Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia katika bajeti hii. Kwanza kabisa, nikupe pongezi kwa kukiendesha vizuri Kiti hicho. Naomba sana kisimamie, endelea na msimamo wako huo huo na Mwenyezi Mungu azidi kukuongoza, kila siku uwe pale pale, nakuombea Mwenyezi Mungu akutangulie katika kukalia Kiti hicho.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba kumpongeza Waziri pamoja na Naibu wake kwa kutuletea bajeti nzuri. Nawapongeza Wizara na Serikali kwa sababu hii bajeti ni nzuri, inajielekeza kutatua kero za wananchi. Pia naipongeza Serikali kwa kutenga asilimia 40 za bajeti nzima kwenda kwenye miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo muhimu naomba sana hizi hela zipatikane kwa sababu zikipatikana zitafanya kazi muhimu kama ilivyopangwa. Uzoefu uliokwishajitokeza ni kuwa tunapitisha hela nyingi za kufanya mipango kama ilivyopangwa vizuri sana lakini hela hazipatikani kama tulivyopanga na haziendi maeneo husika kama tulivyopanga na kufanya miradi ya maendeleo kutotekelezwa kama tulivyopanga. Bajeti hii ni nzuri sana kwa sababu ina ongezeko la asilimia 31. Shilingi trilioni 29.5 zikitumika vizuri naamini kuwa kero za wananchi zitaweza kutatuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naomba kuliongelea ni kuhusu shilingi milioni 50 ambazo zitapelekwa kwa kila kijiji na kila mtaa. Namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anajumuisha aweze kufafanua vizuri hizi shilingi milioni 50 zinakwenda kwenye vijiji au mitaa? Kwa sababu kwenye hotuba yake alisema kwenye vijiji lakini kwenye ahadi za Mheshimiwa Rais alisema zinakwenda kwenye vijiji pamoja na mitaa na sisi wananchi wetu tumewaambia kuwa hela zinakuja shilingi milioni 50 kwenye vijiji na kwa kila mtaa. Naomba awaelezee vizuri, kama tunaanza kwenye vijiji sawa, kama tunaendelea na mitaa sawa lakini wananchi wetu waweze kuelewa hizi hela zinakwenda wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, nashukuru kwa sababu zinaelekezwa kwa vikundi vya vijana pamoja na vikundi vya akinamama kama mikopo. Ninachoomba iwe revolving fund (hela mzunguko) kusudi watakaorudisha ziweze kukopwa na watu wengine kwenye area hiyo hiyo bila ya kurudishwa Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu kampeni za Mheshimiwa Rais na kati ya mambo aliyoyasemea ni maji. Alisema wanawake waache kubeba ndoo lakini mpaka sasa hivi wanawake bado wanabeba ndoo. Kwa hiyo, tunaomba hii bajeti ya 2016/2017 iweze kutatua jambo hili la kubeba maji hasa wanawake, waweze kuacha kubeba maji vichwani mwao na wenyewe wachane nywele zao na kufanya kazi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yetu ya Maji na Kilimo iliongelea kuhusu tozo ya Sh. 50 iweze kuongezeka kwenda kwenye Sh.100 hasa kwenye mafuta kwa kila lita ya diesel na petrol. Hata hivyo, kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri haipo, naomba sana Mheshimiwa Waziri akubaliane na sisi kusudi huo Mfuko wa Maji uweze kutuna kusudi hela zitakazopatikana ziweze kupeleka maji vijijini pamoja na hela zingine tulikuwa tumesema bilioni 30 ziweze kwenda kwenye kujenga zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalopenda kuongelea ni afya. Wewe na Wabunge wenzangu mnakubaliana kuwa ni kweli vituo vya afya vimejengwa katika kila kata na zahanati zimejengwa lakini mpaka sasa hivi nyingi ni maboma. Wilaya ya Ulanga, Mbagamao ina zahanati ambayo bado haijakamilika mpaka sasa hivi. Hivi ninavyoongea sasa hivi kwa mfano kule Morogoro Vijijini, hatuna Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondoa tatizo la vifo vya akinamama na watoto tunaomba sana hii ahadi iweze kutekelezwa hasa yale maboma ambayo yameshajengwa yaweze kukamilika ili yawe vituo vya afya, zahanati na hospitali. Pia tunaomba sana kwa akinamama, kuna wale wanaopata matatizo ya kujifungua, theatre ziwepo ili waweze kupata msaada wa kujifungua na kufanya operesheni kwenye vituo vya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naweza kuongelea ni kuhusu kilimo. Ili tupate viwanda lazima tuwe na kilimo, umeme na maji. Kilimo chetu bado hakijatengewa bajeti ya kutosha. Maazimio ya Malabo pamoja na Maputo ya kutenga asilimia 10 ya bajeti yote kwenda kwenye kilimo bado hayajatekelezwa. Asilimia 75 ya wananchi wanategemea kilimo na kilimo ndiyo kitaweza kuondoa umaskini wa Mtanzania lakini mpaka sasa hivi naona maazimio haya bado hayajatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hata hizo hela chache ambazo zimetengwa kwenye upande wa kilimo ziweze kwenda zote. Kilimo cha umwagiliaji ndiyo mkombozi wetu, tabia nchi mnaiona, nchi yetu inakuwa jangwa, miti inakatwa hovyo, naomba Mheshimiwa Waziri atenge hiyo hela iweze kwenda kwenye kilimo. Naomba sana bajeti inayokuja iweze kukipa kipaumbele kilimo kwa sababu Watanzania wanategemea sana kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa viwanda, viwanda vingi vya Morogoro vimekufa. Kuna mikoa ambayo imetajwa kuwa ni ya viwanda lakini hapo mwanzoni hata Morogoro ilikuwa ni mkoa wa viwanda. Tulikuwa na viwanda 11 mpaka sasa hivi yapata kama viwanda nane vyote vimekufa havifanyi kazi, inakuwaje? Naomba sana hivi viwanda kama alivyosema kwenye bajeti viweze kufufuliwa na viweze kufanya kazi. Kwa mfano, kiwanda cha Moproco, kiwanda cha ngozi na viwanda vingine vyote viweze kufanya kazi kusudi akinamama na vijana waweze kupata kazi ya kuajiriwa kwenye viwanda hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu elimu, hapa kuna ukarabati na ujenzi wa vyuo vikuu, Serikali tunaongeza vyuo ni vizuri sana lakini vyuo vikuu vile vya zamani kama SUA, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam viweze kukarabatiwa ili viweze kuendelea vizuri ndiyo na vyuo vikuu vingine viweze kujengwa. Naona zimeanzishwa degree programs, kwa mfano University of Dar es Salaam wameanzisha digrii ya kilimo, je, wana Walimu? Imeanzishwa digrii ya medicine, kuna Muhimbili na Mloganzila imeshajizatiti sawasawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali yetu iangalie kwanza vitu vile vilivyokuwepo ndiyo tuweze kuanzisha vingine. Kwa hiyo, naomba hivyo vyuo nilivyovisema viweze kukarabatiwa na miundombinu iweze kuangaliwa. Pia hela za maendeleo hazijapelekwa mpaka hivi ninavyosema…
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana ingawa muda ulikuwa mdogo sana. Naunga mkono hoja.