Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru kupata nafasi hii kuweza kuchangia bajeti ya mwaka huu. Kwanza napenda kukupongeza sana wewe kwa ujasiri ambao unao na katika hali ya sasa hivi jinsi ambavyo unaliendesha Bunge hili. Nakupongeza na haya matatizo ya wenzetu yasikupe tabu sisi tunaku-support moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kumshukuru Waziri, Naibu wake na wataalam wake ambao wameweza kutuletea bajeti nzuri ambayo haijawahi kutokea tangu tumepata uhuru. Ni bajeti yenye mwelekeo ambayo inajieleza yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi kifupi tu tangu Awamu ya Tano imeingia madarakani imeweza kukusanya mapato mengi sana ambapo nchi yoyote bila kuwa na mapato haiwezi kwenda vizuri. Mapato ni kitu cha msingi kwenye nchi yoyote. Hata ukiangalia wakati wa ukoloni ukusanyaji wa kodi ni kitu muhimu, kulikuwa na kodi za vichwa, kulikuwa na kodi za vipande na kodi za matiti. Zote hizo zilikuwa ni kodi ambazo zinakusanywa kwa lengo la kuweza kupata mapato ya Serikali na kuweza kufanya nchi iweze kuendelea, nchi iweze kutengeneza miundombinu mbalimbali. Ndiyo maana mpaka leo hata wenzetu wa Ulaya watu ambao wanakwepa kulipa kodi wanakwenda jela. Hapa tuna kesi ya mcheza soka bora duniani Lionel Messi ambaye yuko Mahakamani kwa kosa la kukwepa kodi. Sasa huo ni mfano tu wa kuonesha namna gani kodi ni muhimu katika kuendeleza maendeleo ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii kama ambavyo ilivyo asilimia 40 imekwenda kwenye maendeleo, ni kitu ambacho hakijawahi kutokea hapa nchini na imelenga kuleta maendeleo kwenye maeneo mbalimbali. Mheshimiwa Waziri pia kwenye bajeti hii ameweza kuangalia ni vitu gani ambavyo vinaweza kuboreshwa kwenye huduma za jamii, mambo ya maji, umeme, barabara na mambo mengine kwa lengo la kuweza kupata maendeleo ya haraka hapa nchini. Hii ni pamoja na bajeti ambayo imejikita zaidi kuondoa tozo mbalimbali kwa manufaa ya wakulima. Kuna tozo zimeondolewa, tozo za mazao ya korosho, chai, pamba na kadhalika. Sasa yote haya ni muono wa bajeti hii ambao kwa kweli naunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na yote hayo ningependa Mheshimiwa Waziri na wataalam wake wajielekeze kwenye baadhi ya maeneo ambayo ningependa kuyataja. Wakati tunachangia Wizara ya Maji, Wabunge wengi sana walisisitiza suala la Wakala wa Maji Vijijini. Suala hili lingepewa umuhimu wa kipekee kwa sababu tatizo la maji ni kubwa hapa nchini, hata Jimboni kwangu ndilo tatizo linaloongoza. Kwa hiyo, uanzishwaji wa Taasisi ya Maji Vijijini ni muhimu na naomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kuliangalia aone kama anaweza kulipenyeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni road toll. Road toll kwenye nchi hii naona halipewi umuhimu, nikiambiwa kwamba kodi yake imeongezwa kwenye mafuta lakini huwezi kuona impact hiyo. Nchi nyingi duniani kubwa na ndogo ukiangalia zimewekwa road toll barabarani. Nashangaa ni kwa nini sisi hatuwezi kuiga na kuona kwamba tunaweza tukapata mapato mengi kutokana na road toll. Naamini kabisa kwenye highway zetu pamoja na matatizo ya barabara zetu kuwa ndogo lakini tukianzisha road toll tunaweza kupata mapato ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la transit good, sasa hivi naambiwa kwamba meli nyingi zinakwepa kuja Dar es Salaam na meli nyingi sasa hivi zinakwenda Beira na Maputo kwa sababu ya VAT ambayo imewekwa kwenye transit goods. Ni vizuri Waziri akaliangalia eneo hilo kama ni kweli akaangalia namna gani anaweza kutoa hiyo VAT ya asilimia 18 ambayo inatukosesha malipo ya transit kwa mizigo ambayo inapita hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni reli ya kati. Naipongeza kabisa kwamba bajeti hii imegusa reli ya kati kwa standard gauge, lakini nasikitika kwamba sijaona reli ya kwetu, reli ya Tanga sijaiona kwenye bajeti hii ambayo nilitegemea hata itaguswa pia. Pia nasikitika sijaona maboresho ya bandari ya Tanga ukitilia maanani bomba