Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Moshi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, malalamiko ya waendesha utalii wa ndani (local investors) kuhusu gharama kubwa ya leseni yashughulikiwe. Waendesha utalii wa ndani wanaoomba leseni TALA kwa uwekezaji wa ndani iwe dola za Kimarekani 500 badala ya dola 2,000. Hii itasababisha Serikali kupata mapato zaidi kwa vile mzunguko wa fedha utabaki ndani tofauti na sasa ambapo fedha nyingi zinabaki nje kutokana na kampuni nyingi za kitalii kumilikiwa kwa ubia na wageni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maslahi ya waongoza watalii na wapagazi bado ni duni sana, mikataba yao ni mibovu na mazingira yao ya kufanyia kazi ni magumu. Serikali ni vyema isimamie Sheria ya mwaka 2008 iliyotangazwa katika GN mwaka 2008 ambapo pamoja na mambo mengine sheria hiyo itasimamia usajili wa waongoza watalii na kuwapatia leseni; ambapo mapato yataongezeka kwa Serikali kuwa na takwimu za waongoza watalii. Kuwe na waongoza watalii wanaokidhi vigezo na kuongezeka kwa watalii kwa kuwa huduma itakayotolewa itakuwa ina ubora na inakidhi viwango vya utalii wa ushindani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kukomesha wageni ambao wanafanya kazi ya kuongoza watalii, Serikali inaelewa kwamba ni kinyume cha sheria kwa wageni kuongoza watalii. Aidha, kumekuwa na volunteers ambao wanaingia nchini na kuingiza watalii kwa kuwalaza katika malazi bubu, hali hii huchangia kudumaza utendaji wa hoteli zetu katika Mji wa Moshi na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mpango wa kuboresha njia za kupandia Mlima Kilimanjaro, mfano ni njia ya Machame, ni vyema kukawa na namna bora ya KINAPA kutengeneza tent za kulia (mess tent) zinazofanana ili kutunza mazingira kuliko kuacha kila muendesha biashara ya utalii akajenga tent lake la kulia. Hivyo, nashauri njia ya Machame katika camp ya Machame Hut patengenezwe uniformity plan ya kujenga ma-tent yanayofanana na yenye kiwango kizuri kinachovutia kwa ajili ya wageni kupata chakula. Machame Hut iwe kama pilot na njia nyingine zitafuata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuongeza mapato kwa kuagiza TRA wawe na maafisa wao ambao watakaa kwenye lango la mlima kukagua tax clearance za wenye makampuni ya utalii ili kulinganisha taarifa za usajili wa makampuni hayo na uhalisia wa kodi wanazolipa. Tatizo kubwa lililopo ni kwamba makampuni yanakuwa na leseni lakini yanakuwa ni makampuni ya nje yanayotumia baadhi ya waongoza watalii kujificha katika hicho kivuli chao na hivyo kukwepa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii wa Mlima Kilimanjaro kwenda sambamba na hali ya uchumi ya wananchi wa Kilimanjaro, hususan wananchi wa Manispaa ya Moshi. Nashauri Serikali kuona jinsi ambavyo itakubali ombi la Manispaa ya Moshi kuwa Jiji kwa vile ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete kwa wananchi wa Moshi, jambo ambalo lilisababisha Manispaa ya Moshi kuanza mchakato wa kuhamasisha maeneo ya vijiji na kata jirani ili wakubali wazo la Manispaa ya Moshi kupanukia katika maeneo yao. Jambo la kusikitisha baada ya mchakato huo uliotumia fedha za ndani za Halmashauri, Serikali haijaleta majibu mazuri ya kuridhisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa Manispaa ya Moshi kuwa Jiji ni kuinua thamani ya mlima ambapo watalii wataiona Moshi kama Jiji la Mlima Kilimanjaro, hivyo kusaidia kuongeza idadi ya watalii wanaofika Moshi na Kilimanjaro kwa ujumla na hatimaye kuhamasisha watu kuwekeza kwenye miundombinu ya utalii na hivyo kukuza uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro ambao umeanguka kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja wa ndege wa Moshi ni lazima uboreshwe. Hoja kwamba Kilimanjaro kuna uwanja wa KIA haitendei haki utalii wa Mlima Kilimanjaro ambapo uwanja wa Moshi ungetumika vizuri ungeweza kupokea ndege ndogo kutoka Mbuga za Serengeti na mbuga nyingine za wanyama za Kanda ya Kaskazini. Aidha, uwanja wa ndege wa Moshi unaweza kupokea ndege ndogo moja kwa moja kutoka Kenya, vilevile unaweza kusaidia kupokea helkopta za uokoaji katika Mlima Kilimanjaro kwa wale watalii wanaopata shida za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii wa utamaduni unaweza kufanyika Moshi kwa kujenga Jumba la Makumbusho (Museum) ambalo litatunza historia ya watu wa Mkoa wa Kilimanjaro, hivyo kutumika kama eneo la kuvutia watalii kabla na baada ya kupanda Mlima Kilimanjaro.
Aidha, Msitu wa Rau katika Manispaa ya Moshi unafaa kutumika kama eneo la kivutio cha watalii kwa vile lina aina za miti ambayo haipatikani maeneo mengi duniani. Hivyo, ni vizuri ikawa kama recreational centre.