Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Godfrey William Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia jioni ya leo.
Awali ya yote, napenda sana kuwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Kalenga kwa nafasi ambayo wamenipa kuweza kuliwakilisha Jimbo langu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara nyingine tena, mara ya pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huu wa Miaka mitano tunaenda kuchangia kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao, ningependa kuchangia mambo kadhaa yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kujikita kwenye masuala mazima ya ujenzi wa reli. Suala la Reli ya Kati ni suala la muhimu na kwa namna yeyote ile, uchumi wetu wa viwanda ambao tunaenda kuufanya katika kipindi hiki, lazima utegemee mawasiliano ya reli na biashara zake kwa ujumla.
Kwa hiyo, ni lazima tuangalie ni namna gani reli hii tunaweza tukaijenga na Serikali iseme kinagaubaga kwamba ni maeneo gani ambapo reli hii itaenda kujengwa ili tutakapokuja katika Mpango unaofuata tuweze kujua kiuhalisia kwamba Serikali ilifanya nini na imefanya wapi. Tunajua reli ya kati inapita katika mikoa gani, lakini tunaomba katika yale maeneo ya michepuko, basi tujue wazi Serikali inaongea maeneo gani katika uwakilishaji wa reli hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa sana kuzungumza ni kwamba katika masuala haya, hasa katika viwanda tunavyovizungumzia, masuala ya viwanda yanaendana moja kwa moja na masuala ya umeme na upatikanaji wa elimu bora. Hatuwezi tukazungumzia masuala ya upatikanaji wa viwanda kama elimu yetu ni duni.
Vile vile hatuwezi tukazungumzia masuala ya viwanda kama masuala mazima ya nishati ya umeme bado haijapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda sana kuanza kuwashukuru na kuishukuru Serikali na Mheshimiwa Mhongo kwa kazi nzuri wanayoifanya, wametuonesha njia, hata kule vijijini umeme sasa hivi unawaka. Mheshimiwa Mhongo nakushukuru sana, katika vijiji vyangu 84, leo hii tunazungumza vijiji kama 50 hivi ambavyo vimeshapata umeme. (Makofi)
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Kwa hiyo, nakushukuru na naomba Mheshimiwa Muhongo na Wizara yako tuweze kufanya namna, tuweze kufika katika Jimbo langu, wananchi bado wanahitaji umeme. Ninaamini Mheshimiwa Muhongo na Serikali kwa ujumla na Wizara tutafanya kila namna tuweze kuhakikisha kwamba vijiji vilivyobaki vinapata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa upatikanaji wa umeme katika vijiji hivi ndiyo itatoa dira nzuri ya namna gani tunavyoweza kusonga mbele katika masuala haya ya ukuaji wa viwanda. Tunavyoongelea masuala ya viwanda, ni muhimu sana kujua kwamba ikiwa kama gesi ambayo tayari tumeshaivumbua huko Mtwara tutaitumia vizuri na itakwenda kuwakilishwa au kwenda kutumika ipasavyo katika maeneo yetu, ina maana kwamba upatikanaji wa viwanda utakuwa ni mwepesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika kupatikanaji wa viwanda, ni lazima tujue Serikali ina malengo gani au inalenga viwanda vya namna gani? Ni viwanda vya namna gani ambavyo Serikali inakwenda kuvijenga? Siyo tuamke asubuhi na kusema tunaenda kujenga kila aina ya Kiwanda, hatutaweza. Nchi yetu bado ni changa, tunahitaji tuweze kupata mchanganuo ni namna gani au Serikali imejipanga vipi katika ujenzi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashauri kwamba katika upande wa kilimo, kuna maeneo mbalimbali hasa ukiangalia maeneo ya nyanda za juu Kusini, tunalima sana mahindi na maharage, lakini bado hatuna viwanda ambavyo vinaweza kusaidia kuchakata haya mambo na kuhakikisha kwamba tunapata mazao na masoko bora katika maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, tukitaka kuangalia, Mkoa wa Iringa kipindi cha nyuma kulikuwa na Shirika la NMC; Shirika hili limekufa na hatujui litafufuka lini. Nina imani kubwa sana na Serikali ya Chama cha Mapinduzi; na naamini kabisa Serikali ya Mheshimiwa Magufuli itakwenda kufufua viwanda hivi na kile kiwanda cha NMC ambacho kipo pale Iringa kitaenda kufufuliwa tuweze kupata nafaka kwa sababu kilikuwa kinainua uchumi katika Mkoa wetu wa Iringa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitaka kuangalia katika maeneo mengine ya namna gani