Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi hii kuweza kuchangia hoja hii ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja hii ni muhimu sana kwa sababu suala la Maliasili na Utalii ni kitu kimoja ambacho ni muhimu na kinachangia pato kubwa kwenye uchumi wa Taifa asilimia 17.3 siyo mchezo. Sasa kuna mambo mengi ambayo yapo ndani ya Wizara hii lakini mimi ningependa kujikita kwenye mambo ya hifadhi na pili kwenye suala la utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo hifadhi nyingi sana lakini kuna hifadhi nyingine ambazo zimesahauliwa, kuna hifadhi ya misitu ya Amani kwa mfano, ni hifadhi kubwa ambayo ina hekta karibu 47,000 na ina mambo chungu nzima ndani yake. Kuna vitu ambavyo viko ndani ya msitu huo ambavyo havipatikani ulimwengu huu. Kuna vipepeo ndani ya msitu huo ambavyo huwezi kuvipata dunia yote hii, kuna kima weupe ambao wako mle, kuna nyoka wa ajabu ambayo mimi nilipata nafasi ya kuyaona pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo yapo ndani ya msitu huo na ambayo naona kama Wizara hii haikuyaona kama ni muhimu na ndiyo maana msitu wa Amani imechangiwa kidogo sana kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukiangalia kwenye page 54, page 61, 62 na 63 ni kama imeguswa tu by the way. Lakini kuna mambo muhimu ambayo yapo huko kwenye msitu wa Amani ni msitu mkubwa na msitu ambao una mambo mengi sana kuna ua ambalo liko pale huwezi kulipata dunia nzima, kule Amani wanaliita Dungulushi. Hili ni ua ambalo lina harufu ambalo likichanganya na mambo ambayo yako kule Amani mambo ya hiliki, mambo ya karufuu sasa ile mandhari yake ambayo unaipata kule ni kitu tofauti sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Maofisa wa Mheshimiwa Waziri wamesahau kitu kama hicho kwamba Amani kuna vitu ambavyo ni muhimu, Amani kuna vitu ambavyo ni vya msingi na ingetakiwa waweke umuhimu sana kwenye hifadhi hiyo ya misitu. Pamoja na msitu huu kuwa na hekta 47,000, lakini pia umezungukwa na misitu mingine midogo midogo karibu sita ambayo ipo pembeni yake. Kuna misitu midogo kwa mfano msitu wa Derema, Lunguza, Tongwe Kwani, Nilo, Kambai, Manga, Mlinga yote ni misitu ambayo inazunguka pale Amani na kuufanya ule msitu uwe mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mtafiti mmoja na mtalii mmoja ambaye alitembea hifadhi nyingi hapa duniani na alipofika pale Amani alishangaa sana namna ambavyo hatuupi ule msitu wa Amani. Aliulinganisha msitu wa Amani na Kisiwa kimoja kiko kule Amerika ya Kusini Ecuador, hicho kisiwa kinaitwa Galapagos muangalie kwenye ramani mtakiona. Kuna vitu ambavyo vina vutia zaidi sasa alipoangalia msitu wa Amani akaona msitu ulivyo jaa, ulivyo nona, akasema huu ni msitu kwa ulimwengu na hifadhi ambayo nimewahi kutembea huu unaweza kuwa wa pili duniani. Sasa hii ni kitu muhimu sana ambacho Mheshimiwa Waziri inabidi uangalie na uone umuhimu wa msitu huu ambao una kila aina ya vitu, viumbe mbalimbali ambavyo viko pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, msitu huu pamoja na kuwa ni wa asili kuna malalamiko ambayo wananchi wa Derema wako 1,128, ambao wamehamishwa kutoka kwenye ule msitu na kwamba tunaenda kuwapa maeneo mengine na wale wananchi fedha ambazo wamelipwa ni ndogo sana. Wananchi hawa wamezunguka wamekwenda Ikulu karibu sijui mara ngapi? Wamekwenda hapo Wizarani kwako Mheshimiwa Waziri sijui mara ngapi? Na mimi tu nilipokuwa Mbunge hii ni barua yangu ya tatu kukuandikia kwamba hawa wananchi 1,128 kwa nini wamepunjwa wamepewa hela kidogo mimea yao ambayo ilikuwa ndani ya hifadhi kama hiliki, karafuu ilikuwa ni mingi, lakini hela ambayo wamepewa wamekadiriwa ni kidogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, last week nimepokea barua kutoka Wizarani kwako inasema kwamba kufuatana na sheria hao walitakiwa walipwe sijui kila mche shilingi hizi, jamani, kila sheria