Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpendae
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SALIM HASSAN ABDULLAH TURKY: Mheshimiwa Naibu Spika, hamu imenishika, fahamu imeondoka! Nashukuru sana. Mimi nina-declare interest ni mfanyabiashara mwenye viwanda kwa hivyo ninachotaka kuzungumiza ni uchumi wetu wa viwanda. Kwa masikitiko makubwa sana nasimama kwa huzuni kwamba Rais wetu anataka nchi hii iwe ya viwanda lakini nafikiri watu wanaoshauri Wizara hawashauri vizuri, mfano hai wa kwanza ninaotoa ni huu.
Kuna kiwanda kinazalisha pasta (macaroni), tambi, kiwanda hiki kiliomba msamaha wa kodi kwa sababu raw material inayotumia ni unga wa semolina ambao katika East Africa yote haipatikani na walikubaliwa na Serikali wakajenga kiwanda, uzalishaji umeanza miezi miwili iliyopita. Na hapo hapo waliahidi kwamba wataweka na kiwanda cha pili cha kusaga ngano inayotengeneza semolina. Kiwanda hiki kimechelewa kutokana na sababu zisizoweza kuepukika, kwa hivyo wenye viwanda wakaandika barua kuomba kwamba wanaomba waongezewe muda wa semolina kupewa msamaha huo, kilichotokea kwa masikitiko makubwa, kiwanda cha pasta sasa hivi kinazalisha kontena tano kwa siku yaani tani 96 kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachojitokeza sasa hivi ni kwamba pasta tayari inazalishwa, kile kiwanda cha kutengeneza unga hakijawa tayari. Wameandika barua kuendeleza msamaha wa mwaka mmoja tena waongezewe, msamaha huo hawajapewa. Sasa matatizo yatakayojiyokeza kwenye kiwanda hiki ni kwamba semolina ndiyo inayotengeneza pasta (macaroni) maana yake mtu anayeagiza macaroni kutoka nje tayari anaweza akauza hicho kiwanda hakina kazi Tanzania, watu 156 wanakosa ajira hivi hivi! Kiwanda kile cha pili kinajengwa ili kusaidia kiwanda kile.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwekezaji wa dola milioni 40, Serikali hii kwa uongozi huu uliyopo ndani ya Bunge hili, Waziri wetu wa Fedha jambo hili halioni? Nimemwambia, katia pamba kwenye masikio, halafu tunakuja hapa kujadili viwanda, kweli tunaifanyia haki Tanzania hii? Ninaomba sana Waziri wa Fedha jambo hili ukija utujibu kama kiwanda hiki kifungwe, kwa sababu ulishaniambia Watanzania wanakula muhogo pasta hawali! Uwekezaji huu unakuja kuwalisha pasta watu wote. Hivyo ninaomba sana, dakika zangu tano bado zipo?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Suala lingine ninalotaka kuliongelea ni kwamba Serikali yeyote unapotaka kuja kuwekeza katika nchi ni lazima sheria zako mwenyewe unazojiwekea uziheshimu. Kuna sheria hapa inasema kwaba mtu yeyote anayetaka kuja kuwekeza Tanzania basi aweke kiwanda, kiwanda kitatoa msamaha kwa mtu yeyote ambaye ataleta raw material katika nchi, kwa hiyo, anapewa zero. Mtu ambaye ataleta semi-finished product atapewa asilimia kumi na mtu ambaye ataleta finished product atalipa asilimia 25 ya kodi katika nchi yetu hii.
Sasa kinachojitokeza wawekezaji wameiamini Serikali yao, wamekuja wamewekeza, unakuja unabadilisha unasema sasa raw material tutatoza asilimia kumi na hiki kiwanda ambacho kinatumika kutengenezea raw materials na semi finished products ni viwanda viwili tofauti, uwekezaji wake ni mkubwa mno. Huoni kama unaanza kudumaza maendeleo ya viwanda hivi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kauli yako mwenyewe unaanza kutia ulimi puani, kwa hivyo lazima tuheshimu maamuzi yetu. Serikali lazima iwe na kauli ya kuheshimu viwanda na kuendeleza viwanda. Kinachojitokeza sasa hivi mtu anakwambia kwamba mafuta yanayoletwa siyo mafuta ghafi, sasa tunataka Bunge hili watu waje wathibitishe kwamba toka tumeanza Bunge hili watu wangapi wamekamatwa hawajaleta mali ghafi wamedanganya Serikali hii tuletewe orodha yao hapa na wamepewa adhabu gani? Siyo tunakaa kwa kusema tu kwamba hapana, watu wanadangaya mafuta hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiki kinachofanyika sasa ni kifo kwa wananchi wetu wa Tanzania. Mfumuko wa bei sasa hivi kama tunavyojua sukari bei yake ilivyoelekea huko na mafuta haya kwa kodi hii leo nataka muandike kwa kalamu tarehe ya leo na bajeti hii itakapoanza kufanya kazi kwa kutoza asilimia kumi mfumuko wa bei ya mafuta ya kula Watanzania mtapiga kelele humu humu. Naomba sana Wabunge wote tushirikiane, kodi hii tusiikubali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba sitounga mkono hoja hii mpaka nipate majibu ya Waziri. Ahsante sana.