Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kunijalia tena kwa mara nyingine kuwepo katika Bunge hili. Pia nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Musoma kwa kuweza kunipa ridhaa hii kwa mara nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, naomba nijielekeze moja kwa moja katika mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2016/2017. Kazi yetu ni kuishauri Serikali. Wakati najaribu kupitia Mpango huu kwenye ule ukurasa wa 24, umesema wazi kwamba malengo mahususi ni kuimarisha kasi ya ukuaji na kuongeza uchumi. Hii ni pamoja na uchumi huo uweze kuwanufaisha wananchi waliyo wengi, pamoja na kuongeza fursa za ajira hasa kwa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Waziri wa Fedha na Mipango. Kusema kweli amepanga mipango yake vizuri. Ukisoma kwenye huu ukurasa wa 24 mpaka 26 na kuendelea mbele, mipango iliyopangwa ni mizuri sana. Wenzetu wamekuwa wakitubeza kwamba sisi ni wazuri kwa kupanga mipango, lakini tuna tatizo la utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kupitia Mpango na kusoma ukurasa wa 37, kwamba mojawapo ya mikakati ya kutekeleza mipango hii ni pamoja na kuwa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kwa maana ya Public, Private Partnership. Mashaka yangu yawezekana pamoja na mipango yetu mizuri, lakini bado tukakwama kwa sababu ya ukwasi wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka tu kushauri au kuchangia katika maeneo manne, nilitaka kuchangia katika eneo la viwanda, kilimo, uvuvi pamoja na mifugo kama muda utaniruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tunataka kuendeleza viwanda, maana Mpango huu mlisema umebainisha namna ambavyo hivi viwanda vinavyotakiwa kwa maana ya vile viwanda vitakavyosaidia kuajiri watu wengi zaidi. Kwa upande wa viwanda, kama tunahitaji kuona Matokeo Makubwa ya Sasa, nashauri tujielekeze kwenye vitu vitatu; kwanza, tuendelee kupanua hivi Vyuo vyetu vya VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Musoma kipo Chuo cha VETA kimoja ambacho kinachukua wanafunzi kila mwaka wasiozidi 200, sasa ukiangalia wanafunzi wanaomaliza Darasa la Saba pamoja na Kidato cha Nne wale ambao hawapati nafasi ya kuendelea Kidato cha Tano, maana yake tuna wanafunzi wasiopungua 6,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Chuo cha VETA kinachukua wanafunzi wasiozidi 200 tafsiri yake ni kwamba watoto zaidi ya 5,000 wanakaa Mtaani na hawana kazi ya kufanya. Kwa hiyo, nadhani tukiongeze wigo wa Vyuo vya VETA pamoja na Vyuo vya Ufundi kuchukua wanafunzi wengi, matokeo yake tutapata wanafunzi wengi wenye elimu ya kawaida ya ujasiliamali, elimu ya kawaida ya ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitoka hapo kama tumepanga kujikita kwenye viwanda, ningeshauri tufufue lile shirika letu la viwanda vidogo (SIDO)..
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba leo tukipata Mkurugenzi Mtendaji mzuri wa SIDO, mfano kama alivyo yule Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba, akaangalia namna gani mafunzo mengi yanaweza kutolewa kwa vijana wengi zaidi; yale mafunzo yatawasaidia kuwajenga vijana wetu, wapate elimu ya ujasiriamali, tena kwa gharama nafuu. Maana kama wote mmetembea; Waheshimiwa Wabunge nadhani ninyi ni mashahidi, mafunzo mengi ya watu wanayojifunza Kule SIDO, kitu kikubwa kwanza wanajifunza usindikaji. Kama ni usindikaji wa alizeti, watajifunza; kama ni wa unga watajifunza, lakini ni pamoja na ufundi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani watakapoenda pale watajifunza usindikaji pamoja na mambo ya packaging. Kwa kufanya hivyo sasa itawapa nafasi ya kuwa na bidhaa ambazo sisi wenyewe tutazitumia na hata nchi zote zinazotuzunguka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda nchi kama Kenya kuna hawa wanaoitwa Juakali. Juakali Kenya ina nafasi kubwa sana na inawasaidia watu wengi sana. Kwa hiyo, ukiangalia hili Shirika letu la SIDO kama tukilifufua na likapata mwendeshaji mzuri, ni dhahiri kwamba tutakuwa na vijana wengi ambao watakuwa na ujuzi wa kuweza kujiajiri. Kwa utaratibu huo sasa, hata hizi taasisi zetu za fedha ni rahisi kuwapa fedha kwa kuwakopesha kwa sababu tayari wanao ujuzi utakaowasaidia katika kusukuma maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine basi, hebu tuendelee kuimarisha hizo Ofisi zetu za Ubalozi. Maana Ofisi zetu za Ubalozi ni kwamba tukiwa na wale ma-business attache wataweza kujua kwamba bidhaa gani zinazotakiwa huko ili waweze kutusaidia watu wetu hawa waweze kuuza huko.
Eneo lingine ni eneo la kilimo, mfano pale Mara, tunalo eneo kama lile shamba la Bugwema ambalo ni heka 20,000, mashamba kama haya yako mengi katika nchi hii. Leo ukitangaza tenda ya nani yuko tayari kufanya irrigation katika eneo hilo, labda katika kipindi cha miaka kumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka Serikali inawalipa fedha za kufanya irrigation, matokeo yake ni kwamba lile bonde lenyewe linaweza kuzalisha mazao mengi kama mpunga, alizeti ambayo itasaidia sana watu wetu, siyo wa Musoma peke yake wala si wa Mara, lakini maeneo kama haya yako mengi ambapo Serikali nadhani kwamba ikijikita katika utaratibu huo itaweze kusaidia watu wetu wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unapozungumza kwenye suala la mifugo, nini kifanyike? Tunahitaji tutenge maeneo madogo, maana Mpango huu umesema tunahitaji tufungue Vituo vya Uhamilishaji.
Ni kweli kwamba tatizo kubwa tulilonalo, ng‟ombe wetu; sisi ni wa tatu katika Afrika, lakini ng‟ombe wetu thamani yao ni ndogo. Tunachohitaji, ni lazima tufanye crossbreed ili tuzalishe mifugo ambayo itakuwa na tija.
Kama hivyo ndiyo basi, sasa ni lazima tuwe na vituo kama vile ambavyo vitazalisha ng‟ombe wanaokuwa haraka ndani ya kipindi cha miaka miwili unaweza kuuza ng‟ombe kwa Shilingi milioni moja, mpaka Shilingi milioni mbili kuliko hawa wetu unawachunga miaka mitano mpaka minane lakini unauza kwa Sh. 500,000/= ambazo hazina tija. Kwa hiyo, tunadhani hilo nalo katika mipango yetu linaweza likatusaidia katika kuhakikisha kwamba tunaendelea. nashukuru sana. (Makofi)