tunaweza tukakuza uchumi wa nchi yetu; nchi yetu bado ina matatizo makubwa sana katika upatikanaji wa mapato, nami lazima niongelee suala hili kwa sababu Bunge la Kumi lililopita, nilikuwa Mjumbe katika Kamati ya Bajeti. Tulijaribu kugusa maeneo mbalimbali kuona kama tunaweza tukafanikiwa vipi katika maeneo ambayo tunaweza tukapata vyanzo mbalimbali vya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo Serikali bado inasuasua. Kuna maeneo ya uvuvi wa Bahari Kuu. Uvuvi wa bahari kuu ni uvuvi ambao Tanzania bado tupo nyuma na nchi za kigeni, wageni wanaendelea kuhakikisha kwamba wanaifilisi nchi yetu katika uvuvi wa bahari kuu. Lazima tuamke tuweze kuona kwamba uvuvi wa bahari kuu tunaufanyia kazi na Serikali inaingiza nguvu zake za kutosha ili kuhakikisha kwamba mapato yanapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania leo hii tuna loss ya zaidi ya Shilingi trioni moja kwa kutojiingiza kwenye uvuvi wa bahari kuu. Kuna wageni (foreigners) wengi ambao wanaenda kule kuhakikisha kwamba wanapata samaki, lakini vilevile tukiangalia soko la samaki katika bei ya dunia, liko juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uvuvi wa samaki wanaoitwa Tuna, ambao leo hii samaki hao kwa kilo moja inaanza Dola 10 mpaka Dola 50, lakini bado nchi yetu ya Tanzania hatujajikita huko kuhakikisha kwamba tunapata mapato ya kutosha. Leo hii bado tunaendelea kuwadidimiza wafanyabiashara ndogo ndogo ambao bado mitaji yao ni midogo. Ni lazima tuangalie maeneo makubwa kama haya ili kuhakikisha kwamba tunapata uchumi ambao ni endelevu na uchumi wetu binafsi, tukaachana na uchumi ule wa kuendelea kukopa nje wakati tunavyo vyanzo vyetu wenyewe katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningalie pia suala la utalii; nyanda za juu kusini tumeachwa sana. Najua kabisa kuna mambo mengi yanaendelea Kaskazini, nchi yetu ni moja lakini lazima Serikali iweze kuangalia maeneo ambayo tunaweza kupata vyanzo vya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Iringa tuna Mbunga ya Ruaha. Mkoa wa Iringa bado tunaendelea katika utaratibu wa kukuza viwanja vyetu vya ndege. Mheshimiwa Rais allivyokuja alituambia watu wa Iringa kwamba atahakikisha Airport yetu ya Mkoa wa Iringa inafufuliwa na inaendelea kuleta watalii katika Mkoa wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbuga yetu ya Ruaha ambayo inapita kwa Mheshimiwa Lukuvi, inapita kwenye Jimbo langu, bado mapato hatupati, jambo ambalo ni la ajabu na kusikitisha. (Makofi)
Vile vile upande wa kusini niliongea juzi, nikasema kuna Mbuga la Selous ambayo bado nayo tukiamua kuitumia vizuri kwa miundombinu yetu tuliyonayo tunaweza kupata fedha nyingi za kigeni na kuhakikisha kwamba tunasonga mbele kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kuisihi Serikali, kuhakikisha kwamba tunafanya kila njia kuweza kuangalia nyanda za juu kusini na maliasili zake kuhakikisha kwamba tunasonga mbele na tunapata hizi fedha ambazo Tanzania bado haijazipata ili kuhakikisha uchumi wetu unasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo kama sitazungumzia masuala ya maji. Jimbo langu la Kalenga lina matatizo makubwa sana ya maji.
Nimeongea na Mheshimiwa Waziri, tukakubaliana kwamba tuongee kuhusu masuala ya maji na naendelea kukuomba Mheshimiwa Waziri wa Maji. Naomba miradi mitano ya maji ambayo haijakamilika katika Jimbo langu, ikamilike, tuokoe akina mama! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la maji bado ni kubwa! Wakandarasi hawajalipwa! Naomba fedha ambazo wanadai watu hawa ziweze kulipwa mapema ili bajeti inayokuja tusiweze tena kufika hapa, tukaanza kubishana na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana fedha zifike Halmashauri, Wakandarasi walipwe, waendelee kufanya kazi, miradi ikamilike, wananchi wapate faida na waendelee kuwa na matumaini na Chama chetu na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kuendelea lakini, napenda sana kurudia kwamba suala hili la maji ni la muhimu. Tuhakikishe kwamba Wizara ya Maji inawezeshwa, inapata fedha na inafika vijijini kuhakikisha kwamba maji yanaweza kuwafikia wananchi. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mgimwa, ahsante sana, muda wako umekwisha.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.