Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyenijalia kupata uzima siku hii ya leo, nikushukuru pia wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Bajeti Kuu ya Serikali 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza na suala la ujenzi wa zahanati, vituo vya afya pamoja na hospitali ni jambo ambalo lilikuwa limelenga kabisa maendeleo yetu ili yaweze kufanikiwa ni lazima kwanza wananchi wetu wawe na afya bora na hapo ndipo tutakapoweza kufikia uchumi wa kati, lakini pia katika kufanikisha malengo ya milenia kufikia uchumi huu wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niiulize Serikali leo ni lini itakamilisha ujenzi wa vituo vya afya, zahanati pamoja na hospitali za Wilaya ili tuweze kufikia sasa uchumi huu wa kati, kwa sababu tusipokuwa na afya njema ni wazi kabisa Taifa litakuwa na wananchi ambao ni goigoi, watashindwa kufanya kazi vizuri ili kuweza kufikia uchumi huu. Hivyo, Serikali iniambie lini ujenzi huu utakamilishwa katika vituo vile vya afya, zahanati pamoja na hospitali za Wilaya ambazo hazijawa tayari kwa maana ya kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuainisha hizo zahanati ambazo zipo katika Wilaya ya Mbinga, Mbinga Mjini kuna zahanati karibu 15 ambazo zinahitaji kumaliziwa, lakini pia Mbinga Vijijini kuna vituo vya afya na zahanati ikiwemo katika Kata ya Kilimani kuna zahanati, Lipilipili, Luwahita, Luhaga, Mikatani na Kihuka. Pia katika Wilaya ya Nyasa pana shida kubwa sana kwa maana ya hospitali ya Wilaya imeanza na haijakamilika, ni lini Serikali itakamilisha ili tuweze kupata wananchi ambao watakuwa na afya bora tuweze kufikia malengo ya milenia.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya hiyo hiyo ya Nyasa kuna zahanati ya Chiwanda, Ngindo, Liweta, Mpotopoto, naomba pia nazo zitiliwe uzito zitengewe pesa kwa ajili ya kukamilisha. Tunduru pia kwenye eneo hili kuna wodi ya wanaume katika hospitali ya Wilaya ya Tunduru, watoto wa kiume wanaenda kulala kwenye wodi ya akina mama, hii ni hatari sana kiafya lakini pia hata kimaadili. Wodi ya wanaume kule Tunduru inatakiwa imaliziwe, lakini pia kuna wodi ya wanawake nayo pia imaliziwe katika Wilaya ya Tunduru nikienda sambamba na zahanati za Masonya, Sisi kwa Sisi, Cheleweni, Njenga na Fundimbanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Madaba pia naomba mfahamu mchango mzuri wa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Madaba na jitihada ambazo anaendelea kuzifanya ili kuhakikisha kwamba, Jimbo la Madaba litakuwa na hospitali ya Wilaya lakini pia na vituo vya afya pamoja na zahanati ili nao pia waingia katika malengo ya milenia. Hali kadhalika na katika Wilaya ya Namtumbo zahanati na vituo vya afya ni muhimu. Zahanati na vituo vya afya vikikamilika ni wazi kabisa tutakuwa tuko vizuri na afya zitaboresheka na hata hivyo tutafikia hizo asilimia saba za uchumi wa Tanzania ambao tunautarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kuondoa tozo zisizokuwa na tija kwenye mazao ya korosho, kahawa na tumbaku, naipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma bajeti hii na maelezo ya Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii kwa maana ya bajeti ya Serikali maelezo ni matamu na hata uchambuzi wake ni mzuri mno. Hii inaonyesha wazi ni namna gani Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba inakuza uchumi wa ndani kwa kukusanya mapato pia inafikia hatua ambayo Serikali sasa itaacha kuwa tegemezi na itaenda kujitegemea yenyewe. Naipongeza sana Wizara hii kwa kujipanga vizuri kwenye eneo hili. Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake mko vizuri pamoja na delegation yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia kwenye eneo hili iangalie sekta zile ambazo zimekuwa zikitoa mchango mkubwa sana kwa maana ya kuingiza mapato mengi katika nchi yetu ikiwemo sekta ya utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sekta ya utalii kumekuwa na jambo moja ambalo lilikuwa kama vile wenzetu ambao walikaa kwa maana ya mahusiano haya ya East Africa wakakaa kwa pamoja Mawaziri wa Fedha wakiwa na lile jambo ambalo kwa mfano, labda wanasema kwamba, kuna chakula cha mgeni na chakula cha wote. Kilichofanyika hapa ni kama hivi changa la macho.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wa Kenya mara ya kwanza walikuwa wameingia kwenye suala la kutoza VAT kwa watalii wanaoelekea Kenya. Baada ya hapo wakaona kwamba ile VAT haitawasaidia na kwamba imeshusha sana kiasi cha mapato yanayopatikana katika utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 Mawaziri hawa walipokaa walikubaliana vizuri kilichojitokeza ni kwamba, mwaka 2015 Kenya ilipata watalii 3,000,000 na waliingiza dola za Kimarekani bilioni 1.5. Tanzania iliingiza watalii milioni 1,100,000 ilipata dola za Kimarekani bilioni 2.5. Sababu kuu ilikuwa ni kwamba Tanzania ililenga kuwa na watalii wakubwa tu ambao wana uwezo wa kulipia hoteli, lakini Kenya walikuwa wamelenga wapate watalii wadogo wadogo pamoja na kutoza kodi kwa hiyo mapato yao yalishuka. Baada ya kugundua hilo sasa wamerudi na habari nyingine wakasema kwamba, wao ni vizuri wakaondoa kodi kwa hiyo, tumebaki sisi ambao kimsingi tumeenda kujiingiza kitanzi wenyewe, tunaenda kujikaba wenyewe ili tujinyonge na hatimaye tushindwe kuongeza mapato kwenye eneo hili la utalii. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge wenzangu, niwaombe sana kwenye jambo hili tushirikiane, tufike mahali tukubaliane kama wamoja tuondoe VAT kwenye eneo hili la utalii ili utalii uendelee kuingizia mapato Serikali, kinyume na hivyo maana yake tutakosa hizi dola za Kimarekani bilioni mbili na point zake, badala yake wenzetu Kenya wanaenda kufanikiwa sisi tunabaki tuko tunabembea tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Wabunge kama nilivyosema nisingependa kurudia pia nitakuwa sijatenda haki endapo kama sitaongelea kodi ya Wabunge. Kwenye suala hili kwa kweli mmegusa pabaya, panaumiza kweli kweli ukizingatia kwamba Mbunge hata sasa mshahara wake bado anatozwa kodi kila mwezi Mbunge anakatwa shilingi milioni moja na laki tatu na kadhalika mpaka itakapofika miaka mitano maana yake kunakaribia milioni 50 ambayo Mbunge anakatwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niwaambieni mimi kama Mbunge toka asubuhi mpaka sasa hivi hapa niliposimama nina simu 30 zinatoka kwenye Jimbo langu la Mkoa wa Ruvuma, wananchi wana mahitaji mbalimbali na ukizingatia kwamba Wabunge wa Viti Maalum hatuna Mfuko wa Jimbo, tunafanyaje kwa kile tunachokipata? Kile tunachokipata kidogo ndiyo kinaenda kusaidia hata ukaenda kufanya hili, ukafanya lile na hata kuwezesha vikundi mbalimbali. Ninaomba Waziri atakapokuja tena, aje na maelezo mazuri kuhusu eneo hili ili tuweze kwenda sambamba, vinginevyo hatumuelewi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana naomba kuunga mkono hoja.