, ni kero, hebu ziondoeni kwa sababu zinawapa matatizo watu wetu, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumefanya kazi nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho Waziri wa Ardhi, Waziri wa Kilimo, Waziri wa Maliasili wakae pamoja waangalie namna ya kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji, yale maeneo ambayo sasa hayana sifa tena ya kuwa mapori ya hifadhi, wakae na waangalie namna nzuri wayagawe ili watu wetu, wakulima na wafugaji waweze kuyatumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.