Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Korogwe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARY P.CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwa kuunga mkono hotuba ya Waziri wa Fedha. Nipongeze jitihada za Serikali katika ukusanyaji wa mapato, lakini bado tuna safari ndefu ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wetu juu ya kudai risiti pale wanapokuwa wamenunua bidhaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niendelee kuishauri Serikali kwamba ni wakati muafaka sasa katika jambo hili la ukusanyaji wa mapato au kutoa elimu, tuanze kutoa kwa shule zetu za msingi na sekondari ili watoto wetu waweze kufahamu mapema juu ya suala la ulipaji wa kodi na kudai risiti pale wanaponunua bidhaa kwenye maduka.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali ya hiyo Serikali imefanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato, lakini bado kuna ukwepaji wa kodi kwa baadhi ya vituo vya mafuta. Viko vituo vya mafuta ambavyo vyenyewe vinatumia ile mashine, ukienda kununua mafuta unapomdai risiti anakwambia mashine nimeipelekea kwenye chaji, unamwambia sasa inakuwaje umeshaniwekea mafuta, anakwambia sasa nifanyaje nimeipeleka kwenye chaji.
Kwa hiyo, pale hupati risiti kwa sababu ameshakwambia amepeleka kwenye chaji. Sasa niombe Serikali tuendelee kuwasimamia hawa wafanyabiashara wazifunge zile mashine kwenye zile mashine zinazotoa mafuta ili anapotoa mafuta na risiti inajitoa badala ya hizi mashine ambazo wanasema zinakwenda kuchajiwa huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoteza mapato kwenye vituo vya mafuta kwa ujanjaujanja huo, kwamba wanapeleka kuchaji zile mashine.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la TRA kukusanya mapato. Nakubaliana na jambo hilo lakini sasa tunaliwekaje kwa sababu Halmashauri zetu katika bajeti zao hususani Halmashauri yangu ya Korogwe ni sehemu ya own source ya mapato yao ya ndani kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika Halmashauri. Sasa endapo TRA itakusanya mtatuwekea utaratibu gani wa kurejesha zile pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, bado nina uzoefu wa huko nyuma, viko vyanzo ambavyo Serikali ilivizuia kwamba Halmashauri isikusanye kwamba Serikali kuu itafidia, lakini bado kumekuwa na usumbufu na ucheleweshaji wa fedha hizo kurejeshwa kwenye Halmashauri baada ya kuwakataza kwamba wasikusanye yale mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri aniambie baada ya kuwa TRA imekusanya fedha hizi na hasa ikizingatiwa kwamba ndiyo chanzo cha mapato katika Halmashauri zetu, watakuwa wanarejesha kwa wakati ili hizi fedha zikafanye kazi za maendeleo katika Halmashauri zetu? Nitamwomba Waziri aniambie atakapokuwa anafanya majumuisho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo mengi ambayo yanapoteza mapato, tukikusanya vizuri hata upande huu wa madini tukiangalia vizuri hii mikataba ndugu zangu inaweza ikatusaidia kupata mapato ya kutosha tukaachana na hili suala hata la kutaka kukata kodi kwenye kiinua mgongo cha Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kukata kodi kwenye viinua mgongo hatukatwi Wabunge tu, nimeona kumbe wanakatwa mpaka Watumishi wa Serikali. Watumishi hawa wa Serikali na sisi Wabunge tunakatwa tayari kwenye mishahara yetu, sasa inakuwaje tena tunaendelea kukatwa kwenye kiinua mgongo? Niiombe Serikali iliangalie jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye Mfuko wa Maji na naungana na Kamati ya Bunge ambayo ilitoa taarifa yake kwamba iongezwe tena angalau Sh. 50/= kusudi iwe Sh. 100/=, ikiwa Sh. 100/= maana yake itatusaidia kwenye Mfuko wa Maji, lakini wakati huo huo zikajengwe zahanati na vituo vya afya. Wanawake wajawazito na watoto wanapata shida, endapo hatutajenga zahanati, endapo hatutakamilisha zahanati zilizokuwa zimejengwa na vituo vya afya, wanawake wataendelea kupata shida kwenda mwendo mrefu kwa ajili ya kwenda kujifungua na kwa ajili ya kuwapelekea watoto kupata matibabu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe Serikali yangu ikubaliane na suala la kuongeza Sh. 50/= ili iwe sh. 100/= na hatimaye fedha zile zigawanye ziende kujenga vituo vya afya pamoja na zahanati. Ukiangalia pale kwangu Korogwe Mjini sina hospitali ya Wilaya, nina zahanati pale ya Majengo, nakusudia sasa ile zahanati iwe ndiyo kituo cha afya ambacho kitakuwa kama sehemu ya Hospitali. Sasa kama hakijatengewa fedha hawa wananchi wangu wa Korogwe wanatibiwa wapi? Niombe Serikali tukubaliane kwa hili ambalo limependekezwa na Kamati ili kusudi fedha hizi ziweze kusaidia kujenga zahanati pamoja na vituo vya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge, nakubaliana na naunga mkono kwa asilimia mia, lakini hebu tuitazame na reli ya Tanga, kwa sababu sasa hivi tunasema litajengwa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga. Hebu tuiangalie na reli ya Tanga kuweza kuipa fedha ili kusudi iweze kujengwa kwa kiwango cha standard gauge.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yangu kwamba Waziri naye ataliangalia hili kwa sababu tumekubaliana bomba hili linaanza kujengwa hivi karibuni, ni kwa nini sasa Tanga haijatengewa fedha kwa ajili ya kujenga reli kwa kiwango cha standard gauge? Wamesema hili bomba kwa taarifa nilizonazo litakuwa linapita kando kando mwa reli mle, niombe sana Serikali yangu iliangalie hilo kuona kwamba ni namna gani ambavyo inaweza ikajenga reli ya Tanga kwa kiwango cha standard gauge.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja na kushukuru sana kwa kunipa nafasi.