Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkutano wa Bunge la Kumi kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali ilianzisha kauli mbiu isemeyo; “Utalii Uanze kwa Mtanzania.” Pamoja na kauli hii kuonesha msisitizo kwa Watanzania kuweza kujivunia na kunufaika na sekta hii, bado zaidi ya robo tatu ya Watanzania hawanufaiki hata kidogo na sekta hii ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli hii iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo, ni hadaa kubwa kwa Watanzania. Inajulikana bayana kwamba kima cha chini cha mshahara wa Mtanzania hakizidi shilingi 300,000. Kutembelea mbuga zetu ni lazima kila Mtanzania kuchangia kiasi cha shilingi 5,000 mpaka shilingi 15,000, lakini pamoja na mchango huu, kama Mtanzania atalazimika kulala mbugani katika hoteli kwa usiku mmoja itamlazimu kulipa gharama mara mbili zaidi ya mshahara huo kwa kima cha chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema Watanzania wakafahamu kuwa Mtanzania anapotaka kwenda mbugani kwa siku mmoja tu inagharimu dola za Kimarekani takribani 145 sawa na fedha za Kitanzania shilingi 316,825 kwa exchange rate ya shilingi 2,185. Hii ni kwa hoteli yenye gharama nafuu zaidi mfano Rhino Lodge. Gharama hii haijahusisha chakula wala huduma nyingine yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayojipambanua na kauli ya Hapa Kazi Tu kwa nini isingeona umuhimu wa kuvaa viatu vya wananchi hawa wa kipato cha chini na kuona ilivyo kazi kuweza kuishi kwa kiasi hicho cha fedha kitakachomfanya Mtanzania huyu aweze na yeye kujisikia sehemu ya kulinda na kuzifahamu mbuga zetu? Ni kwa nini Serikali isifike mahali ikaona umuhimu wa dhati kuweza kumsaidia Mtanzania huyu kuweza kujisikia kuwa sehemu ya rasilimali zilizo ndani ya nchi yake kwa kuweka mazingira nafuu zaidi kwa bei ambayo Watanzania wengi wataweza kulipia na kufurahia mandhari mazuri ya mbuga zetu? Ni vyema sasa tukaaza kujivunia vya kwetu kwa vitendo ili basi Watanzania wasiwe ni watu wa kusimuliwa au kuona mandhari ya mbuga zetu kwenye runinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali inafumbia macho malipo yanayofanywa kwa fedha za kigeni hasa kwenye sekta ya utalii? Mara nyingi tumekuwa tukilizungumzia suala la matumizi ya dola katika mzunguko wa fedha hapa nchini, lakini ni kwa nini Serikali haichukui hatua?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, Mtanzania anayeamua kufanya utalii wa ndani na kuamua kulala kwenye hoteli zilizopo ndani ya mbuga, hasa zile zilizoko kwenye Hifadhi ya Ngorongoro, Serengeti na hata hoteli kubwa za Zanzibar, ni lazima afanye malipo kwa dola. Katika hali ya kawaida, ni Watanzania wangapi wanamiliki dola katika uchumi wao? Hii ina maana kwamba ni lazima wabadili fedha zao katika maduka ya kuuza fedha ili waweze kufanya malipo. Ifike mahali hasa Serikali ijitathimini. Ukienda nchi za wenzetu walioendelea, mfano, Norway, Switzerland, German na nyingine, huwezi kununua kitu kwa fedha ya kigeni. Wanathamini fedha yao zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni aibu na ni fedheha kubwa kwa Serikali kuendelea kushiriki katika michezo ya kuua thamani ya shilingi yetu kwa kuruhusu makampuni haya kuendelea kufanya tozo mbalimbali ndani ya nchi kwa fedha za kigeni. Serikali ije na sera lazimishi ya kuhakikisha kuwa fedha yetu inatumika. Wageni waweze kununua fedha yetu ili tuwe na akiba ya dola. Tunawezaje kufikia ndoto ya kuwa na uchumi na kati wakati sisi wenyewe ndiyo tunadidimiza thamani ya shilingi yetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza sana kuwa booking za hoteli za kitalii kwenye hifadhi za nchi hii zinazofanywa kupitia kwa mawakala walio nje ya nchi yaani ukitaka kupata nafasi ya hoteli unapiga simu Afrika Kusini au Nairobi kwa Wakala ambaye yeye ndio atakupa nafasi au laa. Tunataka kujua ni kwa nini jambo hili linafanywa kwa namna hii? Ni kwa nini booking zote za hoteli zilizopo hapa nchini zisifanyike kupitia mawakala waliopo ndani ya nchi yetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati sasa Tanzania kuweza kuthamini vitu alivyotupa Mwenyezi Mungu. Inasikitisha sana kuona vyura wa kipekee kabisa duniani hawapewi nafasi ya kutosha kuweza kufahamika kwa wananchi wetu. Vitu hivi vya kipekee kabisa ambavyo duniani kote hakuna, mfano wa vyura hawa wa Kihansi wanaozaa na kunyonyesha, ni dhahiri kabisa tunakuwa hatuwatendei haki wananchi wetu na hata watoto wetu ambao watakuwa watu wazima na hawaifahamu nchi yetu na vivutio vyetu vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ije na mpango mkakati wa kuhakikisha vyura kama hawa ambao ni amphibia, pamoja na malikale nyingine zinaingizwa katika mitaala mbalimbali ili watoto wetu waweze kuvifahamu vizuri.