Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Joyce Bitta Sokombi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu fidia ndogo kwa wakazi wanaoishi karibu na hifadhi na Serikali kushindwa kuwadhibiti tembo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnyama akimuua mtu au binadamu fidia yake ni ndogo sana. Familia inalipwa shilingi 100,000 au wasipate kabisa kutokana na figisufigisu za viongozi wa eneo husika; lakini endapo mtu akikutwa kaua wanyama, fidia anayotozwa ni kubwa sana na ni kuanzia shilingi milioni sita na zaidi. Swali la kujiuliza je, kipi kina thamani kati ya binadamu na mnyama? Maana hii inaonyesha moja kwa moja kuwa Serikali yetu inathamini wanyama kuliko binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali, iangalie sheria hii kwa umakini, kwani haiwezekani hata siku moja mnyama akawa na thamani kuliko mtu au binadamu. Ni vizuri wananchi wa eneo husika wapewe elimu ya kutosha juu ya fidia wanazostahili kulipwa maana kila mwananchi akijua juu ya umuhimu wa malipo wanayostahili kulipwa, naamini hakutakuwa na kelele kuhusiana na jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakazi wanaoishi karibu na maeneo ya mbuga au hifadhi wananyanyasika sana utafikiri watu hawaishi katika nchi yao (wakimbizi). Wananyanyaswa, wanafukuzwa kwenye maeneo yao wakati Serikali haijawaandalia maeneo ya kwenda kuweka makazi hayo. Ina maana wakati wananchi hao wanajenga, Serikali ilikuwa wapi? Ina maana ilikuwa inawaangalia tu wanapomaliza ndiyo iwaambie wananchi kuwa wamevamia hifadhi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza sana na inasikitisha pia. Inabidi Serikali iwaangalie kwa upya wananchi hawa kwani wanaishi kwa hofu kubwa na maeneo hayo ni Maliwanda, Mihale, Mcharo, Serengeti, Hunyali, Kunzugu na Balili, hivyo vyote ni vijiji vya Wilaya ya Bunda. Kwa upande wa Serengeti ni Merenga, Machochwe, Nyamakendo, Mbalibali, Tamkeri, Bisarara, Mbilikiri, Bonchungu na Robanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshindwa kuwadhibiti wanyama (tembo) wanaoharibu mazao ya wananchi bila kujali hasara wanayoipata wananchi hao. Kwanza kabisa bila kuwadhibiti tembo hao umaskini hautaisha, kila siku wananchi hawa wataendelea kuwa ombaomba kutokana na umaskini unaotawala kutokana na mazao yao kuliwa na tembo au kuharibiwa na tembo ama wanyama wengine waharibifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Serikali ikajipanga upya juu ya jambo hili la kuwadhibiti tembo ili wananchi wanapolima mazao yao wavune na kupata chakula na wananchi wengine wanahamia ili wapate kuvuna mazao yao na kuyauza kwa ajili ya kusomesha watoto wao, lakini tembo wanamaliza mazao ya wananchi kabla hawajavuna na kuendelea kuwadidimiza wananchi hawa kuwa maskini. Ninaamini Mheshimiwa Waziri atalishughulikia suala hili kwa ukaribu ili kuwasaidia wananchi hawa.