Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nami nichangie katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Niungane na wenzangu kupongeza uteuzi wa Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe katika nafasi hii nyeti na ngumu kidogo ya Uwaziri pamoja na Naibu Waziri. Niwapongeze kwa kuteuliwa lakini niwapongeze kwa kazi yenu nzuri mlizozionyesha toka mmeteuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni miongoni mwa Wabunge ambao majimbo yao yanapakana na mapori ya akiba. Napakana na pori la Rungwa Game Reserve na Muhesi, liko katika Halmashauri yangu mpya ya Itigi lakini Jimbo la Manyoni Magharibi. Ni miongoni mwa wanufaika wazuri sana na mapori haya na mchango wao mkubwa umekuwa ukisaidia vijiji vyetu katika maendeleo mbalimbali kutokana na mgawanyo ule unaotokana na asilimia ile ambayo inapelekwa katika vijiji na pia katika Halmashauri husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi hiki cha madawati na sisi ni miongoni mwa watu ambao tumenufaika kwa pesa zile lakini hatujajua tu hizi zilizotolewa na Wizara ni kiasi gani tutapata. Sasa si vibaya Mheshimiwa Waziri akatuonesha Halmashauri yangu ya Itigi imepatiwa nini kwa sababu nasi tunapakana na Game Reserve hizi za Rungwa na Muhesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na matukio na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa kazi za kila siku za Wizara hii hususani katika vijiji vinavyopakana na hifadhi hizi. Kumekuwa na tatizo ambalo sijui ni la watumishi, sijui ndiyo sera ya Wizara, lakini dhana yangu nadhani ni kwamba baadhi ya watumishi wanapelekea sasa Wizara hii iendelee kulaumiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la watumishi hawa ambao wamekuwa wanajihusisha sana na rushwa ndio wanaofanya leo Mawaziri toka mwaka 2010 waliopita katika Wizara hii wamekuwa na hesabu kubwa na wengine wakiwa wanatoka kwa muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi hawa wameendelea kuwepo pale na watumishi wa juu sana ni watumishi wa kati kati wakiwemo Maafisa hawa wa Wanyamapori tuseme Maaskari wa Ma-game hao wanachukua pesa kidogo wanawaweka watu katika hifadhi wanaposhindana ndipo migogoro inapokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu miaka miwili iliyopita kulitokea tatizo kama hili, walishindana na kijana mmoja katika Kitongoji cha Matumaini katika Kijiji cha Kintanula, yule Bwana aliuwawa kwa kutofautiana tu lakini hadi leo hamna taarifa nzuri iliyotokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi majuzi tu hata mwezi bado katika Kijiji cha Mwamagembe Maaskari wa reserve walimuua kijana mmoja. Walikwenda kijijini akawasaidie kwenda nao porini kutafuta majangili kwa sababu wanakuwa na knowledge ya kujua ni nani na nani wanaojishughulisha; walipofika yule kijana mmoja walimuua wao wakasema kauawa na majangili. Lakini wale watatu wengine ambao walikwenda nao walikuja kuonekana baadaye. Bahati mbaya au nzuri shauri hii tumeliachia vyombo vya usalama vishughulike nalo pamoja na Diwani wa Mwamagembe ambaye alifichwa juu ya tukio hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na-declare interest, mimi ni mdau katika uvunaji wa mazao ya misitu katika nchi hii lakini pia nashughulika na usafirishaji wa mazao haya ya misitu nje, sasa nihamie katika sekta ambayo naijua vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna jambo hili la recovery rate ya mbao ambayo ni asilimia 30. Recovery hii iliwekwa wakati ule mashine zilipokuwa za kizamani, misumeno ilikuwa na milimita zaidi ya tano, sita; sasa hivi taaluma imeongezeka, teknolojia imepanda bado tuna-recovery rate ya asilimia 30 ambayo inapelekea kuchonganisha wadau wavunaji wa mazao ya misitu pamoja na Maafisa ambao wanakagua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka porini kupata 70 percent ni sawa, recovery ya asilimia 60 ya slipper ni sawa, kunakuja shida hapa tunapokuja katika recovery ya asilimia 30 ya mbao. Ukitumia mashine nzuri recovery ni kubwa sasa unapoonyesha kiwango kikubwa basi inakuwa tatizo linahamia hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Wizara ichukue juhudi za makusudi kabisa kupitia Taasisi zake za FIT lakini na Taasisi zingine ikiwepo TAFORI kufanya tafiti za sasa recover rate iliyo nzuri kwa mbao ni ipi ili kuondoa mgogoro huu ambao unatengeneza rushwa kwa sababu wale wakaguzi wanatumia fursa hii ya wavunaji wengi wasiojua hesabu za kutafuta volume hii ya cubic meter kuwasulubu kwa kutumia Sheria namba 14 ya mwaka 2002.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utendaji mbovu wa baadhi ya maafisa hawa ambao tumesema katika Wanyamapori lakini huku upande wa misitu ndio umekithiri sana. Kamati ya TFS tangu imeundwa imekua ni taasisi iliyofanya kazi vizuri sana kuanzia juu mpaka katikati; lakini kule chini bado ni kuzuri, hapa katikati ndiyo kuna shida kama nilivyokwisha kusema. Kuna Maafisa ambao wanafanya kazi kwa kutegemea sana kupata kipato nje ya mishahara yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ndio wanaopelekea leo Mawaziri wengi wanasulubiwa. Hapa katikati Mheshimiwa tunavyovizuia ambavyo ukaguzi wake haueleweki, ni vigumu sana kukagua mzigo ukiwa ndani ya gari, lakini kuna checkpoint ya mwisho, Mbezi pale ambayo nayo wanakagua, bandarini ambapo mizigo ya export inapelekwa nayo ina ukaguzi; kuna Maafisa zaidi ya saba pale, lakini hawaaminiani, hakuna Afisa mmoja anayekuwa na maamuzi mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe Wizara hii, ni wakati umefika wa kufanya kama walivyofanya TRA. TRA wao walikuwa wanakimbizana hivi hivi na wadau wao, lakini mwisho wa siku walipoamua kuwa waaminifu, wakweli kwamba wewe unatakiwa kulipia kodi ya asilimia ya pesa hizi, basi watu wote walipe asilimia hizo. Yule mwingine anayekuja ana-verify kwamba wewe ulistahili kulipa hiki. Na kama hukustahili kulipa anafanya maamuzi ya papo kwa hapo na ni maamuzi ambayo yana tija na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwenye TFS watumishi wao wamekuwa na shida. Kuna miongoni mwao Mheshimiwa Waziri nilishampa na taarifa na anajua, jinsi wanavyotumia udhaifu huu wa watu hawa ambao hawajui kutengeneza volume hii ya cubic meter, wanavyosulubiwa na Maafisa hawa. Anatumia kutokujua kwa yule mtu anam-sue mara mbili na anam-compensate mara nne zaidi ambacho hawakupaswa kukilipia. Sasa shida ni pale anapokutana na watu kidogo wanaojua ndipo linakuwa tatizo. Tuliwaambia huyu mtu amekuwa akitajwa mara nyingi, amekuwa akizungumzwa na watu wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri sasa asiingie katika mtego ambao wamekuwa wakiingia Mawaziri wengi, wa kukumbatia watu na taasisi za rushwa zilishawakamata, lakini kwa sababu ushahidi wa moja kwa moja unakuwa ni mgumu kumtia hatiani mtu wa namna ile, ni vizuri akaondoka katika lile eneo ambalo nadhani kwamba atatengeneza mazingira ya kupata rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nataka nizungumzie leo kinachoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam. Inapofika mwezi wa Saba, Wizara hii huwa inatoa kitu kinachoitwa approval, yaani nikibali cha mtu kusafirisha mazao ya misitu nje ya nchi. Kile kibali kinampelekea mtu aingie mikataba na mabenki na wadau mbalimbali….
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.