Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nikushukuru kwa nafasi hii niliyoipata ya kuchangia bajeti ya Wizara yetu hii ya Maliasili na Utalii. Pia naomba niendelee kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Profesa Maghembe na kaka yangu Naibu Waziri, Mheshimiwa Mhandisi Ramo Makani. Nataka tu niwaambie kwamba wafanye kazi na wala wasitishike na haya manenomaneno mengine ya kuwavunja moyo na sisi tunaelewa juu ya weledi na uwezo wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine hata mimi naanza kushawishika kuunga mkono wale wanaofikiria kwamba kabla hatujaingia kwenye jengo hili tuwe tunapimwa pale kama tumevuta hata marijuana hivi. Katika hali ya kawaida, kijana hata kama umepigiwa kura na kuaminiwa na wananchi ukaenda kumtukana mzee wa namna ile na kumuita majina ya hovyo, lazima utakuwa una tatizo kidogo katika akili yako, siyo wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imedhihiri hata jana, yupo mwenzetu mmoja hapa wa kutoka katika chama ninachotoka mimi amezungumza mambo ya ajabu sana hapa. Unaweza ukaona ni kwa namna gani watu hawaelewi ni nani katika nyumba hii ameingia bila ya chama kilichomleta hapa. Wote kwa umoja wetu, iwe wa upinzani, iwe wa chama kinachotawala, sisi tumezaliwa na vyama vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima sisi kama viongozi tujue wajibu wetu na hii michezo haitaki hasira. Wala usidhani kwamba wewe ukiwa na hasira sana ndiyo hoja yako itafanikiwa, la hasha! Wakati mwingine unajielekeza tu katika kukata udugu. Nataka nikuhakikishie sisi kule kwetu tunasema mkataa udugu kala hasara huyo! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme juu ya misitu na Mheshimiwa mama Mariam Kisangi amesema vizuri hapa juu ya msitu, mkaa na vitu vya namna hiyo. Nafahamu kwamba mkaa, kwanza naomba ni-declare interest, mimi ni mwana mazingira na profession yangu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni Shahada ya Sayansi ya Mazingira. Nina weledi mzuri na mkubwa sana juu ya masuala ya mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Dar es Salaam nyumbani kwetu na Mkuranga yake watu wanaendelea kutumia nishati ya mkaa na Serikali tunajua kwamba inapiga vita matumizi ya mkaa. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba nguvu tunayoitumia katika kupiga vita matumizi ya nishati hii ya mkaa, tutumie nguvu hiyohiyo katika kuhakikisha tunawatafutia nishati mbadala wananchi hawa. Watu wanapata shida sana, watu hawaelewi wafanyaje, tunawaambia watumie gesi, hata elimu yenyewe ya matumizi ya gesi inafahamika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya gesi hayakuanza leo, watu walio wengi, hata wasomi wenyewe wanaogopa kutumia majiko ya gesi maana yameua watu wengi sana katika nchi hii. Wewe mwenyewe unafahamu mwaka mmoja, mwishoni mwa miaka ya tisini, hoteli ya Kibodi ya Dar es Salaam katikati ya mji iliungua moto kwa sababu ya jiko la gesi. Sasa tufanye jitihada ya kutoa elimu, kabla ya kusema kwamba watu hawa wasitumie mkaa, tumefanya jitihada gani ya kuwaelimisha, tumefanya jitihada gani ya kupeleka nishati mbadala? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti imezungumzwa hapa kodi ya vitanda nami naunga mkono hoja ya kodi hii ya vitanda ni lazima itazamwe, lasivyo yanaendelea kuwa ni yale yale ya kutokuwasidia watu hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa Msitu wa Mwandege pale Mkuranga, kile kimekuwa ni kichaka cha majangili. Mkuranga yenyewe imetajwa kama ni eneo ambalo si salama sana. Wewe mwenyewe unafahamu kwamba walikamatwa pale watu zaidi ya 50 na bunduki, wamezificha. Haukupita muda mrefu Benki yetu ya NMB pale Mkuranga ikavamiwa na majambazi. Hatujakaa muda mrefu Benki ya Access pale Mbagala Rangitatu ikavamiwa na majambazi. Hawa wote wanakimbilia kwenye msitu huo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kumwambia Mheshimiwa Waziri, kama tunashindwa kwa kuwa hatuna pesa za kutosha za kuutunza msitu ule Dar es Salaam imejaa, ni kweli. Eneo lile ni kubwa sana linachukua vijiji zaidi ya vinne Mwandege yenyewe, vikindu, Mlamleni Luzando na kwingineko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitenge eneo lile dogo tupate eneo la kutosha pale tujenge kituo cha kisasa, watu wanaotoka Mikoa ya Kusini hawana haja ya kwenda na mabasi yao mpaka Ubungo mpaka Dar es Salaam. Waishie pale Mkuranga waingie kwenye shuttles waende Dar es Salaam hii itatusaidia tutapata pesa tutafanya msitu ule kuwa ni botanical garden. Badala ya kuuweka tu vile kuwa ni kichaka cha majangiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niseme juu ya ng‟ombe na hasa hao wanaoingia katika maeneo ya hifadhi. Juu ya wakulima na juu ya ng‟ombe imeshazungumzwa sana. Naomba niseme wazi hapo kwetu sisi ng‟ombe ni kitu kipya, hapa nasema jambo jipya kabisa. Kwanza zamani tulikuwa tunamwita mdudu, leo tumeletewa ng‟ombe wengi sana na ugomvi ni mwingi sana pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama inavyosemwa na wenzangu ni lazima tutafute suluhisho la kudumu la jambo hili, wakulima wetu hawamjui ng‟ombe na wala hawana haja ya kumjua. Eee!
Mheshimiwa Mwenyekiti, issue ya misitu tena katika mazingira naomba nimwambie jambo moja Mheshimiwa Waziri kwamba hili jambo liwe ni two way traffic. Mpaka hivi sasa sisi tunatumia nguvu nyingi sana juu ya kulinda hifadhi zetu lakini bado hatujajifunza. Nilipokuwa Mkuu wa Wilaya kule Kilwa ninao mfano mzuri sana wa Kijiji cha Nanjilinji, tulikuwa na jambo kule la hifadhi ya misitu ya jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Nanjilinji kimefanikiwa sana katika uhifadhi wa jamii wa misitu yake. Leo mtu akikuona umeshika fito hawezi kukuelewa, lazima atakuchukulia hatua yeye mwenyewe pasipo kwenda na askari wa games wala jambo la namna gani. Kwa hivyo, hebu tuiangalie sera yetu vizuri hapa, namna ambavyo tunaweza tukawashirikisha jamii tukawasaidia ili wao wenyewe wawe walinzi wa rasilimali hizi badala ya kutumia maguvu mengi sana ambayo wakati mwingine wala hayana tija na yanatupotezea pesa zetu nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji nawahakikishia watani zangu Wasukuma na wengineo watoe mifugo ile; kule South Africa, Limpopo kwenye hifadhi ile maarufu kabisa ya Great Kruger pametokea tatizo. Ng‟ombe wote wamepata matatizo ya magonjwa ya miguu na midomo na ule ugonjwa sasa umeshaanza kutokea kwa wanadamu na umeshaingia mpaka Zimbabwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipofanya jitiada hao ng‟ombe watakufa na watu nao watakufa na mazingira yetu yataharibika. Kwa hivyo, ni lazima watu kukubaliana na jambo hili, ni kinyume cha utaratibu kabisa kufanya jambo la namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalize na utalii. Nafasi ya Tanzania katika utalii ni nzuri, tunahitaji kufanya jitihada zaidi ili kuhakikisha kwamba utalii wetu uweze kuwa na faida hasa ya kuondoa umaskini. Juzi hapa China tarehe 21 umemalizika Mkutano wa World Tourism Organization, ulifanyikia Beijing pale, moja ya jambo kubwa kabisa lililokubaliwa katika mkutano ule ni kuhakikisha kwamba utalii uondoe…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.