Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Katavi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hotuba ya Wizara ya Utalii ambayo imesheheni mipango mizuri ya utalii nchini ili kuongeza Pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi halali na wawindaji nchini, kuhusiana na wavuvi ambao wapo katika maeneo yenye mito, maziwa, mabwawa na bahari, naomba hawa wavuvi leseni zao zichunguzwe upya maana kumekuwa na malalamiko mengi kwa wageni kuingia nchini kwa lengo la utalii na kumbe baadhi yao wanavuka mipaka ya kilichowapeleka katika maeneo ya utalii, hawana vibali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na matatizo mengi sana ya ujangili katika mbuga zetu. Serikali imejipangaje kuhusiana na kudhibiti hawa wawindaji halali wanaoingia kama watalii katika mbuga zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike, Serikali ichunguze ni namna gani ya kudhibiti hawa watalii na siyo kuwaacha peke yao mbugani. Wanafanya nini hasa maana tumeona ujangili mwingi umekuwa ukifanyika na wanaokamatwa wengi ni wageni. Hivyo, Serikali iongeze vitendea kazi kama magari kwa ajili ya kufanya patrol ndani ya mbuga zetu, kuwapa silaha zenye uwezo askari wa wanyamapori. Pia Serikali iboreshe maslahi ya askari wa wanyamapori ili wafanye kazi kwa moyo na kuwazuia kufanya biashara haramu (pembe za ndovu).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwekezaji ndani na mbuga, kumekuwa na malalamiko mengi kwa baadhi ya mbuga kwamba wawekezaji hawa wanaajiri watu wengi ambao ni wageni kutoka nchi jirani na maeneo kama Pakstani, Wahindi na Wazungu. Je, Serikali haioni kwamba kwa kuendelea kuwapa uhuru hawa wawekezaji kuajiri wageni zaidi kuliko wazawa ambao wapo wenye uwezo na elimu kuweza kuhudumia mfano hoteli zilizopo mbungani, customer services na madereva. Shughuli hizo wangeweza kufanya wazawa kwa wingi kuliko wageni wanaoletwa kuchukua fursa hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbuga ya Katavi ichungwe zaidi. Je, ni jinsi gani wawekezaji hawa wanasaidia wakazi wa vijiji vya jirani kwa huduma kama maji, zahanati, barabara na madawati? Wawekezaji hawa wanaingiza vipato vikubwa hivyo wanapaswa pia kusaidia jamii inayowazunguka katika mbuga hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanja vya ndege, kutokana na uhaba, ukosefu wa vifaa vya kisasa kama kamera katika viwanja vya ndege inachangia kutoroshwa kwa rasilimali zetu mfano ndovu, vyura na kadhalika. Hivyo, Serikali ihakikishe inawezesha upatikanaji wa vitendea kazi bora kama kamera, mashine za ukaguzi, x-ray na screening machine. Nini kifanyike? Ulinzi uongezwe zaidi hasa katika viwanja vya ndege ambavyo viko ndani ya hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia kwa waathirika wa Operesheni Tokomeza Serikali iangalie namna gani ya kufidia watu walioumizwa, kuibiwa na kupigwa. Mfano katika Mkoa wa Katavi, Wilaya ya Mpanda Vijijini, Kata za Isengule na Kapalamsenga, askari polisi walijeruhi watu ambao hata hawahusiki. Je, Serikali ina mpango gani wa kushughulikia suala hili?