Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chemba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Pia nimshukuru sana Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kwa kunijalia afya njema siku ya leo ili na mimi niweze kuchangia katika hoja hii iliyo mbele yetu ya Bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nitakuwa ni mwizi wa fadhila nisipoungana na wenzangu kwenye jambo hili la kiinua mgongo cha Wabunge. Wengi wamesema sana, wametoa na mifano kwamba pengine Mheshimiwa Waziri kwa sababu hana jimbo, hajui adha za Wabunge na mimi nimuombe tu ili ajue taabu wanayopata Wabunge ajaribu mwaka unaokuja wa 2020 aone adha yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunazungumza bajeti ya 2016/2017, sijaona impact yoyote ya kuwa na haya makato ya Wabunge katika bajeti ya mwaka huu. Ukikaa ukijiuliza kwamba kwa nini ameileta sasa, ni swali ambalo bado linaleta ukakasi kupata majawabu yake. Ukipita mitaani kuna hearsay kwamba unajua ameagiza Mheshimiwa Rais, nadhani watu wamefika wakati wanashindwa kuweka mambo yao wanataka kumchonganisha Rais na watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amekuwa Mbunge kwa miaka 20 na anajua matatizo ya Wabunge. Kwa hiyo, kila kitu kusingizia kwamba ni Rais kaagiza naamini si kweli. Mheshimiwa Rais ni mtu makini sana, lakini sasa hivi kila anayetaka kufanya maamuzi ameagiza Rais nadhani tunakosea, tufanye kazi zetu kwa mujibu wa kazi tulizokabidhiwa. Namuomba Mheshimiwa Waziri, ni rafiki yangu alitazame vizuri sana hili, kazi hii ngumu baba, ondoa hicho kitu. Mimi nampenda ni rafiki yangu, amefanya kazi na marehemu kaka yangu, lakini kwenye hili hatuko pamoja. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili napenda kuzungumzia hili suala la VAT kwa utalii. Mimi nimeiona bajeti ya Kenya ambapo kwenye ukurasa wa 29, Waziri wa Kenya amefuta VAT. Hoja yake ya msingi Kenya wanasema baada ya kuweka VAT watalii wamepungua sana kwenda Kenya. Kwa hiyo, wameamua kuiondoa sasa ili ku-motivate watalii waingie na naamini mapato yao yataongezeka zaidi. Sasa kama ulikaa nao kama ulivyodokeza awali hiyo wamekutia changa la macho.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kidogo suala la ule Mfuko wa Maji na Mafuta, jambo hili umelizungumzia lakini kwa kweli hatujalizungumza sana humu ndani, maji ni tatizo kubwa zaidi katika nchi yetu. Mheshimiwa Dkt. Kafumu amezungumza pale, lakini tusipokuwa na fedha katika Mfuko huu wa Maji ndoto ya kuondoa tatizo la maji bado itaendelea kutusumbua Watanzania. Kwa hiyo, naomba tuliangalie jambo hili kwa kina sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa mara ya kwanza kwa kugundua kwamba crude oil kutoka nje yanashusha bei ya alizeti ambayo tunaizalisha Tanzania na inaweza kuongeza bei yake. Naomba kwa hili kwa kweli nimpongeze sana na Mungu aendelee kumbariki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la TRL na RAHCO, ni-declare interest, mke wangu ni mtumishi wa TRL, kuna haja gani ya kuwa na makampuni mawili ndani ya nyumba moja? Unganisheni iwe kampuni ya TRL ifanye kazi ya kuwatumikia Watanzania. Kama lengo ni kuwa na utitiri wa viongozi tu watafutieni mahali pengine, lakini kwa kweli suala hili ni muhimu sana, hebu angalieni muone namna gani mtafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye makusanyo ya fedha kwenye Halmashauri na Majiji, mimi naomba sana TRA wakusanye na ni nchi hii tu duniani sijawahi kuona labda Somalia kwa sababu sijawahi kufika, mtu anaweza kujenga ghorofa 25 haulizwi fedha katoa wapi, ni Tanzania tu. Huwezi kujenga nyumba Uingereza au Marekani usiulizwe fedha umetoa wapi, lakini ni nchi hii tu ambako mtu anaweza kwenda Magomeni akaporomosha ghorofa 25 haulizwi umetoa wapi fedha.
Kwa hiyo, naamini kama kodi itakusanywa na TRA, kwanza kutakuwa na nidhamu lakini tunaomba sasa mrudishe zile fedha kule kwenye halmashauri ili zikatumike vizuri. Naomba Serikali muwe makini kwenye jambo hili. Kama siyo fedha haramu, ni halali kwa nini msiwe mnahoji? How come leo kama mfano Mheshimiwa Keissy umkute anajenga ghorofa 25 pale Kariakoo, fedha anatoa wapi halafu Serikali mnamuacha tu. Waulize hawa watu fedha inatoka wapi ni halali au ni haramu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa nilitaka kuzungumzia suala la vifaa vya michezo kwa Tanzania. Michezo ni afya, hujenga urafiki, hujenga undugu lakini nchi nyingi duniani zimetambulika kutokana na michezo. Leo watu wanakesha tukiwemo Wabunge humu kuangalia Euro 2016, ondoeni kodi ya vifaa vya michezo. Vifaa vya michezo ni ghali sana na wanaoendesha michezo nchi hii wengi ni Wabunge. Hakuna Mbunge anayemaliza kipindi cha Bunge akaenda jimboni kwake bila kwenda na jezi, mipira na vitu vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mashindano ya UMISETA analetewa barua, mkoa sijui timu ya netball inakwenda wapi Mbunge, punguzeni ama ondoeni kabisa kodi ya vifaa vya michezo angalau kwa miaka miwili, mitatu tuweze kuondoka hapa tulipo twende tunapotaka kwenda. Nadhani tukifanya hivi tutakuwa tumefanya jambo la maana sana kwani tutaboresha michezo yetu kuanzia primary school, secondary school hadi katika vyuo vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kuwashukuru sana Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri, dada yangu hapo Dkt. Ashatu, niendelee kuwaombea ila nimkumbushe tu gratuity aachane nayo, atafute vyanzo vingine. Kwenye simu kuna hela, anzisha TV license, madini, fedha iko nyingi huko. Hii ya Wabunge wenyewe nilikuwa napiga hesabu haifiki hata shilingi bilioni nne, kwa nini tugombane kwa kitu kidogo hiki? Tuachie kwani hiyo fedha ndiyo inatujengea msingi mzuri. Kama nilivyomuomba mwaka 2020 ajaribu kugombea aone adha yake na kama hata hii gratuity huna sijui kama tutamuona hapa tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi namhakikishia kabisa, hii miaka mitano namuombea amalize aende jimboni tuone kama atarudi hapa kama ataondoa hii graduity. Kura za maoni tu saa nne misa ya kwanza pengine hayupo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe hii atusaidie sana ibaki tuendelee na sisi kwenda kujenga Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante.