Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ili nami niweze kuchangia hii hotuba ya bajeti. Naomba kwanza nianze kwa kusema naiunga mkono hotuba hii kwa asilimia mia moja. Nianze pia kumpongeza Waziri wa Mipango, Mheshimiwa Philip Mpango, kwa bajeti yake nzuri, lakini pia na Serikali yote kwa ujumla inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa utendaji mzuri wa kazi pamoja na Mawaziri wote na watendaji wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na suala la muhimu katika uchumi wa nchi yoyote ambalo linatokana na afya. Napenda kuipongeza Wizara ya Afya, kwa takwimu ambazo zimeonekana humu katika kitabu zinazoonesha kwamba vifo vya mama na mtoto vimepungua kwa kiwango kikubwa, naipongeza sana Wizara ya Afya. Hata hivyo, kuna data imenishtua kidogo, data hii inahusiana na ongezeko la mimba au ujauzito usiotarajiwa kwa watoto wa miaka 19 na ambao wanafanana na hiyo kutoka asilimia 23 mwaka 2010 mpaka asilimia 27 mwaka 2015, hii data kwa kweli inatisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachelea kujua ni nini hasa tatizo, pengine ni elimu, lakini pengine kuna tatizo lingine. Sasa tusipoangalia, hata tunapojadili bajeti ambayo inahusiana na uchumi na hasa tunapokwenda kwenye uchumi wa kati ambao ndiyo matarajio yetu, kama kutaendelea kuwa na ujauzito usiotarajiwa kwa vijana wetu kwa kiwango kikubwa cha namna hii, basi hata ile nguvukazi yenyewe tunayoitarajia tutakuwa na mashaka nayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia labda nielekeze hili kwa Mheshimiwa Waziri wa Afya. Suala la elimu kwa ajili ya hawa vijana wetu ambao sasa wanaongezeka kupata mimba zisizotarajiwa, vijana wadogo. Pengine suala la elimu sasa limekuwa limefifia na hasa njia hizi za kujikinga na matatizo mbalimbali yakiwemo haya ya kupata mimba za utotoni pamoja na magonjwa mengine. Kulikuwa na kampeni mbalimbali miaka ya nyuma na nadhani sasa zinaendelea ila inaelekea zimepoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kupoa huko sasa watoto data zinaanza kupanda kupata ujauzito utotoni. Nitolee mfano, kwa mfano suala linaloongelewa zaidi na Wizara na watu mbalimbali ni kuwaambia watu namna ya kujikinga kwa kutumia njia mbadala,kwa mfano njia za uzazi wa mpango zinaongelewa sana. Nadhani tuna aibu kidogo, mimi sioni sana likiongelewa suala la watoto hawa ambao tayari wameshakuwa watu wazima, kutumia njia kwa mfano kama mipira ya kiume (condoms), watu wanaona ni aibu kuzungumza hili wakati nchi tunazojilinganisha nazo, nchi zilizoendelea kwa mfano kama Uingereza, Marekani na nyingine, hili ni suala la wazi kabisa huwa wanajadili, wanawaambia vijana wao kwamba njia mbadala ili muweze kujikinga na mimba za utotoni lazima mtumie vitu kama mipira.
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia hilo kwa sababu kuna wengine wanadhani hili suala la kuongelea masuala kama condom ni aibu fulani na hapa tunafanya makosa makubwa sana. Kuna watu wanatembea na silaha kwa ajili ya kujikinga, si kwamba wanategemea kwamba labda watakumbana na majambazi wakati huo, hapana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo hata watoto hawa ambao tayari ni watu wazima, wanapotembea na mipira kama hii kwa ajili ya kujikinga, si aibu. Nakumbuka kipindi fulani cha nyuma kuna Waheshimiwa Wabunge fulani walipokuwa wanasachiwa wakakutwa kwenye mabegi yao kuna condoms, watu wakasema hii ni aibu, mimi sioni kwamba ile ilkuwa ni aibu. Hawa wanaonekana kabisa wanajali na wako tayari kujikinga, ile ni silaha, ni anti-missile ya kupata ujauzito, ni anti-missile ya kupata magonjwa yasiyotarajiwa, kwa hiyo nadhani elimu ni kitu muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala hili ambalo ni la hivi karibuni kuhusu kuitoa kwenye halmashauri kodi ya majengo na kuipeleka kwenye Serikali Kuu. Hili suala, halmashauri zetu nyingi zinatumia kodi hii…
Mheshimiwa Naibu Spika, naona kengele kama imegonga mapema sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kodi hii ndiyo inategemewa na halmashauri nyingi saa hapa nchini, sasa kuifuta kuna halmashauri ambazo zitakufa kifo kinachoitwa natural death. Kuna halmashauri ambazo kipato chake kinategemea zaidi kodi hizi, naipongeza sana Serikali kwa kuondoa kodi nyingi za mazao ya kilimo, lakini kuna halmashauri ambazo hata kwa mwaka mzima haifikishi zaidi ya milioni 100, kwa mfano ile halmashauri ya Gairo, Morogoro. Ile halmashauri, nilikuwa kwenye Kamati ya LAAT, ile halmashauri ina kipato kidogo sana kwa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee pia hili suala la hizi kodi za simu. Nina mashaka, pamoja na kwamba Serikali inatuambia haitatuathiri watumiaji wa kawaida, wale wa makampuni ya simu ni wajanja, lazima kodi zile zita-back-fire kwa mtumiaji wa kawaida, atakuja kuathirika na kodi zile.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hizi kodi pia za usajili wa magari na usajili wa pikipiki, imepandishwa kutoka 150,000/= mpaka 250,000/= kodi ya magari, hii itasababisha watu wengine kuanza kukwepa suala la ku-transfer gari, watu wengi watatumia majina ya wenzao. Hiki kitu kitawakosesha Serikali mapato, bora utoze kidogo lakini uwe na uhakika wa kupata kodi ile kuliko kuikosa kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kupanda kwa hii kodi ya pikipiki kutoka 45,000/= mpaka 95,000/= ni kodi kubwa mno. Kodi hii itatufanya tuweke uadui ambao si wa lazima kati ya wamiliki wa pikipiki (bodaboda) ambao walitetewa na Bunge hili. Miaka iliyopita, bodaboda hawa ndiyo walitetewa kuhusu kodi, wakatetewa zikaja pikipiki nyingi nchi hii, sasa leo wanapandishiwa kodi kwa zaidi ya asilimia 100, sijui tunawaweka katika hali gani. Inaweza ikapelekea hawa wasiwe na imani na Serikali yao; naomba kodi za namna hii ziangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni hili suala la maagizo elekezi kutoka Wizara ya Ardhi. Kuna maagizo elekezi kutoka Wizara ya Ardhi kuhusu kusimamisha kwa muda usiojulikana uuzwaji wa viwanja…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja.