Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Malinyi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba ya Wizara hii, lakini kabla sijaanza hivyo naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa neema, ameniwezesha leo kwa afya njema kusimama mbele yako na kuweza kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali yangu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli kwa mwanzo mzuri aliouanza. Tunaiomba Tanzania na Watanzania wengine wote bila kujali vyama, tumuunge mkono kiongozi huyu, ana dhamira ya kweli na tukimuunga mkono tutafika mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mchango wangu nitajikita zaidi kwenye sekta ndogo ya wanyamapori na migogoro inayoendelea baina ya mapori haya tengevu au mapori ya akiba na vijiji ambavyo vinapakana. Wenzangu wameongea sana, nitaongea kwa vielelezo zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mtakumbuka mwaka 2009 wakati tunarejea Sheria ya Wanyamapori, Bunge hili lilitoa maelekezo kwa Serikali na yalikuwa mawili, kwamba, kwa kuwa sheria zamani ilikuwa inaruhusu matumizi ya binadamu katika mapori haya ya akiba, mapori tengevu, lakini sheria ile baada ya kurejewa hairuhusu tena. Kwa hiyo, lilikuwa la maangalizo mawili, Serikali ilipewa kazi wakaifanye, lakini mpaka leo bado linasuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwanza waangalie umuhimu wa uendelezaji wa mapori tengevu hayo na mapori ya akiba. La pili, urekebishaji wa mipaka, lakini naweza kusema na wote tunashuhudia mpaka leo Serikali hawajafanya. Naomba nimwombe ndugu yangu, Profesa Kaka yangu, yeye amebobea kwenye mambo haya na hapa kama upele umepata mkunaji, hembu athubutu kufanya haya mawili. Kwa kuwa mazingira haya wananchi tunalalamika, Serikali wanashindwa kuchukua hatua, nitatoa mfano kwanye pori tengevu la Kilombero. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2012 baada ya kusisitiza kusukuma sana ndiyo kidogo walijaribu kuweka mipaka, kurejea ile mipaka ya pori tengevu baada ya marekebisho ya ile Sheria ya Wanyamapori 2009, lakini walichofanya wamemega ardhi ya vijiji na ndiyo maana mgogoro kule bado unaendelea. Maeneo ya Vijiji vya Igawa, Kiwale, Lupemenda na vijiji vingine eneo lile wamekuja kurekebisha ile mipaka wamemega ardhi yao, wananchi wale wanapotumia ardhi yao kiuhalali, ndiyo migogoro kila siku inaendelea na wananchi wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama haitoshi, badala ya kurekebisha mipaka mrudishe ardhi ile sasa kwa Serikali ya vijiji eneo lile mkatengeneza kitu kinaitwa buffer zone. Buffer zone kwenye eneo lile la bonde la Mto Kilombero kwenye Wilaya zile mbili; Malinyi na Ulanga ina range inatoka kilomita moja, maeneo mengine mpaka kilomita 12. Ukubwa wote huo wanaita buffer zone, matokeo yake sasa mmeingiza vijiji 18 na vitongoji karibu 22, vijiji na vitongoji hivyo vimesajiliwa, watu wanaishi kihalali, kuna shule za msingi, kuna mashamba, wananchi wanaishi kule kihalali, lakini wanaishi kila siku kwa hofu. Hawana amani, wanashindwa kujiendeleza kwa sababu hawajui hatima yao ni nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Kijiji cha Kiswago, kuna Kitongoji cha Salamiti, kitongoji kile kinashindwa kuendeleza shule ya msingi, watoto inabidi watoke kule kilomita 18, mtoto huyu wa shule ya msingi miaka saba aende mpaka shule ya msingi Kiswago kwenda na kurudi kilomita 36 kwa siku. Matatizo yote haya ni kwa sababu bado wameng‟ang‟ania, bado hawataki kutoa uamuzi ili maeneo ambayo wametenga kama buffer zone watayarejesha kwenye ardhi ya kijiji ili wananchi waendeleze pale kwa maendeleo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nimesema na mara ya mwisho na mpaka Bunge lililopita watani zangu majirani walikuwa wananiita mzee wa buffer zone na nitaendelea kwa sababu Serikali bado kila wakiambiwa hawasikii. Mara ya mwisho kuuliza swali hapa Bungeni 2015 mwezi wa Nne, niliuliza swali hapa nikitaka majibu ya Serikali kuhusu suala la buffer zone ndani ya pori tengevu la Kilombero.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya Serikali walisema Serikali tayari kupitia Waziri Mkuu, wakati huo Mheshimiwa Mizengo Pinda alitoa agizo kwamba Wizara hizi tatu,Wizara ya Maliasili,Wizara ya Mazingira, Wizara ya Ardhi na TAMISEMI pamoja na Ofisi ya Mkoa Morogoro, wakae pamoja na walisema tayari wameshakaa na wataalam wameshapendekeza na taarifa njema kwamba tayari hata tafiti za TAWIRI zimeelekeza maeneo yale ya buffer zone maeneo mengi siyo rafiki tena kwa wanyama wanatakiwa wayarudishe kwa matumizi ya binadamu, matumizi ya wananchi kwa ajili ya kilimo na mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ilikuwa 2015 mwezi wa Nne, wamesema tayari wataalam wameshakaa wamependekeza. Namwomba Mheshimiwa Waziri Profesa, leo atakapohitimisha hapa, wananchi wa Malinyi, wananchi wa Ulanga wanataka wasikie nini hatima ya hii buffer zone.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake wanaishi kule kwenye buffer zone kila siku wanawasumbua, hiyo mifugo kila siku wanawapiga faini, wengine wamefika hatua mpaka wamekata tamaa, wakienda Lindi wanafukuzwa, wakienda maeneo mengine wanafukuzwa, hawa Watanzania wana haki ndani ya Katiba na sheria zinawalinda, mpaka lini wataendelea kuwanyanyasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali ndiyo inayosema nawashauri tena, habari njema Sheria ile ile ya 2009 ya Wanyamapori, ukiangalia kifungu cha 21 imempa mamlaka Waziri, wakati huo kabla hawajafanya maamuzi yao, lakini eneo lile la buffer zone Waziri ana mamlaka ya kutoa matumizi ya eneo lile. Sasa namwomba Profesa leo anapohitimisha atuambie kwa kutumia mamlaka aliyokuwa nayo, ni lini sasa hiyo buffer zone ndani ya pori tengefu la Kilombero inarejeshwa kwa wananchi kwa ajili ya maendelezo ya kilimo na mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo naona nisichanganye mada, nataka nimalizie hapo lakini naomba unipe nafasi wakati tunapopitisha bajeti hii nataka nishike shilingi ya kaka yangu. Kama hatakuwa na kauli thabiti juu ya suala hili la kuondoa migogoro kati ya Pori Tengefu la Kilombero na wananchi wanaoishi vijiji jirani na pori hilo, basi nitakuwa tayari ndugu yangu hata kama hatutaelewana siku nyingine leo nitatoa shilingi yake na naomba nitendewe hiyo haki, nataka nikamate mshahara wa Waziri leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.