Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hoja hii nyeti na muhimu sana kwa mustakabali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Profesa Maghembe na Naibu Waziri, Mheshimiwa Injinia Ramo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuiongoza Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mdau mkubwa na naamini kwamba maendeleo ya watu na utunzaji wa mazingira ni vitu viwili ambavyo vinaendana (environmental conservation can co-exist with social economic development). Kwa hali inayoendelea katika Pori la Hifadhi la Kimisi nimeanza kuwa na mashaka kwamba tusipojipanga vizuri kama nchi itafika mahali nchi yetu itageuka kuwa jangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nikiwa mtoto Pori la Akiba la Kimisi tulikuwa tuna wanyamapori wengi, kulikuwa kuna twiga, zebra, tembo na wanyama wengi lakini sasa hivi limejaa ng‟ombe kutoka nchi za jirani. Nimeangalia kwenye sheria za nchi yetu, nimeangalia kwenye Mpango wa Taifa wa Ardhi wa 2013 - 2033 sijaona sehemu yoyote inayosema kwamba mapori ya akiba yatumiwe na ndugu zetu wa nchi za jirani kufuga ng‟ombe wao na wakati wananchi wetu wana shida ya malisho bora na maeneo ya kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa upande wa Karagwe, Kata ya Rugu, Nyakasimbi, Nyakakika, Nyakabanga na Bweranyange wananchi wangu wana shida sana na maeneo ya malisho bora na maeneo ya kulima lakini wanapakana na Pori la Akiba la Kimisi ambalo inasemekana kuna ng‟ombe wengi sana kutoka nchi za jirani. Naiomba Serikali iliangalie suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama kiongozi siwezi kuingia mle kwenye pori hata wananchi wangu wanashindwa kuingia na kwa kuwa wananchi wanafahamu kwamba haya mapori matumizi yake hayafuati sheria za nchi za mapori ya akiba, wengine wanashawishika kuingia mle kwa sababu hawako tayari kuona ng‟ombe wao wanakufa kwa kukosa malisho na wakati kuna wafugaji kutoka nchi jirani wapo kwenye lile pori. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali iandae Tume iende mle ichunguze status ya Kimisi irudi kwenye Pori la Akiba. Mimi na Madiwani wangu tutafuata utaratibu pale itakapobidi kama ni kuomba Serikali itenge maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji basi tufuate utaratibu wa bottom up kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. Watu wanatoka nchi jirani wanakuja kufugia kwenye mapori ya akiba na hiki ndiyo chanzo cha migogoro. Nazungumzia kwa Kimisi, lakini naamini pengine picha ya Kimisi inafanana na mapori ya akiba mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali baada ya ku-clear Kimisi ikawa katika hali ambayo inafuata utawala wa sheria, turudi kule zamani ambapo lile pori la akiba lilikuwa ni pori ambalo tunaweza tukafanya utalii. Wenzetu nchi ya jirani ya Rwanda wana ardhi chache lakini wanaitumia vizuri. Kwa mfano, pale Kimisi natamani sana Serikali ituletee twiga, zebra na tembo pawe conserved tuweze kufanya utalili kama majirani zetu Rwanda wanavyofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili niombe Serikali kwa sababu wakati wa kutenga Kimisi Serikali haikuhusisha vijiji vya jirani kunyoosha mipaka iende pale Kimisi katika hizi kata ambazo nimezitaja tuangalie upya ile mipaka na tuweke mipaka ya kudumu. Mimi kama Mbunge wa Karagwe naamini kabisa kwamba wananchi wa Karagwe tunaweza tukawa tuna conservation ya pori ambalo linatuletea mapato ya kitalii na wakati huo huo tukapata malisho bora na sehemu za kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuiomba Serikali, sasa haya ni mambo ya Kitaifa kidogo, kuna asilimia 25 ya mapato kutoka mapori ya akiba yanatakiwa kwenda kwenye Halmashauri kusaidia vijiji ambavyo vipo jirani na mapori ya akiba, lakini kwenye Halmashauri ya Karagwe hii hela hatujawahi kuiona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Waziri Mheshimiwa Profesa Maghembe atakaposimama kujibu hoja nisikie msimamo wa Serikali kwenye Kimisi na pia nisikie msimamo wa Serikali kuhusu asilimia 25 ambayo inatakiwa kuja kwenye Halmashauri ya Karagwe kutoka kwenye mapato ambayo yamepatikana kutoka kwenye mapori ya akiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la utalii kwenye nchi yetu umekuwa ni wimbo sasa tunasema nchi yetu ina-potential ya utalii inaweza ikatuingizia fedha za kigeni zaidi lakini sioni mikakati ambayo inanipa matumaini kwamba sasa sekta ya utalii itakua na kuweza kuchangia pato la Taifa. Napenda kuishauri Serikali, Wizara ya Maliasili na Utalii wasifanye kazi kwenye silos, washirikiane na Wizara nyingine kwa mfano kama kuna maeneo ambayo ni ya kipaumbele kwenye uwekezaji wa utalii, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ishirikiane na Wizara ya Maliasili kuhakikisha hayo maeneo yanapata miundombinu ili tuweze kuvutia uwekezaji kwenye maeneo hayo ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania kwenye ranking imekuwa nchi ya 130 na wakati kwenye vivutio duniani ni ya pili. Hii inaonesha kwamba hatujajipanga na tukijipanga sekta ya utalii inaweza ikatusaidia kukuza uchumi wa nchi na kutengeneza ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la mambo ya kale na hii ni sehemu ambayo tukijipanga vizuri inaweza ikatusaidia kuongeza pato na ajira kwa wananchi wetu. Karagwe kwenye historia na sisi tumo. Kama mnakumbuka Speke na Grant walipita Karagwe wakati wanaangalia jinsi ya kwenda Uganda. Kwa mfano sehemu ambapo Chifu Rumanyika alipokuwa anakaa tunaiomba Wizara ya Maliasili na Utalii itusaidie. Nimeshaongea na wana diaspora kutoka Karagwe wapo tayari kushirikiana lakini tunahitaji msaada wa Serikali kutuwekea miundombinu ya pale na tukae tuangalie ni namna gani tunaweza tukasaidia kuhifadhi malikale kwa Karagwe na sehemu nyingine za nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto kidogo kwenye Kata ya Bweranyange, hizi ni Wilaya ambazo ziko mipakani na nchi za jirani na ni vizuri tukahakikisha tunatunza ulinzi na usalama wa mipaka yetu. Kule kwenye Kata ya Bweranyange kuna kambi ndogo ya jeshi wananchi wangu wananipigia simu wanalalamika kwamba wamefika mahali wanaogopa kuoa wanawake wazuri kwa sababu wanahofia eti watanyang‟anywa na wanajeshi. Mimi siamini kwamba hali iko hivi lakini…
MWENYEKITI: Ahsante sana.