Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Mchango wangu wa kwanza utajikita katika suala zima la misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeendelea kushuhudia misitu yetu ikizidi kutoweka kwa kasi kubwa sana na hatujaona mikakati ya dhati ya Serikali kuhakikisha kunakuwa na misitu endelevu. Kuna takwimu ambazo zinaonesha national annual deforestation ni kati ya 0.8% mpaka 1.1%. Kwa kiwango kikubwa misitu hii inatoweka kwa shughuli mbalimbali ikiwemo shughuli za kilimo, uvunaji wa miti, moto na pia biashara kubwa ya mkaa. Ni vizuri Serikali ikatambua misitu hii leo tunaipoteza miaka 20, 30 ijayo nchi hii inaenda kuwa jangwa na hatujaona mkakati wa dhati kabisa wa Serikali kuhakikisha tunakuwa na misitu endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba tuna hiyo TFS ambapo jukumu lake kubwa ni kuhakikisha inasimamia na kutunza hiyo misitu ya asili. Hata hivyo, hii TFS imejikita katika kukusanya mapato zaidi bila kuwa na mipango endelevu ya misitu hii. Mheshimiwa Mbunge mmoja jana alichangia hapa akahoji hata mapato yenyewe yanakusanywaje na haya mapato yanayokusanywa kweli yana uhalisia? Ukichukua mfano, kuna tafiti zimefanywa, kwa Mkoa wa Tabora peke yake kwa mwaka wanazalisha magunia ya mkaa 2,244,050 wanapata shilingi bilioni karibu 21 kwa mwaka kwa shughuli za mkaa peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma taarifa za TFS wao wanasema makusanyo ya mkaa tu kwa mwaka ni shilingi bilioni saba, lakini Mkoa tu wa Tabora ni bilioni 21, kitaifa wanasema ni shilingi bilioni saba. Kwa hiyo, nadhani Mheshimiwa Waziri anapaswa ku-deal na hawa watu wa TFS, kuna tatizo hapa. Kuna watafiti wamefanya utafiti wanaonesha hizi takwimu mkoa mmoja wanaingiza fedha nyingi, lakini Kitaifa TFS wanasema ni shilingi bilioni saba tu. Wizara inatakiwa kuhakikisha wanaitazama vizuri hiyo TFS kwa sababu wao nadhani ama ni rushwa ama kuna watendaji ambao si sahihi wanakwamisha shughuli hizi za kukusanya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niishauri Serikali kwamba pia wasiitazame TFS katika kuhakikisha inawaletea mapato tu au kutoa vibali vya misitu na vitu kama hivyo. Ni muhimu TFS ikatekeleza majukumu yake kama dhamira ya uanzishwaji wa TFS ilivyokuwa katika taratibu zake za uanzishwaji. Ni muhimu sana Serikali mkatazama hawa TFS wanapotoa leseni, watoe leseni lakini hao wanaopewa leseni walete mpango mbadala au mkakati mbadala wa kuendeleza misitu yetu ili tuweze kuondokana na kutoweka kwa misitu kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la migogoro ya mifugo inayoingia hifadhini. Waheshimiwa Wabunge sisi kama viongozi pia wakati mwingine ni lazima tuangalie kauli zetu zisije zikalibomoa Taifa. Ni kweli kwamba tunawahitaji wafugaji, ni kweli tunawahitaji wakulima, ni kweli kwamba tunahitaji hifadhi au misitu. Ni muhimu tukafahamu kuwa mifugo inaongezeka na mahitaji ya kilimo kwa maana ya wakulima wanaendelea kuhitaji ardhi lakini ardhi ni ile ile tu haiongezeki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sana Serikali wakakaa na Wizara zote ambazo zinaingiliana katika masuala haya ya mifugo, kilimo na wa maliasili kuhakikisha wanaweka mipango madhubuti ya kuhakikisha wafugaji wanapata maeneo yao, wanatengewa kabisa, hifadhi nayo inakuwa na maeneo yasiingiliwe na wafugaji, vivyo hivyo kwa wakulima pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kusema pia wakati mwingine unaruhusu moja kwa moja mifugo inaingia hifadhini lakini kama hawa watu wangetengewa maeneo yao hakika tusingekuwa na hii migogoro ambayo inaendelea. Serikali lazima ipime, ukipima kati ya suala la maliasili na utalii na kati ya sekta ya mifugo utaona kwa takwimu kwa sasa kwamba maliasili inaiingizia Serikali pato zaidi kuliko mifugo. Inawezekana pia mifugo ingeweza kuliingizia Taifa pato zaidi kuliko maliasili lakini kama wangekuwa na ufugaji wa kisasa, wakapangiwa maeneo yao, wasiingiliane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu sana Serikali wakayapima haya, wakahakikisha migogoro hii ya wakulima na wafugaji inakwisha. Niwasihi Waheshimiwa viongozi wenzangu Wabunge, ni muhimu sana tukachunga kauli zetu, tuangalie tunawahitaji watu wote. Tunawahitaji wakulima, tunawahitaji wafugaji, tunahitaji pia na misitu yetu na uhifadhi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la utalii. Wizara imetoa takwimu hapa kwamba kwa mwaka nchi yetu inaingiza watalii karibu 1,200,000 na kuna Mheshimiwa Mbunge wa Arusha jana alichangia vizuri sana akafanya comparison na nchi nyingine ambazo zinakuwa na idadi kubwa ya watalii. Nchi yetu mtalii kuja hapa anakumbana na tozo kibao. Anaanzia kwanza kwenye viza, akienda kama ni Ngorongoro getini kuna fees, akilala kwenye hoteli kitanda kina fees, kila mahali Mzungu huyu au mtani huyu anatozwa tozo na hizi tozo zimekuwa ni fixed mwaka mzima na watalii ni wale wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niishauri Serikali kwa nini msiwe na promotion package kwa kipindi fulani ili muongeze idadi ya watalii halafu baadaye mkifika kwenye pick fulani mtaendelea na hizi tozo zenu ambazo ziko fixed ili tuhakikishe tunaongeza idadi ya watalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni muhimu sana pia wakahakikisha wanakuza utalii wa ndani. Kuna baadhi ya maeneo, mimi natoka Wilaya ya Karatu, Wilaya ya Karatu ina hoteli za kitalii 54, wako Watanzania ambao hawajui. Mtanzania yuko Dar es Salaam anafikiria kwenda kupumzika South Africa lakini kumbe angekuja kupumzika Karatu kuna hoteli nzuri, zile ambazo wanazifuata nje ya nchi pia ziko pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti,una hoteli nzuri sana ambazo wageni wengi wanapenda kulala pale halafu wanakwenda kutembea Ngorongoro. Wilaya kama hizi ambazo ziko pembezoni mwa Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ni sehemu ya lango la kuingilia Ngorongoro tayari kuna hizi hoteli za wawekezaji na wazawa pia wamejitahidi kujenga hoteli za standard mbalimbali, unakuta kuna hoteli ya mpaka kulala siku moja ni karibu dola 700, hoteli yenye standard na quality ya juu kuliko labda hizo mnazofuata South Africa na kwingine, ziko Karatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu pia Wizara wakaangalia Wilaya kama hizi ambazo tayari kuna hoteli kama hizi wakazitangaza, wakafanya utalii wa ndani pia wakawa na target ya kukuza utalii wa ndani na si tu kuangalia target ya kukuza utalii wa wageni kutoka nje. Kwa hiyo, ni muhimu sana wakalitazama hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu TANAPA. TANAPA ina jukumu la msingi la kusimamia hifadhi za Taifa, uhifadhi wa wanyamapori na shughuli za utalii. Leo TANAPA mapato yake yote yanapelekwa kwenya pool moja kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, lakini hawa baadaye wakitaka kutekeleza shughuli zao maana yake waje tena waombe huko, kwa maana ya Hazina au Mfuko Mkuu wa Serikali waweze kwenda kutekeleza majukumu yale. Mfano, leo pale Ziwa Manyara liko chini ya hifadhi ya TANAPA linapotea kwa sababu limejaa tope hakuna kinachofanyika. TANAPA wanakusanya fedha badala nyingine zirudi kwenda kutekeleza zile shughuli zinapelekwa Mfuko Mkuu wa Hazina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wanaipa TANAPA kazi ya kutengeneza madawati nchi nzima halafu Waheshimiwa Wabunge wanapongeza wakati TANAPA ina kazi ya kudhibiti ujangili, ina kazi ya kudhibiti na kuhakikisha kunakuwa na uhifadhi endelevu, ina kazi ya kuhakikisha mfano Ziwa Manyara linaendelea kuwepo? Mheshimiwa Waziri baada ya miaka 10 au 20 Ziwa Manyara linapotea kwa sababu limejaa tope maji yale yanakuwepo tu msimu wa masika baada ya muda ni tope linajaa pale. Kwa hiyo, ni muhimu sana Wizara wakaangalia shughuli za TANAPA zisiweze kusimama. Haiwezekani wao wanakusanya fedha wanawapelekea halafu mwisho wa siku yale majukumu yao ambayo wanapaswa kuyafanya hawawezi kuyatekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.