Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii kuchangia bajeti hii ya Serikali ya Awamu ya Tano ya 2016/2017. Kwanza napenda kukupongeza wewe mwenyewe Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Fedha, Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa ndani ya Bunge hili. Vile vile napenda kutoa shukrani nyingi kwa wapigakura wangu wa Jimbo la Kahama kwa kunipatia kura nyingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita sehemu moja ya kuongeza mapato. Ni sehemu ngumu kidogo, lakini naomba nichangie na naomba Waziri wa Fedha kama anaweza kunisikiliza ni vizuri akanisikiliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ya Tanzania imezungukwa na nchi nyingi ambazo zina madini na maliasili nyingi na nchi hizi zinategemea nchi yetu ya Tanzania kupitishia madini haya na maliasili hizi. Vile vile zinategemea kuuza nchi za nje kupitia hapa kwetu. Ninachoomba kwa Waziri wa Fedha, kama anaweza kutukubalia, nitatoa mfano wa nchi ya Burundi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi ya Burundi imekuwa iki-export dhahabu tani tatu mpaka tani nne kwa utafiti unaoonesha, lakini nchi hii ina migogoro mingi ya vita na haina machimbo au mgodi wowote wa dhahabu, lakini sisi nchi yetu ina amani, ina dhahabu nyingi, imezungukwa na nchi nyingi kama Congo, Mozambique; nchi hizi zote zinataka kuuza madini yao hapa. Kuna madini ya almasi, nickel, copper, aluminium na madini zaidi ya 50.
Mheshimiwa Naibu Spika, na madini haya sisi si watumiaji. Tungeomba kwenye bajeti hii, kwa kuwa haiingiliani na bajeti hii, Mheshimiwa Waziri wa Fedha kama atakubali yaruhusiwe yawe zero wakati wa ku-export yawe one percent. Kwa hesabu ya harakaharaka Tanzania inaweza kupata kwa wiki tani mbili na nusu za dhahabu, maana yake kwa mwezi tutapata tani kumi na mbili na nusu zikiwa za sisi nyumbani na za watu wa nje. Kama tuta-charge kwa one percent kwa bei ya leo ya Dola 40 kwa gram au Dola 40,000 kwa kilo, tutapata zaidi ya Dola milioni 500. Dola milioni 500 kwa exchange ya harakaharaka ni trilioni moja kwa mwezi, hiyo ni kwa madini ya aina moja. Tukichukua madini mengine haya yaliyobaki yanaweza kutuchangia zaidi ya bilioni 900 kwa mwezi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukichukua one percent pia kwenye hiyo tutakuwa karibu tuna bilioni tisa kwa mwezi. Kwa hiyo, total itakuwa na bilioni 20 kwa mwezi na pesa hii haiingiliani na Bajeti ya Serikali, ni pesa ambayo ipo tukikataa au tukikubali yenyewe iko vile vile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, attendance ya watu hawa wakija kuuza madini lazima asilimia 20 ya pesa zao wafanye shopping hapa. Kama watafanya shopping asilimia 20, maana yake watatuachia sisi bilioni 400. Bilioni 400 maana yake tutakua sisi kwa asilimia 18 ya VAT ya vitu vilivyoingia nchini ambavyo watanunua hapa, Serikali itakuwa imepata bilioni 40 tena zaidi. Kwa hiyo, madini haya yatakuwa yametuchangia zaidi ya bilioni 70 kwa mwezi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna mahali ambapo Bajeti ya Serikali itakuwa imeguswa. Ni kiasi cha Waziri wa Fedha kusema kesho kwamba, sawa amekubali na watu hawa wanaanza kupita. Maana yake hata bila kukubali au namna gani hawa watu wanaendelea kupita hapa, wanahangaika kutoka hapa mpaka Dubai kwenda kuuza; kutoka Congo mpaka Dubai ni karibu masaa tisa, lakini kuja hapa ni masaa mawili. Kwa hiyo ingekuwa vizuri Waziri wa Fedha akaliangalia sana suala hili. Suala hili ndio utajiri wa hawa tunaowaomba pesa leo na ndio wanaotunyanyasa, lakini pesa zote zimetokana na njia hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, madini haya, sisi hatuyatumii, yanakwenda yote Ubeligiji, yanakwenda Dubai, yanakwenda Singapore, yanakwenda China, yanakwenda Hong Kong na mwisho wake sisi tunakwenda kuwaomba pesa wao. Ingekuwa vizuri, tukarekebisha sera yetu ili madini haya yaweze kutusaidia sisi hapa na jirani zetu waweze kugeuza hapa kuwa Dubai ya kwao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote, kwa madini haya tutapata wageni zaidi ya 10,000 kwa mwezi. Wageni hawa ni wageni ambao wana pesa, maana yake hakuna mtu anayebeba madini akiwa hana pesa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatarajia Sekta zote zitapata pesa kuanzia Usafirishaji, TRA, Uhamiaji, maduka, nyumba za kulala wageni, zote zitapata pesa na itatusaidia vile vile, kutuongezea na kutufungulia mlango mpya wa biashara ambao sisi hatukuwa nao. Sisi tumeelekeza zaidi kwenye utalii na nafikiri huu unaweza kuwa ni utalii mpya. Kwa namna hiyo, inaweza ikamsaidia Waziri wa Fedha akawarudishia na Wabunge pesa tunazozozana hapa za posho kama ataweza kukubaliana na wazo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa leo mchango wangu ni huo, asante sana na naunga mkono hoja.