Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka zake tele.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Serikali ningependa kuanza kwa kumpongeza Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Pia kwa niaba ya wafanyakazi wote nchini nipende kuishukuru Serikali, Serikali zote mbili iliyokuwa ya Awamu ya Nne na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa wasikivu na kusikiliza kilio cha wafanyakazi cha muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Nne wafanyakazi wote nchini tunaishukuru sana kwa kukubali kuanzisha Sheria ya Mfuko wa Fidia (Workers Compensation Fund) Sheria Na. 8 ya mwaka 2008 na kuachana na ile Sura Na. 263 kwa Private na Public Service Act Na.19 kwa upande wa wafanyakazi wa utumishi wa umma kutumika kufidia once wanapoumia ama kupata ulemavu mahali pa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano tunaishukuru kwa kukubali kuwasilisha michango ya mwajiri ya 0.5 percent ya mshahara katika Mfuko huu wa Fidia ili itakapofika tarehe Mosi Julai, mwaka huu wafanyakazi wote watakaoumia ama kupata ulemavu kazini wataenda kufidiwa na Mfuko huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena kwa niaba ya wafanyakazi wote nchini, tunaishukuru sana Serikali tena sana kwa kuja na jambo hili jema la kuanzisha huu Mfuko. Nipende tu kusema kwa kuanzisha Mfuko huu automatically tunaongeza muda mrefu wa wafanyakazi kuwepo kazini, lakini pia tunaongeza uzalishaji, kitu ambacho kitaenda kuchochea ukuaji wa uchumi wetu na hali kadhalika pato la Taifa letu litakua. Ni ukweli usiopingika Serikali inapata kodi yake ya uhakika pasipo kusuasua kutoka katika kundi hili la wafanyakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nipende kuipongeza Serikali kwa kupunguza kodi ya Pay As You Earn hadi kufika single digit kwa wafanyakazi wa kima cha chini. Napenda kuiomba Serikali na niliuliza hapa swali katika Bunge lako Tukufu kwamba, je, Serikali ina mpango wowote ama ina mpango gani kwenda sasa kupunguza hii kodi ya Pay As You Earn kwa wafanyakazi wa kima cha juu wanaokatwa 30%.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya wafanyakazi au watumishi wa nchi hii Mheshimiwa Angellah Kairuki alitupa majibu mazuri sana kwamba tayari Workers Task Force imeshaundwa na inayafanyia kazi haya mapendekezo na tayari yamepelekwa kwenye Baraza la Majadiliano la Utumishi wa Umma wanayafanyia kazi na muda wowote wataturudishia feedback, naamini feedback itakuwa njema.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu Serikali kwa mwaka 2017/2018, ione sasa umuhimu wa kuwapunguzia kodi hawa watumishi wa umma ama wafanyakazi wanaokatwa kima cha juu ili kuwapunguzia makali ya maisha na kama nilivyozungumza hili ndilo eneo ambalo Serikali inapata kodi yake ya uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa tatu ni kuhusiana na afya ama vituo vya afya katika Halmashauri zetu. Kiukweli uwezo ama hali ya Halmashauri zetu katika ujenzi wa hivi vituo vya afya, zahanati ama niseme majengo ya wazazi hali yao haiko vizuri, wanatumia own source na yenyewe wanaipata kwa kuhangaikahangaika. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa ku-windup aweze kutueleza kiukweli kabisa kwa sababu hizi Halmashauri zinajaribu kuingia kwenye huu ujenzi wa hivi vituo vya afya ama majengo ya wazazi wanafikia usawa wa lenta, kupaua wanashindwa, yale majengo yanabakia kama magofu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikitolea mfano katika Halmashauri yangu ya Wilaya ya Kibaha katika Kata ya Magindu kuna jengo la wazazi pale tangu mwaka 2012 mpaka leo hii 2016 ninavyoongea halijakamilika na wala halina dalili ya kukamilika. Tunahitaji shilingi milioni 26 tu ili kuweza kulikamilisha jengo lile, wanawake wa Kata ya Gwata na Kata ya Magindu waweze kutimiza haki yao ya msingi ya kuleta watoto hapa duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana kumwomba Mheshimiwa Waziri alione hilo, tunazihitaji hizo shilingi milioni 26 ili tuweze kuwasaidia wanawake hawa ambao ni wapiga kura wetu lakini hali kadhalika niseme ni walezi wa watoto wa Taifa hili. Hii shilingi milioni 26 kwa ajili ya kumalizia hiki kituo tumeanza kuiomba tangu mwaka wa bajeti 2014/2015 hakuna kitu, 2015/2016 hakuna kitu, 2016/2017 nimechungulia hakuna kitu. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri atufikirie na atuonee huruma na hili suala lifike mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine uko katika hili suala zima la private number. Hapa pengine Mheshimiwa Waziri atakuja anipe shule lakini nikiangalia kwa uelewa tu wa kawaida sasa hivi katika gari yangu nimeandika Mchafu nalipa shilingi milioni tano, lakini anasema kwamba anatutoa kwenye shilingi milioni tano anatupeleka kwenye shilingi milioni 10. Katika hali tu ya kawaida ambayo wala haihitaji akili nyingi, mimi nasema tunaenda kupunguza mapato na siyo kwamba tunaenda kuongeza mapato. Kwa sababu ni hiari ya mtu, naweza nikaamua kuacha jina langu Mchafu na nikaenda nikarudi kwenye Na. T302 BZZ.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo nitapenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja anifundishe kutoka kwenye hii shilingi milioni tano kwenda kwenye shilingi milioni 10 anaongezaje mapato ilhali hili jambo ni hiari na siyo lazima. Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuzungumza nitaomba aje anifafanulie suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni kuhusiana na suala zima la kuongeza tozo ama kuweka tozo kwa bidhaa za mitumba. Nilitoka kuuliza swali hapa asubuhi Watanzania milioni 12 ni maskini wa kutupwa, kila mwaka vijana takribani laki nane wanaingia kwenye soko la ajira, je, Serikali kwa mwaka inatengeneza ajira ngapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna vijana wengi ambao ni hawa tunawaita Machinga, wanafanya kazi ya kutembeza hizi nguo za mitumba ili waweze kupata riziki na familia zao. Leo ukiweka tozo kwa lengo la kuizuia hii mitumba, niulize hivi viwanda vitakavyotengeneza nguo kutuvalisha Watanzania viko wapi? Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri jambo hili alifikirie mara mbili, je, tupo tayari kuongeza hizi tozo kwenye mitumba hivyo viwanda viko tayari? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni kuhusiana na CAG, wengi wamesema na mimi lazima nilizungumzie hili. Halmashauri zetu uaminifu wao ni wa kulegalega, CAG ndiye mkombozi mkubwa ambaye ameweza kutusaidia, CAG ndio jicho ambalo limeweza ku-penetrate na kuweza kuona kuna watu wanalipwa mishahara hewa, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri na niungane na wenzangu wote waliosimama hapa kuzungumzia suala zima la CAG kuongezewa pesa, hebu akae afikirie mara mbili mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema bajeti yetu ni shilingi trilioni 29 na hela hizo hatuna in cash, ndiyo tunataka twende tukazikusanye sasa kama CAG tunamwekea hela kidogo namna hiyo atakwenda kufanya kazi gani? Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri afikirie tena na tena kuhusiana na suala zima la CAG, aone namna bora ya kuweza kumuongezea pesa ili aweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki unigongee kengele, napenda kusema nakushukuru sana na naunga mkono hoja.