Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Dr. Pudenciana Wilfred Kikwembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia katika hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kuwashukuru waandaaji, maana yake kuandaa hizi taarifa nayo ni shughuli. Kwa hiyo, wameweza kutuandalia vitu ambavyo na sisi tumeweza kuviperuzi na sasa tunaweza tukatoa michango yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Kavuu kwa uvumilivu wao na ushirikiano wao wanaonipatia mimi Mbunge wao wa Jimbo la Kavuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea na hotuba, naomba niwaombe wafugaji wangu wa Kata ya Ikuba, Kijiji cha Kikulwe na Ikulwe (Maji Moto), wawe na uvumilivu wa kuhamisha mifugo yao vizuri pindi watakapooneshwa maeneo ya kupeleka mifugo hiyo. Niiombe Serikali kupitia tangazo lake la kuwaambia watoke mita 500 kwenye vyanzo vya maji, niliomba kuchangia katika Wizara ya Kilimo na Mifugo, nikawaambia waende wakatengeneze malambo, ni ahadi ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakatengeneze malambo kule ili wafugaji wale wa Kata ya Ikuba wasiweze kwenda kwenye ule mto wanaowaambia waondoke mita 500 na wanawafukuza bila kuwapa mbadala wa maeneo ya kwenda. Wizara na Serikali wanasema wametenga maeneo Katavi, sasa wanawaondoa hawajawapeleka kule, leo wakikataa kutoka kule watasema wanaleta vurugu, hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hawatawaonesha maeneo ya kwenda kuweka mifugo yao maana yake ni nini? Sasa hivi wakulima wanavuna, maana yake watatoka pale walipo wanaenda kuongeza shughuli na vita nyingine na wakulima. Wamenitatulia tatizo lile lakini sasa wameongeza tatizo lingine jana. Leo hii ninavyoongea hapa wakulima na wafugaji kule ni shughuli kubwa, ni vita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Profesa Maghembe akitoka hapo saa saba kapige simu kule uwaeleze waache vurugu zile. Mkuu wa Mkoa na Serikali ya Mkoa imetoa tamko kule kuwa-disturb wafugaji lakini wakulima hawajatoa mazao yao shambani, kwa hiyo leo wanataka kuleta fujo juu ya fujo, jambo ambalo sitalikubali. Tumesema hapa, tunataka kutatua matatizo na si kuongeza matatizo. Haya ni matatizo ambayo yanatokana na mbuga ya Katavi pamoja na hiki kijiji ninachokisema Kata ya Ikuba pamoja na Kata ya Chamalendi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo mita 500 mkulima wa kawaida, mfugaji wa kawaida anazipimaje? Waende wakaweke alama, wakachimbe malambo waache kwenda kwenye ule mto, hakuna maji, kila siku hapa ni kilio na tunapiga kelele hapa Wabunge wote wanazungumzia tatizo hili la maji. Sasa kama hawana maji wakanyweshe wapi mifugo yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakiingia pale kunywesha askari wa TANAPA wanawaswaga wale ng‟ombe kuwapeleka ndani ya mbuga na kuwaua. Jambo ambalo wanawasababishia umaskini wafugaji na wakulima hawa na sisi lengo letu tunasema watu hawa waende kwenye uchumi wa kima cha kati. Tunafikaje kule kama leo sisi wenyewe tunakuwa ndani ya sheria zetu tunakinzana namna ya kuzitekeleza. Naomba waka-harmonize hizo sheria zao na waangalie ni namna gani wanatekeleza hayo majukumu na kwa wakati gani na kama eneo lile limetengwa wawapeleke wale wafugaji kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja katika suala lingine na naomba Mheshimiwa Waziri anielewe ni suala la utalii. Kwanza kabisa napenda nimpongeze Mheshimiwa Lucy Owenya jana amechangia vizuri sana kwenye suala zima la utalii, hakuwa bias na upande wao. Utalii imeonekana sasa ni Kaskazini tu, jamani kila siku nasema Mbuga ya Katavi ina wanyama wakubwa kuliko wanyama wote Tanzania. Anayebisha hapa leo aende lakini haitangazwi hata kidogo. Tuna twiga mazeruzeru kule, hakuna mbuga yoyote utawapata, tuna viboko wakubwa hakuna popote utawapata Tanzania nzima. Kwa nini hawatangazi mbuga zingine tumekazana tu na Serengeti, Ngorongoro, Manyara, sana sana tukisema tunakuja kusema hii hapa ya Iringa, kwa nini hatuvuki kwenye mbunga nyingine? Tunapoteza mapato kwa ajili tu ya utangazaji. Naomba hilo suala waliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye suala la wahanga katika Operesheni Tokomeza Ujangili. Katika Bunge lililopita Bunge lilitoa maazimio hapa mambo gani yakafanyiwe kazi, mojawapo ikiwa ni pamoja na kuwalipa wahanga ambao kwa namna moja au nyingine hawakuwa majangili bali walikuwa katika utekelezaji wao wa majukumu mbalimbali wakiwemo Watendaji wa Kata na Vijiji na baadhi ya Waheshimiwa Madiwani. Tuliwahi kusema hapa, wapo waliopigwa mpaka kupoteza viungo vyao na tulitoa maazimio wakasema watawalipa fidia. Nataka kujua fidia hiyo imekwenda wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri asiniambie ndiyo kwanza anaingia ofisini, ofisi ipo na shughuli ziko mezani, ukifika ni kuperuzi tu na kuendelea na utaratibu wa kazi. Kwa hiyo, tunaomba hili nalo alitolee ufafanuzi ili wahanga hawa ambao wengine waliweza hata kupoteza watoto wao bila sababu za msingi kutokana na kazi kufanyika bila kufanya utafiti wa kutosha. Kwa hiyo, watu wengi waliumizwa kwa namna moja ama nyingine na tulitoa maamuzi hapa na maazimio kwamba wapatiwe fidia. Kwa hiyo, tunaomba wale wote walioingia katika zoezi hilo bila wao wenyewe kuwa majangili wapatiwe fidia zao na Serikali itupe hapa majibu kwamba wanafanyaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye suala langu la Ikuba na Chamalendi, tafadhali sana Mheshimiwa Waziri mpaka saa nane mchana naomba awe amekwishaongea na Serikali ya Mkoa waangalie wale wafugaji wanawapeleka wapi. Sitaki niende kule nikute watu wamechapwa fimbo, watu wameuawa na kwetu kule unajua wakianza kupigana, ni mapanga na fimbo, hatutaki tusababishe vita kati ya wakulima na wafugaji. Tumeoana na tumeingiliana katika familia, hatutaki sasa tuanze kuwa na demarcation kati ya mkulima na mfugaji. Sisi wote ni wamoja, tuna namna tunavyoishi kule, mkianza kuleta vurugu zile mkulima hatakubali mwingine aingize ng‟ombe mle wala mwenye ng‟ombe hatakubali ng‟ombe wake wauawe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachelea kusema majipu yapo ndani ya TANAPA, maaskari wale wa mbugani wana mipango fulani. Haiwezekani askari anaajiriwa ndani ya mwezi mmoja ni milionea, ndani ya miezi miwili siyo mwenzio, lazima kuna namna inayofanyika kule, naomba wafanye utafiti. Haiwezekani hata kidogo mtu mmoja kapigiwa ng‟ombe 80, ng‟ombe 70, ng‟ombe 200 kwa kosa lipi? Sheria haisemi hivyo, sheria inasema hata kama wale ng‟ombe wamewakamata basi walipishwe faini. Kama faini zao wanaona ndogo walete sheria hapa tufanye marekebisho, tuone tunafanya nini kupata mapato na kuongeza uchumi katika Halmashauri zetu lakini kuwaonea wafugaji, kuwaonea wakulima kwa kweli ni kosa la jinai.