general rules ina exception zake, kwa hiyo exception ambayo unaweza kuipa kutokana na umuhimu wa huo msitu mmeamua kuwahamisha hao watu jamani wapeni haki zao. Nitakuja kukuona Mheshimiwa Waziri, lakini ni muhimu sana uangalie namna gani mtaweza kuwapa hawa wananchi ambao wamelalamika, wamehangaika, wamekwenda kila ofisi wamekuja Dar es Salaam sijui mara ngapi kudai hizo haki zao lakini hawasikilizwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hiyo tulisema kwamba hawa tunawahamishia kwenye shamba moja la Kibaranga pale ambalo shamba hilo ni haya ambayo yamerudishwa hati, lakini shamba la Kibaranga bado halijarudishwa hati na Mheshimiwa Lukuvi, Waziri wa Ardhi simuoni hapa lakini nilishamlalamikia kwamba tunasubiri hati inyang‟anywe ya shamba hilo tuweze kuwakabidhi hao wananchi wa Derema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema kwamba kuna mambo mengine ambayo amesahau, kuna Pango la Amboni kule karibu na Muheza, Tanga pale. Sasa lile pango badala ya kuwa utalii limekuwa ni maficho ya magaidi, magaidi wako mle kila siku askari wanakwenda mle, kila siku wanawatoa, sasa sijui limesahauliwa kwamba siyo eneo moja la utalii au ni namna gani? Ninaomba Mheshimiwa Waziri suala hilo pia liangaliwe na hilo pango pia lipewe kipaumbele kwa sababu ni kitu kimoja muhimu sana. Kuna vitu ambavyo viko vya kihistoria kwenye vitu kama hivyo ambavyo tunatakiwa kuviangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Amani pamoja na kuwa na kutengeneza mbao za mitiki ni sehemu moja ambayo tunatengeneza mbao za mitiki, tuna mashamba makubwa sana ya mitiki pale. Mjerumani alitengeneza reli mpaka inafika Amani kwa ajili ya kuichukua mitiki, lakini hiyo reli imekufa na ndiyo maana nilikuwa napiga kelele kwamba ni muhimu tupate barabara ya lami ya kutoka Amani kilometa 40 mpaka Muheza. Kuna mambo chungu nzima ambayo yako pale ambayo yangeweza kuwa facilitated na huo mlima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niangalie suala la utalii kwa haraka haraka, utalii kama unavyoonekana kwa kweli haulingani, watalii ambao wanakuja hapa nchini hawalingani na vivutio ambavyo tunavyo. Tuna mbuga karibu zaidi ya 15 acha hizo hifadhi ambazo tunazo kubwa kabisa hapa ulimwenguni, nasikitika sana kusema kwamba utalii tunaingiza watalii milioni 1.1.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Victoria falls pale Zimbabwe wao Victoria Fall alone na wanaingiza watalii milioni mbili na nusu wanaingia pale kwa mwaka, tuna kila aina, jamani nafikiri Mheshimiwa Waziri inabidi uangalie namna gani ambavyo tunaweza kufanya au kuwafanya watalii waingie nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua njia moja ni hiyo kwamba hatuna ndege na ninashukuru sana kwa bajeti hii kuweka ndege. Watalii wengi wanapenda direct flight akitoka Ulaya moja kwa moja anatua hapa, kwa hiyo naamini kwamba hizo ndege ambazo zimepatikana mtazitumia vizuri na mtazipanga vizuri ili ziweze kutuletea watalii wengi hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mlima Kilimanjaro, ni muhimu sana mimi nilipata bahati ya kupanda Mlima Kilimanjaro mwaka juzi, mwezi Disemba. Ningefurahi sana mngetengeneza programu ya Waheshimiwa Wabunge wapande mlima huu ili waone huko njiani kukoje, lakini njiani hakulingani na hali halisi iliyopo huko Mlima Kilimanjaro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vibanda ambavyo viko hapo Horombo, vingine vipo pale Kibo, watu wanalala kwa shida. Mheshimiwa Mbunge mmoja alizungumzia mambo ya vyoo, mimi nilipandia njia ya Marangu naomba viangaliwe. Vile vi-hut vimejengwa miaka sijui mingapi iliyopita, ukienda pale Kibo hut kuna vibanda ambavyo vimejengwa sijui lini? Sasa hii sijui kwa sababu labda viongozi hawapandi ule mlima na kuona matatizo ambayo yako mle, lakini ni vizuri wakayatatua....
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.