tumelipata kutoka Uganda. Kwa hiyo, labda Mheshimiwa Waziri aangalie namna atakavyoweza kupenyeza suala hilo ambalo ni muhimu ili vitu hivyo viende simultaneously, reli ya Tanga pamoja na reli ya kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefarijika sana kuona kwamba tutanunua ndege tatu, ndege ambazo naamini kabisa zitatuletea wawekezaji na watalii wengi. Nasikitika kuona kwamba kwenye suala la watalii Kodi ya Ongezeko ya Thamani imewekwa pale kinyume na wenzetu wa Rwanda na Kenya ambao wameondoa kodi hiyo. Kwa hiyo, hii ina maana kwamba watalii ambao watakuja wote wataishia Kenya ukitilia maanani kwamba wao usafiri wa ndege ni wa uhakika na wanao. Kwa hiyo, ni vizuri eneo hilo pia akaliangalia kama ambavyo ameweka kwenye page yake ya 49. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi ni muhimu na ambalo Mheshimiwa Rais ameliongelea tangu wakati wa kampeni. Mahakama hii inategemea sana ripoti au taarifa kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali. Katika kesi ambazo naamini zitapelekwa kwenye Mahakama hiyo robo au nusu ya kesi hizo zitatokana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali. Ni kilio cha Wabunge wengi ambao wameongelea, hivyo ni vizuri wakaangalia eneo hilo, namna ambavyo wataweza kuwaongezea fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine la kodi ambayo imeondolewa hasa kwenye maduka ya vyombo vya ulinzi na usalama. Hivi vyombo vya ulinzi na usalama vilikuwa vimezoea maduka hayo na tozo hiyo imeondolewa hasa baada ya kuonekana kuna misuse kwa hao ambao wamepewa hizo zabuni za kupeleka vyombo hivyo. Nimesoma hotuba lakini haielezi mbadala kwamba ni shilingi ngapi watapewa hawa maaskari au walinzi wetu ambao wapo kwenye vyombo hivyo badala ya kununua hivyo vitu kwenye maduka. Kwa hiyo, ningeomba suala hilo pia liangaliwe litakuwaje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia pia suala la makato ya kodi za Wabunge lakini nimeliona kwamba halina mashiko kwa sababu halina basis. Kama suala hili la viinua mgongo vya Wabunge ambalo inatakiwa likatwe kodi mwaka 2020 sielewi kwa nini limeletwa wakati huu wa 2016. Ni vizuri suala hili likaletwa kwenye bajeti ya 2019/2020. Hapo ndiyo tunaweza tukalijadili kwa kina. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kumalizia kwa ushauri. Ukiangalia taarifa ya Kamati ya Bajeti inaonekana kuna msuguano au hakuna maelewano yaliyokuwepo kati ya Wizara na Kamati ya Bajeti. Ni vizuri wakikaa na kuona wanaweza kulitatua namna gani na kuangalia mawazo ya Kamati ya Bajeti ambayo wameyatoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimefarijika kuona kwamba bajeti hii isiwe tegemezi kwa wafadhili. Nimeona kwamba hela za nje ambazo zimetengwa ni shilingi trilioni 3.12 lakini ni vizuri kabisa kwenye bajeti ambazo zinakuja tujaribu kujifunza, tujaribu kuelewa kwamba tusitegemee fedha za wafadhili ambazo zinakuja na masharti kemkem. Kwa hiyo, ni vizuri kabisa katika bajeti hii hela za wafadhili ni kidogo, lakini katika bajeti zinazokuja suala hili linatakiwa tuliondoe moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kushauri ni hizi fedha ambazo zimetengwa. Tunategemea kwamba fedha hizi zitakapopitishwa na Bunge hili fedha hizo zote ziwe zinafika kwenye Wizara kama zilivyopitishwa. Vinginevyo kama zitakuwa zinakwenda nusu nusu au mwishowe unakuta kwamba fedha hizo hazifiki itakuwa ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia napenda waangalie hili suala ni kwa nini nchi yetu hatuwezi kutumia currency ya kwetu. Currency zinatumika hovyo hovyo tu, unaweza ukawa na dola au pound unakwenda hapo nje unabadilisha tu, wenzetu hawatumii hivyo. Naamini restrictions ambazo wenzetu wameziweka zinakuza uchumi kwa sababu tutatumia currency yetu. Kwa hiyo, naamini kabisa tutakapotumia fedha zetu tutakuwa na uwezo wa kukuza uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ningependa kuunga mkono hoja na nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii.